
Mshambuliaji wa Taifa Stars Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka beki wa timu ya Botswana,  ‘Zebras’ Oscar Neenga wakati wa mechi ya kirafiki ya Kimataifa  iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole mjini Gaborone Bostwana juzi na  kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
 Mshambuliaji wa Taifa Stars Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka beki wa timu ya Botswana,  ‘Zebras’ Oscar Neenga wakati wa mechi ya kirafiki ya Kimataifa  iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole mjini Gaborone Bostwana juzi na  kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Taifa  Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana (Zebras) katika  moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la  Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka  huu) usiku.
Hadi  mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole ulioko  Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo zilikuwa zimefungana  mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17  lililofungwa kwa penalti na beki Erasto Nyoni.
Mwamuzi  Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile  Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji Mrisho  Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.
Bao  hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26  baada ya shuti kali lililopigwa na Lemponye Tshireletso nje ya eneo la  hatari kumshinda nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja.
Dakika tano baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto aliifungia Stars bao la pili kwa shuti la mbali.
Tshireletso aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37. 
Mfungaji  alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi  ya kushoto uliopigwa na Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki Aggrey  Morris.
Kipindi  cha pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo  na Salum Abubakar na nafasi zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman  Idd.
Safari  hii Zebras ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo Michael  Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi fupi  iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika  13 za mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto Nyoni  kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji  Lovemore Murirwa.
Mrisho  Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia Stars  dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon Msuva  aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha  ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ulinzi  ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha washambuliaji  wa Botswana wakifunga bila bughudha. 
Mabeki hawatakiwi kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti washambuliaji wa timu pinzani.
"Kwa  upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi yake ya  kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye timu kwa  mara ya kwanza.
Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia, hivyo nitamrekebisha polepole," alisema Kocha Poulsen mara baada ya mechi hiyo.
Stars;  Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani,  Frank Domayo/Shabani Nditi, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd,  Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi  Kazimoto.
Zebras;  Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin Olerile,  Oscar Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick Motsepe/Jackie  Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo Sembowa,  Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore Murirwa.
Stars  inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani kesho  (Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.

