
 Mkuu  wa Wilaya ya Newala, Christopher Magala amefungua mafunzo ya mgambo  katika Kata ya Mnyambe Wilayani  Newala, mkoani Mtwara jana
  -- 
  Akihutubia  wana mafunzo ya mgambo katika Kata hiyo ya Mnyambe, Mkuu wa Wilaya hiyo  amewaasa na kuwafafanulia wana mafunzo kwamba, mafunzo hayo ya mgambo  yapo kwa mjibu wa sheria namba 147 ya mwaka 1977 na kwa mjibu wa sheria  inayounda jeshi la Wananchi (JWTZ) ya mwaka 1966 na hivyo wapuuze  upotoshwaji unaotolewa na baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakieneza  uvumi kwamba mgambo haupo kwa mujibu wa sheria. 
  Aidha  Magala amesema kushiriki mafunzo ya Mgambo si lazima bali ni hiari ya  mtu mwenye kujitokeza na kujiandikisha ili kuwa wakakamavu na kupata  walinzi wazuri wa amani katika jamii.
  "Mgambo  ni jeshi la akiba linaloundwa na raia wazalendo ambao wako tayari  kufanya kazi mbalimbali zinazofanywa na majeshi mengine kama kuokoa  maisha na mali za wananchi wakati wa maafa," alisema Magala.
  Pia  DC Magala amewataka wana mafunzo ya mgambo kuwa mstari wa mbele na kuwa  mfano katika kutekeleza sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za nchi  kwa kuwa na nidhamu kama wanajeshi wengine mara watakapomaliza mafunzo  hayo.
  Aidha  Mkuu huyo wa Wilaya amewaambia faida zingine watakazopata mara baada ya  kumaliza mafunzo ya mgambo ni pamoja na kushirikiana na jeshi la polisi  kupitia mpango wa ulinzi shilikishi/Polisi jamii katika maeneo  mbalimbali mijini na vijijini, kupewa kipaumbele pale majeshi yetu  yanapotaka kuajiri, na kupata ajira katika makapuni ya ulinzi: 
  "Serikali  imeyaagiza makampuni yote ya ulinzi kutumia wananchi waliopitia mafunzo  ya majeshi mbalimbali na mgambo lakini pia majeshi yote yameelekezwa  kuwapa kipaumbele waliopitia mafunzo ya mgambo wakati wa ajira zao,”  alisema Magala
  Baada ya kufungua mafunzo ya mgambo Mkuu wa Wilaya ya Newala ametembelea shule ya Sekondari ya Mnyambe na kuikagua.