Pages

Monday, September 3, 2012

Uongozi wa Jimbo la Kitope umekusudia kuimarisha sekta ya michezo

Mwakilishi wa Timu ya Soka ya Kitope United akipokea msaada wa Seti ya Jezi pamoja na Fedha Taslimu kwa ajili ya usajili na kujiandaa kwenye mashindano yanayowakabili.
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na wanamichezo wa Timu nne za soka za Jimbo la Kitope hapo ukumbi wa Tawi la CCM la Kitope A.
Khamis Mswahili Mwinyi Mwakilishi wa wanamichezo wa timu nne za soka za Jimbo la Kitope akiwasilisha changamoto wanazokabiliana nazo katika michezo kwa Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi.
--
Uongozi wa Jimbo la Kitope umekusudia kuimarisha sekta ya michezo kwa lengo la kuwawezesha Vijana wa Jimbo hilo kuwa pamoja katika harakati zao za Michezo na zile za kijamii.

Makamu wa pili wa Rais Zanzibar na Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo mara baada ya kupokea matatizo na ushauri wa wanamichezo wa Timu Nne zilizomo ndani ya Jimbo hilo walioutoa katika Kikao chao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Tawi la CCM Kitope A.

Balozi Seif aliwaeleza wawakilishi wa Timu hizo ambazo ni Kitope United, African Boys, Home Boys na Kombora kwamba uamuzi wao wa kufikiria kuanzisha Timu moja imara ndani ya jimbo hilo umetoa faraja kwa viongozi jambo ambalo litarahisisha hata upatikanaji wa vifaa na misaada kwa wepesi zaidi.

Aliahidi kwa kuwa yeye ni Kiongozi wao wa Jimbo atahakikisha kwamba Sekta ya Michezo inapata nguvu zaidi kutokana na umuhimu wake uliojichomoza hivi karibuni wa kutoa ajira endapo Vijana hao watajituma vilivyo. “ Nataka kuona Timu za Jimbo langu la Kitope zinashiriki na kufanya vizuri katika mashindano ya Wilaya, Mikoa na hata Taifa. Lakini kitachosaidia zaidi kwenu ni juhudi ya kuzingatia mazoezi yatakayofuatiwa na nguvu za misaada ya Viongozi wenu”. Alisisitiza Balozi Seif.

Akizungumzia matatizoyanayozikabili Timu hizo Balozi Seif atajaribu kuzungumza na wafadhili mbali mbali wa michezo ili kuona namna gani wanaweza kusaidia uimarishaji wa uwanja wa uhakika na wa kisasa ndani ya jimbo hilo.

Alisema suala hilo litakwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya michezo ikiwemo Mipira, Nyavu Magoli na Jezi ambazo alisema zimo ndani ya uwezo wake kulingana na utaratibu aliokwishauanzisha tokea alipoanza kuliongoza jimbo hilo.

Kuhusu suala la uanzishwaji wa jengo la kudumu la Klabu Balozi Seif aliwaagiza wanamichezo hao kuanza shughuli za maandalizi ya msingi kwa vile tayari wameshaanza kukusanya nguvu za pamoja. Alisema katika kuunga mkono jitihada hizo za wanamichezo atahakikisha anasaidia nguvu za unyanyuaji jengo kwa hatua ya matofali na kuangalia mbinu za kuendeleza ujenzi huo.

Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wanamichezo hao kuwa waangalifu kutokana na ushawishi wanaoendelea kusambaziwa wa kutaka kuingizwa katika vurugu za kisiasa kwa kisingizio cha Kidini. Balozi Seif alitahadharisha kwamba ushawishi huo unaweza kuyayusha kabisa amani na muda wa Vijana hao wa kushiriki kikamilifu katika michezo yao endapo wataamua kuupokea.

Mapema wanamichezo hao walimueleza Balozi Seif matatizo yanayowakabili katika katika harakati zao za kuendeleza michezo ambayo yamekuwa yakipunguza kasi yao ya ufanisi. Wawakilishi wa wanamichezo hao Khamis Mswahili Mwinyi, Ngamia Mohd Ngamia na Amour Amour kwa pamoja walielezea changamoto zinazowakabili katika sekta ya michezo ikiwa ni pamoja na uhaba wa vifaa vya michezo, ujenzi wa Jengo la Klabu pamoja na uanzishwaji wa mashindano ya kombe la Mbunge wa Jimbo hilo ambayo tayari yamesharidhiwa na Mbunge mwenyewe kwa kukubali kutoa Vikombe na zawadi kwa washindi.

Walisema kufanikiwa kwa changamoto hizo kutawawezesha Vijana waliowengi wa jimbo hilo kuwepuka kusambaratika pamoja na vishawishi vinavyoweza kuwapelekea kujiingiza katika matendo maovu.

Katika kikao hicho Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi seti ya Jezi na Fedha Taslimu kwa Timu ya Soka ya Kitope United inayojiandaa na usajili kwa ajili yua mashindano yajayo.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar

Popular Posts