Pages

Friday, September 7, 2012

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Kukagua Taasisi Zote zilizopo chini ya wizara yake

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi amesema anapitia taasisi zote zilizopo chini ya wizara yake ili kusikiliza mafanikio na kujua matatizo yanazozikabili taasisi hizo ili kuweza kuboresha huduma katika sekta ya afya nchini pamoja na kupanga mipango mizuri katika kuendeleza taasisi hizo.

Dkt. Mwinyi amesema hayo leo kwenye ziara yake na kuzungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya Chakula na Liche Tanzania (TFNC).

“Lazima tujiulize uwepo wa taasisi hii,mwanzoni taasisi hii ilikuwa inajikita na utapiamlo, kwa sasa kuna magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ,alitaja mfano wa magonjwa haya ni moyo,kisukari na mengineyo magonjwa haya mapambano yake ni kinga,na wataalamu wa kutoa kinga ni nyinyi,hivyo masuala ya lishe ni muhimu kabla ya kuanza kuyatibu.

Aidha Dkt. Mwinyi alisema wizara yake ina kila sababu ya kuyapa kipaumbele masuala ya lishe nchini licha ya ufinyu wa bajeti wanayoipata, “ipo haja ya kujipanga upya na kufanya kitu cha ziada ili kupunguza kiwango cha utapiamlo nchini pamoja na upungufu wa wekundu wa damu kwa wanawake wenye umri wa kuzaa ambapo inachangia vifo vya akina mama wajawazito nah ii inachangia na akina mama wengi kutokuwa na elimu na mafunzo juu ya lishe na hivyo nchi kuwa nyuma na kutofikia malengo ya millennia ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito nchini.

Awali Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Benetict Jeje alisema taasisi yake ina changamoto ya kuhakikisha kuwa huduma za lishe nchini zinapanuka na kuwafikia wananchi wengi hasa waishio vijijini , hivyo serikali kuamua kuajiri maafisa lishe katika halmashauri 106 kati ya 168 na mikoa 11 imefanya hivyo.

“Lishe ni suala mtambuka na linalogusa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla,ushiriki wa sekta mbalimbali katika kukabliana na changamoto za lishe nchini ni jambo lisiloepukika”alisema Jeje.

Hata hivyo alisema taasisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zimechangia kupunguza kwa kiwango cha utapiamlo nchini kati ya mwaka 1999 na 2010.Asilimia 16 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wana uzito pungufu,asilimia 5 ni wakondefu na asilimia 42 wana udumavu na upungufu wa damu unaathiri asilimia 69 ya watoto wakati upungufu wa vitamin A ni asilimia 33

-MWISHO-


Na.
Catherine Sungura.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamiii

Popular Posts