Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad  akizungumza na viongozi wa CUF kwa ngazi ya majimbo na Wilaya nne za  Pemba katika ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba. 
  Mwakilishi wa Jimbo la Ole Mhe. Hamad Massoud Hamad akizungumza na  viongozi wa CUFngazi ya majimbo na Wilaya nne za Pemba kilichofanyika  ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba. 
    Viongozi wa CUF ngazi ya majimbo na Wilaya nne za Pemba wakimsikiliza  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika  ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba. 
  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad  akisalimiana na baadhi ya viongozi wa CUF wakati akijiandaa kuingia  katika kikao cha viongozi wa CUF kwa ngazi ya majimbo na Wilaya nne za  Pemba kilichofanyika ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemb.Picha, Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
  --
   Makamu  wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar  Maalim Seif Sharif Hamad, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu  katika sensa ya watu na makaazi, ili kuirahishia serikali kupanga  mipango yake ya maendeleo kwa uhakika.  
   Maalim Seif ametoa wito huo leo katika ukumbi wa chuo cha Benjamin Mkapa  Wete Pemba alipokuwa akizungumza na viongozi wa CUF kwa ngazi za Wilaya  na Majimbo. 
    Amesema Sensa ya watu na Makaazi ni muhimu kwa wananchi na serikali kwa  ujumla katika kutathmini na kuandaa mipango yake ya maendeleo kwa  wananchi, na kuwataka kuachana na mtazamo kuwa suala hilo linaihusu  serikali pekee. 
    Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa msimamo huo kufuatia wananchi wengi wa  Kisiwa cha Pemba kuwa na mtazamo wa kutaka kususia suala la sensa kwa  madai kuwa hawakushirikishwa ipasavyo katika suala hilo. 
    Sababu nyengine iliyowafanya wananchi hao kutaka kususia suala hilo ni  kwa madai kuwa hawawezi kushiriki suala la sensa, huku wakiwa bado  hawajatekelezewa haki zao za kisheria ikiwemo kutopewa vitambulisho vya  uzanzibari ukaazi. 
    Amewataka wananchi kupima faida na hasara za kushiriki kwenye zoezi  hilo la sensa, na hatimaye waweze kushiriki kikamilifu kwa maslahi ya  maendeleo ya nchi.
    Akizungumzia kuhusu mchakato wa ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya  mabadiliko ya katiba, Maalim Seif amewataka wananchi kuwa huru kutoa  maoni yao, na kwamba hakuna atakayeadhibiwa kwa sababu ya kutoa maoni.  “Mimi najua wapo wanaotaka serikali moja, wengine mbili, tatu, nne, na  muungano wa mkataba, lakini wengine wanataka waachiwe wapumuwe. 
   Yote hayo ni maoni na kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake bila ya  kulazimishwa, kwa hivyo wakati wenu ukifika nendeni mkatiwe maoni hayo  kwa uwazi”, alisisitiza Maalim Seif.
    Amesema lengo la serikali ya Tanzania ni kuwa na katiba mpya ifikapo  April mwaka 2014, na kufahamisha kuwa kwa Wazanzibari suala kubwa  linalowagusa kwenye mabadiliko hayo ni suala la Muungano.  “Zanzibar tunayo katiba yetu ambayo imejitosheleza kwa mambo yetu ya  Zanzibar, lakini suala kubwa kwenye mabadiliko hayo kwetu sisi litakuwa  ni la Muungano, na hili haliwezi kuepukwa”, alibainisha.
    Amesema Zanzibar kabla ya Muungano ilikuwa nchi huru iliyokuwa na kiti  chake katika Umoja wa Mataifa, na kuelezea haja ya kuwepo kwa Mamlaka  kamili ya Zanzibar ili iweze kurejesha kiti chake kwenye umoja huo. 
    Amewataka wananchi kuangalia maslahi ya nchi yao kwanza katika mchakato  wa kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba, na kuachana na misimamo ya  vyama  katika suala hili linalohusu maslahi ya nchi.  “Katiba ya nchi ni mali ya wananchi sio ya chama chochote, lakini najua  kila chama kina katiba yake na hiyo ndio itabakia kuwa katiba na  muongozo wa chama husika, kwa hivyo ndugu zangu naomba tulifahamu hili  na tuangalie maslahi ya nchi yetu kwanza”, alifahamisha. 
    Makamu wa Kwanza wa Rais alitumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa  wananchi walioathirika kutokana na ajali mbaya ya boti ya Mv. Skagit  ilisababisha vifo vya watu kadhaa. 
   Amewataka wananchi kuweka imani zao kuwa suala hilo limetokana na  mipango ya Mwenyezi Mungu, na kwamba hakuna mtu angeweza kulizuia  lisitokee.  Katika hatua nyengine Maalim Seif amempongeza aliyekuwa Waziri wa  Miundombinu na Mawasilino Mhe. Hamad Massoud Hamad kutokana na kitendo  chake cha kijasiri cha kuamua kujiuzulu nafasi hiyo. 
    Amesema kitendo hicho cha kuwajibika kisiasa kimemjengea heshima yeye  mwenyewe, chama chake na taifa kwa ujumla, kitendo ambacho linapaswa  kuingwa na viongozi wengine wa nchi iwapo litatokea jambo lolote  linalogusa maslahi ya wananchi.  “Mhe. Hamad amekuwa mwalimu wa viongozi wa Afrika, kwani viongozi wa  Afrika hawana utamauni huo hata likitokea jambo gani, lakini yeye  ameamua kujisafisha licha ya kuwa hakuwa na kosa kwa sababu safari ili  haikuanzia Zanzibar”, alifahamisha Maalim Seif 
    Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Ole Mhe. Hamad Massoud Hamad  ambaye alikuwa akishikilia nafasi hiyo ya uwaziri, amesema aliamua  kuachia nafasi hiyo siku chache baada ya tukio, ili kujijengea heshima  kisiasa.  “Niliamua kujiuzulu nafasi ile kwa nia njema, sikulazimishwa wala  kupokea shinikizo kutoka kwa mtu yoyote”, alisema Hamad Massoud. 
    Alisema kwa sasa akiwa Mwakilishi wa wananchi na kiongozi wa chama  hicho, ataendelea kushirikiana na viongozi na wanachama katika kukijenga  zaidi chama hicho ili kiweze kufikia malengo yake iliyojiwekea.  
   Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais aliwataka wananchi wa kisiwa cha  Pemba kuendeleza utamaduni wa kufutari kwa pamoja ili kuongeza upendo  miongoni mwao. 
    Maalim Seif alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti baada ya kushiriki  katika futari ya pamoja aliyoiandaa kwa wananchi wa mikoa ya Kusini na  Kaskazini Pemba iliyofanyika Ukumbi wa kiwanda cha makonyo Wawi na  viwanja vya Ikulu ya Wete.
 Na
   Hassan Hamad 
  Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar