Pages

Sunday, July 8, 2012

Rais Jakaya Kikwete Ampongeza Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Kwa Kuteuliwa Kuwa Rais wa TEC

Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa
--

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kwa kuteuliwa kwake kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) akichukua nafasi ya Baba Askofu Yuda Tadei Rwaich aliyemaliza muda wake.

“Nimefarijika sana na uteuzi wako kushika wadhifa huo muhimu hasa kutokana na imani kubwa waliyonayo Maaskofu kuhusiana na uwezo wako katika kukiongoza chombo hicho muhimu”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.


“Ninatambua na kuthamini mchango mkubwa ambao, kwa muda mrefu sasa, Kanisa Katoliki limekuwa likiutoa kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake hasa katika nyanja za huduma za jamii.

Aidha uhusiano mzuri uliopo kati ya Serikali ninayoiongoza na Kanisa Katoliki unaendelea kunitia moyo, hivyo ninakuhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza na kuimarisha uhusiano huu kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla”, amesema na kusisitiza Rais Kikwete katika salamu zake za pongezi.

Rais Kikwete amemtakia Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kila la heri na mafanikio makubwa katika kuliongoza Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
6 Julai, 2012

Popular Posts