Mkuu wa huduma za Elimu ya Makumbusho Zanzibar Ramadhan Machano  akizungumza na Wawakilishi wa vikundi vinavyofanya mazoezi ya viungo  Zanzibar hawapo pichani katika Makumbusho kuu ya Taifa Baitil elajaib  
   Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 
    Washiriki ambao wameenda kuzuru katika maeneo tofauti ya makumbusho ya  Taifa ya Zanzibar wametakiwa kuwa Mabolazi wazuri katika jamii zao ili  kuhakikisha kuwa jamii ya Zanzibar inajenga utamaduni wa kutembelea  katika makumbusho hayo. 
    Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa huduma za Elimu ya Makumbusho  Zanzibar Ramadhan Machano katika ziara yake na Wawakilishi wa Vikundi  vitano vinavyofanya mazoezi ya viungo Zanzibar kwa lengo la kuhamasisha  utekelezaji wa mpango wa Utalii kwa wote. 
    Amesema wameamua kuwaalika wawakilishi hao kutembelea maeneo ya  makumbusho ya Zanzibar ili wasaidie kuwahamsisha wananchi kutembelea  maeneo hayo kwa lengo la kujua historia ya Zanzibar.   Machano amefahamisha kuwa,kwa vile wawakilishi hao wanajumuika na jamii  kwa ujumla anaamini kuwa wanaweza kuibadili jamii na kuepukana na dhana  iliyojengeka kwa wananchi wengi kuwa utalii unafanywa na Wageni. 
    Aidha amefahamisha kuwa kufanikiwa kwa Mpango wa Utalii kwa Wote  kutaiwezesha Idara ya Makumbusho kutokutegemea wageni katika kupata  mapato yake badala yake Wenyeji wanaweza kuchukua jukumu hilo. 
    Machano ametaja kingilio ambacho wenyeji wanapaswa kuchangia wanapofika  katika maeneo ya Makumbusho kuwa ni Shilingi 1,000 kwa mtu mzima na  mtoto Shilingi mia tano.   Aidha Machano amesema wataendelea kuwashirikisha viongozi wengine  ikiwemo Mashekh na Walimu wa Shule ili waweze kuisaidia Serikali katika  kuhimiza utalii kwa wote. 
    Kwa upande wao washiriki wa ziara hiyo wamemuahidi Mkuu huyo kuwa  Wataendelea kuwahamasisha wanachama wao na jamii kwa ujumla ili waweze  kutenga muda wao kwa lengo la kutembelea maeneo ya makumbusho. 
    Wamesema wamejifunza mengi katika ziara hiyo ikiwemo kujua asili ya  utamaduni wa Mswahili sambamba na kujionea uhalisia wa mambo kinyume na  kusimuliwa katika vitabu vya kihistoria.   Ziara hiyo ambayo ilijumuisha vikundi vya Kata Presha, New Generation,  Obama, Nameless na Mandela ilianzia katika Makumbusho kuu ya Taifa  Baitil Ajaib na kuendelea katika Magofu ya Mwinyimkuu Dunga, Bi  Kihole-Bungi na kumalizia katika Pango la Kuumbi-Jambiani.
    IMETOLEWA NA
   IDARA YA HABARI MAELEZO 
  ZANZIBAR 01/09/2012