Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi  na Teknolojia, Habari na Utafiti { RAAWUZ } Bibi Mwatum Khamis Othman  akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Bibi Mwatum aliambatana na Viongozi Waandamizi wa Chama hicho kufikisha  baadhi ya Kero zinazowakwaza Wafanayakazi wa Chama hicho katika maeneo  yao ya Kazi. 
    Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Seif Ali Iddi akizungumza  na Ujumbe wa Jumuiya ya Viwanda ya Jamuhuri ya Sudan { Giad Industrial  Group } Ofisini kwa Vuga Mjini Zanzibar. Kulia ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ni Balozi wa Jamuhuri ya  Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohammed Ali.
   Ujumbe wa Jumuiya ya Viwanda ya Nchini Jamuhuri ya Sudan { Giad  Industrial Group } ukifuatilia maelezo ya Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi walipokutana Ofisini kwake Vuga Mjini  Zanzibar. Ujumbe huo uliongozwa na Balozi wa Jamuhuri ya Sudan Nchini Tanzania Dr.  Yassir Mohammed Ali. 
  ---
   Wawekezaji wa Jamuhuri ya Sudan wameombwa  kuangalia vyema mazingira ya  Zanzibar katika dhana nzima ya kuwekeza Vitega Uchumi vyao  vinakavyosaidia kushajiisha Uchumi wa Pande hizo mbili. 
   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli  hiyo hapo Ofisini kwake Vuga wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa  Jumuiya inayojishughulisha na Viwanda Nchini Sudan ya { Giad Industrial  Group } ukiongozwa na Balozi was Sudan Nchini Tanzania Dr.Yassir  Mohammed Ali. 
   Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria  kuimarisha Uchumi wake kupitia Sekta Tofauti ikiwemo ile yaViwanda kwa  kukaribisha Makampuni, Mashirika na Taasisi hisani. 
   Aliiomba Jumuiya hiyo ya Giad Industrial Group ya Sudan ambayo  imeshiriki na kupata ushindi katika maonyesho ya saba saba Mjini Dar es  salaam kujipanga vyema kuleta maombi yake ili ipate fursa ya kuwekeza   hapa Zanzibar. 
   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itakuwa tayari kuipa  mashirikiano Taasisi hiyo muhimu ambayo uzalishaji wa bidhaa zake  ambazo ni pamoja na fanicha unahitajika sana Nchini. “ Zanzibar inahitaji takriban Madeski 25,000 katika Skuli zake Unguja na  Pemba ili kuondosha tatizo la vikalio kwa Wanafunzi wake. Hivyo kitendo  cha Jumuiya hiyo kuanzisha Tawi lake kunaweza kutatua kadhia hiyo”.
    Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi. Mapema Balozi waa Jamuhuri ya Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohammed  Ali alisema Ujumbe wa Jumuiya hiyo upo Zanzibar kuangalia uwezekano wa  kuja kuwekeza Vitega Uchumi vyao Nchini. Balozi Yassir alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif kwamba Uhusiano uliopo wa muda mrefu kati ya Tanzania na Sudan  ikiwemo Zanzibar kwa ujumla utaendelea kuimarishwa kwa ustawi wa Jamii  za pande zote mbili. 
   Ujumbe huo tayari umeshaahidi kufanya maandalizi ya kuandaa maombi ya  namna ya kuja kuwekeza Miradi  yao hapa Zanzibar ndani ya kipindi cha  Mwezi Mmoja. Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi amekutana na Uongozi wa  Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi na  Teknolojia, Habari na Utafiti { RAAWUZ } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini  Zanzibar. 
   Katika Mazunguimzo yao Katibu Mkuu wa Chama hicho cha Raawuz Bibi Mwatum  Khamis Othman alisema suala la ushirikishwaji wa Wafanyakazi katika  Bodi na Kamati za Uongozi ndani ya  Taasisi za Kazi umesahauliwa kwa  kipindi kirefu sasa. 
   Bibi Mwatum alifahamisha kwamba endapo Uongozi katika sehemu za Kazi  ungekuwa ukiitumia vyema ile sheria nambari 10 ya Kamati za Uongozi  Makazini kusingekuwa na malalamiko mengi katika sehemu za Kazi. Katibu mikuu huyo wa Chama cha RAAWUZ alivitaja vyuo viwili tu vya   Maendeleo ya Utalii Maruhubi na Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka ndivyo  pekee vyenye uwakilishi wa Wafanyakazi katika Kamati za Uongozi wao. 
   Bibi Mwatum na Ujumbe wake pia walizungumzia masuala kadhaa  yanayowakabili watendaji wa Taasisi za Kazi ikiwemo ukosefu wa uangalizi  wa afya wakiwa kazini,mishahara duni kwa wafanyakazi wazoefu pamoja na  bakaa ya fedha za Mishahara kwa wafanayakazi waliokatwa mishahara yao  wakati wa zoezi la mabadiliko ya mishahara. 
   Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja hizo Makamu wa Pili wa Raisn wa  Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kwamba Serikali itaendelea  kushirikiana na Wafanyakazi katika Taasisi za kazi ili kuimarisha  ufanisi wa Kazi. 
   Balozi Seif alisema atahakikisha anaziandikia Taasisi zote  katika kuona  ushiriki wa Wafanyakazi unapatikana vyema . Aliueleza Ujumbe huo kwamba suala la Wafanyakazi wazoefu  litaangaliwa  kutokana na mchango wao wa muda mrefu katika Taifa hili pamoja na  kusisitiza kuandaliwa utaratibu kwa wafanyakazi kupimwa afya zao. 
   Na
   Othman Khamis Ame
  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar