Pages

Friday, July 20, 2012

JWTZ : :Wito wa Adhabu ya Viboko Wakati wa Mafunzo Haukubaliki

JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA

19 Julai, 2012

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linapenda kutoa taarifa kwa vyombo vya habari na wananchi wote kwa ujumla kuwa, wito uliotolewa na baadhi ya magazeti nchini tarehe 18 Julai 2012 kwamba Jeshi litumie nguvu na viboko wakati wa mafunzo kwa Maafisa na Askari, haukubaliki. Kwa mujibu wa Kanuni za Jeshi na Sheria za Ulinzi wa Taifa, Afisa au Askari akitumia viboko ni kosa la jinai, atashitakiwa chini ya kifungu C.32 na akipatikana na hatia anaweza kufungwa kwa kipindi kisichopungua miaka miwili jela. Tunapenda kunukuu kifugu hicho, “C.32 Every serviceman who strikes or otherwise ill-treats any other serviceman who by reason of rank or appointment is subordinate to him is guilty of an offence and on conviction is liable to imprisonment for a term not exceeding two years or less punishment”.

Aidha, tungependa kueleza kwamba kanuni hiyo inatumika kwa wanajeshi waliopo JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa. Yeyote atakayepata taarifa ya kupiga wanafunzi, aziwasilishe Makao Makuu ya Jeshi (MMJ) ili kuchukua hatua sahihi, kwani si mila na desturi za Jeshi. Tunazo njia za kitaalam za kuwafunza na kuwakomaza wanajeshi wetu siyo kwa viboko kwani huo ni udhalilishaji, hivyo ni batili.

JWTZ linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa, kazi ya Jeshi ni ya kitaalam na mafunzo ya zama hizi ya kijeshi yameendelea kuboreshwa kila wakati na huendeshwa kisayansi, ili kutoa elimu inayoendana na karne hii. Kutokana na mafunzo hayo, Maafisa na Askari wa JWTZ wamekuwa wakifanya vizuri sana hata wanapopewa majukumu nje ya nchi kwa mfano kule Lebanon na Darfur. Majeshi yetu yamepata sifa kubwa na chimbuko lake ni mafunzo mazuri.

Mwisho, ushauri huo wa kutumia nguvu katika mafunzo ya JWTZ kama ulivyotolewa na baadhi ya magazeti haukubaliki kwa vile unaenda kinyume na maadili ya kijeshi, Kanuni na Sheria za Ulinzi wa Taifa na pia haki za binadamu. Hatukubaliani na kilichoandikwa kwenye magazeti hayo, kwa misingi ya kijeshi na kibinadamu kwamba ukufunzi wa aina hiyo haukubaliki. Ushauri wa namna hiyo upo nje ya taratibu zetu. Msimamo wa JWTZ ni kuendelea kutumia mbinu za kisayansi katika kuwafunza Maafisa na Askari wake.

Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
SLP 9203, Simu: 0764 742161

Email:
ulinzimagazine@yahoo.co.uk

Popular Posts