Pages

Wednesday, August 15, 2012

Hotuba Kambi ya Upinzani - Wizara ya Fedha na Uchumi 2012 / 2013

Dondoo muhimu za hotuba hii:

Mafuta yala dhahabu yote, korosho na viwanda

2.1 Mauzo ya Nje

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuhakikisha kuwa Akiba ya Fedha za Kigeni nchini inakuwa imara muda wote. Biashara ya nje ndio inaingiza Fedha za kigeni nchini kwa hiyo ni eneo la kutazama kwa makini na kuchukua hatua mwafaka. Taarifa ya mwenendo wa uchumi kwa mwezi Julai iliyotolewa na Benki kuu inaonyesha kuwa jumla ya mauzo ya Tanzania nje yalikuwa dola za kimarekani 7,990.0 milioni ukilinganisha na kiasi cha dola 7,050.7milioni kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2011 na hali hii ilisababishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa bei ya mauzo ya dhahabu. Hata hivyo Manunuzi yetu kutoka nje yamefikia dola za Kimarekani 12,959 milioni.

Mheshimiwa Spika
, taarifa hiyo inaonyesha kuwa mauzo ya dhahabu Nje kwa mwaka 2011 yalikuwa kiasi cha dola 2,330.7 milioni sawa na aslimia 56.7% ya mauzo yote nje, wakati mauzo ya nje kutokana na bidhaa zilizozalishwa viwandani yalikuwa na jumla ya dola 922.0 milioni sawa na asilimia 22.4% ya mauzo yote ya nje. Aidha mauzo ya mazao mbalimbali kama Pamba, Katani, Korosho, Chai, Kahawa na mengineyo yalikuwa na thamani ya dola 761.1 milioni kwa kipindi hicho cha mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika
, taarifa hiyo imeendelea kuonyesha kuwa tuliagiza bidhaa kutoka nje zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 12,958.7. Katika manunuzi hayo tuliyofanya mafuta peke yake yalikuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni3,586.1 ambalo ni ongezeko la asilimia 60.08% ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka 2011.

Mheshimiwa Spika
, takwimu hizi zinaonyesha kwamba fedha zote za kigeni zilizotokana na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani na Korosho zilitumika kuagiza mafuta pekee yake! Hali hii ni mbaya sana kwa uchumi wa Taifa letu na juhudi zote za kuongeza mauzo nje zinaliwa na uagizaji wa Mafuta ambao umepanda sana katika siku za hivi karibuni.

Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa kuanzia mwaka jana Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa Umeme wa dharura ambao umepelekea matumizi makubwa ya Mafuta. Hata hivyo ieleweke kuwa Mpango mzima wa Manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mitambo ya Umeme inaligharimu Taifa Fedha nyingi sana. Takwimu zinaonyesha kuwa Serikali inapaswa kutumia zaidi ya shilingi 42 bilioni kila Mwezi kuendesha mitambo ya dharura ya Umeme. Manunuzi yenyewe ya Mafuta yamejaa mazonge ya ufisadi uliokithiri. Licha ya kutaka Spika aunde timu ya kuchunguza ufisadi katika manunuzi ya Mafuta na licha ya Kamati ya Bunge kutaka Uchunguzi wa kibunge kufanyika katika manunuzi haya bado hakuna hatua inayochukuliwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Mamlaka ya Manunuzi ya Umma PPRA kufanya uchunguzi wa kina kuhusu manunuzi ya mafuta kuzalisha Umeme ambayo yanachoma bilioni 42 za Serikali kila Mwezi. PPRA hapaswi kufumbia macho manunuzi yanayotafuna shilingi 1.4 bilioni kila siku na yanayoongeza manunuzi ya nchi kutoka nje (imports) na hivyo kupoteza fedha za kigeni hovyo.

Mheshimiwa Spika,
Wizara ya Fedha ambayo ndio wizara mama ya PPRA kupitia Fungu 50, na ndio Wizara yenye kusimamia uchumi wa nchi kwa ujumla ituletee Bungeni Taarifa ya Uchunguzi utakaofanywa na PPRA kuhusu manunuzi shilingi 1.4 bilioni kila siku ya mafuta kuendesha mitambo ya kuzalisha Umeme.


TZS 70 Billion zalipwa kama mishahara hewa ilhali Walimu na Madaktari Wanalia


Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2012/2013, tulitaja kiasi cha shilingi bilioni 9[1] ambazo zililipwa kama mishahara kwa watumishi hewa kama ilivyoripotiwa na magazeti ya ‘The Daily News’ na ‘The Guardian’ ya Machi 23, 2011.

Mheshimiwa Spika, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya tarehe 31 Machi, 2012 inaonesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2010/2011 jumla ya shilingi 142,715,827.99[2] zililipwa kama mishahara kwa wastaafu, watumishi walioacha au kufukuzwa kazi na watumishi wengine ambao hawakustahili. Aidha, ripoti hiyo imeonesha kiasi cha shilingi 1,842,607,565.29 zilizolipwa kama mishahara hewa kwa mwaka wa fedha 2009/2010.

Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya fedha na uchumi ya tarehe 7 Agosti, 2012 ni kwamba uhakiki wa watumishi uliofanyika mwezi Januari, 2012 kwenye Halimashauri 133 na kwenye taasisi na wakala za Serikali 154 ulibaini majina 9,949 ya watumishi wasiostahili kuwemo kwenye orodha ya mishahara. Idadi hii ya watumishi hewa ni sawasawa na takribani idadi ya watumishi walioajiriwa katika sekta nzima ya madini kwenye migodi ya dhahabu hapa nchini. Watumishi hewa wanaokaribia 10,000 ni wengi mno na inaonyesha dhahiri namna Serikali isivyo makini katika suala hili ambalo linasababisha upotevu mkubwa wa Fedha za Umma.

Mheshimiwa Spika,
Waziri wa Fedha alikiri mbele ya Kamati ya Fedha na Uchumi kwamba mwezi Februari Serikali ililipa shilingi bilioni 5.1 kama mishahara hewa. Hii maana yake ni kwamba Serikali hutumia zaidi ya shilingi bilioni 70 kila mwaka kwa watumishi hewa wa Serikali.

Mheshimiwa Spika,
tunataka fedha hizi wanazolipwa watumishi hewa zitumike kuwalipa walimu na madaktari madai yao kwani ni nyingi na zinatosha sana. Siku zote sababu za Serikali kutotimiza matakwa ya wafanyakazi kwenye sekta ya Afya na Elimu ni kwamba Serikali haina Fedha. Lakini hapa tunashuhudia Shilingi bilioni 70 kila mwaka zikiteketea kulipa watumishi hewa ambao hawapo, hawafanyi kazi na hivyo kufaidisha mtandao wa kifisadi ambao kwa vyovyote vile unaanzia Wizara ya Fedha na Wizara ya Utumishi. Serikali inakosa vipi fedha za kulipa madai ya Walimu na inapata za kulipa watumishi hewa? Serikali inakosa vipi fedha za kulipa Madaktari na Manesi lakini inapata shilingi bilioni 70 kila mwaka kulipa watumishi hewa?

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka mradi huu wa watumishi hewa wenye mauzo (turnover) ya shilingi 70 bilioni kwa mwaka uvunjwevunjwe ili kupata fedha za kulipa Walimu na Madaktari. Waziri wa Fedha asambaratishe mtandao huu mwovu ambao sasa umeota mizizi kwenye Taasisi za Serikali. Vile vile Waziri agawe kwa Wabunge taarifa ya uhakiki wa wafanyakazi wa Serikali na pia hatua ambazo Serikali imechukua dhidi ya vinara wa mtandao wa watumishi hewa Serikalini.

[1] CorruptionTracker.or.tz
[2] Tazama Ripoti ya CAG toleo la Kiingereza uk.37


Sakata la rada Bado Bichi


2.5 MKOPO WA KUNUNUA RADA ILIYOGUBIKWA NA UFISADI


Mheshimiwa Spika, sehemu ya Malipo ya Deni la Taifa ni Mkopo ambao Serikali ilichukua ili kununua Rada kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza. Suala hili la rada limejadiliwa sana nchini kwa upande mmoja tu wa ufisadi wa kupandisha bei ya Rada na hatimaye kurejeshwa kwa iliyoitwa chenji ya Rada. Hiyo ilikuwa ni nusu tu ya ukweli kuhusu suala la Rada kwani Serikali ilikopa kiasi cha dola za kimarekani 40 milioni kutoka Benki ya Barclays ya Uingereza kwa ajili ya kununulia Rada. Mkopo huo ulikuwa na Riba ya asilimia 4.9 juu ya kiwango cha riba zinazotolewa na Benki ya Dunia au IMF.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama mkopo huu umeshalipwa wote na jumla tulilipa kiasi gani cha fedha. Ukilinganisha fedha iliyorejeshwa kama chenji ya Rada na Fedha ambayo Tanzania iliilipa Benki ya Barclays (Principal amount na Interest), je chenji ya Rada ilikuwa na thamani yoyote kifedha? Mjadala wa ununuzi wa Rada hauwezi kuisha kwa kufurahia kurejeshewa chenji tu. Mjadala huu bado mbichi kabisa kwani tunataka ukweli na ukweli mtupu uelezwe kwa umma na kuona Taifa lilipata hasara kiasi gani kwa ufisadi huu wa kimataifa na hatua stahiki za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote walioingiza hasara kwa Taifa letu.

FULL: Hotuba Kivuli ya Wizara ya Fedha.pdf
Download File

Source: http://www.wavuti.com/index.html#ixzz23bvh3zJl

Popular Posts