Pages

Sunday, July 8, 2012

Twiga Bancorp Yakusanya Maoni Kuhusu Huduma Zake

MKurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Mawasiliano ya Kompyuta wa Benki hiyo, Richard Kombole
---

Na Mwandishi wetu
BENKI ya Twiga Bancorp, imezindua huduma mpya ya kukusanya maoni ya wateja wa ndani na nje ya Tanzania ili kutathimini utoaji huduma wa benki hiyo.

MKurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Mawasiliano ya Kompyuta wa Benki hiyo, Richard Kombole, aliyasema hayo Dar es Salaam jana, alipozungumzia kuzinduliwa kwa huduma hiyo itakayokuwa endelevu.

Alisema wakati huu ambapo benki hiyo imekuwa inajitanua kwa kufungua matawi mbalimbali nchini, kumeonekana ulazima kwa benki kupata maoni ya wananchi kuhusiana na huduma za benki hiyo ili kuongeza ufanisi.

“Hivi juzi tulipata tuzo ya dhahabu ya kimataifa ya utoaji wa huduma bora. Hii inatupa ishara kwamba katika ngazi ya kimataifa, huduma zetu zinakubalika na kuheshimika tumeona kula ulazima wa kukusanya maoni kwa wateja wetu wa ndani,” alisema Kombole.

Alisema ikiwa na ushirikiano na benki zaidi ya 24 zenye mashine za ATM 160 nchi nzima kupitia huduma ya Umoja Switch, Twiga Bancorp imeendelea kujitanua kwa kufungua matawi katika Mikoa ya Arusha na Mwanza na karibuni itafungua tawi jipya mkoani Dodoma.

Alisema katika kuwezesha hilo, benki hiyo itatawanya fomu maalumu za kukusanya maoni ya wateja juu ya utolewaji wa huduma ambayo yatafanyiwa kazi mara moja baada ya kupokelewa.

“Katika hili mteja wetu atakuwa huru kutoa maoni yake katika suala lolote lile linaloihusu benki yetu bila ya kuwa na hofu kwani bila kuwepo kwa wateja benki yetu haiwezi kuwepo,” alisema Mkurugenzi huyo.

Katika hatua nyingine, Benki hiyo ipo katika mchakato wa kuboresha huduma za kibenki kwa kufunga mitambo ya kisasa ya kompyuta ili kuiwezesha kutoa huduma kwa mawasiliano ya kompyuta za benki hiyo na benki nyingine bila kumlazimu mteja kwenda benki.

Akizungumzia mpango huo, Kombole alisema unatarajia kukamilika na kuanza kazi Aprili mwakani ambapo wateja watatakiwa kuwasilisha taarifa zao binafsi ili kuwawezesha kuingizwa katika mfumo huo mpya wa digitali.

“Hii itatuwezesha kuweza pia kuwasiliana kirahisi na wateja wetu litakapojitokeza jambo lolote kama vile kubadilika kwa namba za akaunti au matatizo katika akaunti ya mteja bila mteja kulazimika kuja benki,” alisema Kombole.

Popular Posts