Pages

Monday, June 18, 2012

HOTUBA JUU YA UTEKELEZAJI WA DHANA YA UTALII KWA WOTE NA VIONGOZI WA DINI

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN KATIKA UFUNGUZI WA WARSHA JUU YA UTEKELEZAJI WA DHANA YA UTALII KWA WOTE NA VIONGOZI WA DINI,

HOTELI YA BWAWANI, JUMATATU, TAREHE 18 JUNI, 2012.

Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo,

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,

Waheshimiwa Viongozi wa Dini mbali mbali,

Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Serikali,

Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa kila kitu, Mola wa utukufu wote kwa kutujaaliya afya njema na tukaweza kuhudhuria warsha hii muhimu tukiwa na amani, salama na utulivu.

Natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kupitia Kamisheni ya Utalii kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha hii muhimu inayohusu utalii kwa wote. Aidha, natoa shukurani kwa viongozi wa dini mbali mbali pamoja na washiriki nyote kwa jumla kwa kuitikia mualiko na kuwa tayari kutoa michango yenu ambayo naamini itatoa mchango mkubwa kwa Serikali na wananchi wote kwa jumla katika kuendeleza sekta hii muhimu na katika kutekeleza dhana ya utalii kwa wote.

Ndugu Washiriki,

Nimefurahi kuona warsha hii imewajumuisha washiriki wengi ikiwa ni pamoja na wataalamu wa fani mbali mbali na viongozi wa dini tofauti. Hili ni jambo la faraja kwetu sote kuona kuwa tunakaa pamoja bila ya kujali tofauti zetu za kijamii kwa lengo la kujadili na kupanga mambo muhimu yenye mnasaba na maendeleo ya nchi yetu kwa mashirikiano ya hali ya juu. Hii ni sifa nzuri katika historia yetu na ni sehemu muhimu ya utamaduni wetu. Kwa hivyo hatuna budi kuiendeleza.

Ni dhahiri kuwa, hatuwezi kuzungumzia historia na maendeleo ya Zanzibar bila ya kuhusisha na ufikaji wa makundi tofauti ya wageni kutoka sehemu mbali mbali duniani ambao kwa hivi sasa wanakuja kwa jina jipya la watalii. Historia inatufundisha kuwa maendeleo ya Zanzibar na watu wake yamefungamana na ufikaji wa wageni kutoka sehemu kadhaa za dunia. Wengi walifika Zanzibar kutoka sehemu tofauti za Afrika, wako waliotokea Asia na wengine walifika kama ni watembezi kisha wakaanzisha makaazi ya kudumu hapa Zanzibar kutoka bara la Ulaya katika karne tofauti. Mchanganyiko mkubwa wa wenyeji na wageni katika nyakati mbali mbali ndio msingi wa Zanzibar ya leo yenye utamaduni na desturi za pekee duniani. Haya yanaonekana popote pale Zanzibar na bila ya shaka ni wazi kuwa hata katika hadhira iliyopo hapa hivi leo yanaweza kuthibitika.

Tafiti mbali mbali za Kiakilojia (archaeology) zimethibitisha kufika kwa wageni Zanzibar katika karne nyingi zilizopita. Mwanahistoria wa Kiislamu katika karne ya 13 aliyeitwa Yakuut Al- Hamawy ameandika kuwa Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa cha wasafiri na wageni hata kabla ya kuzaliwa Nabii Issa pale ilipokuwa ikujulikana kwa majina ya Zangh, ’Zingis na baadaeZanj na Zenj. Aidha, vitabu mbali mbali vya kihistoria vimeandika juu ya kufika kwa wageni mbali mbali kutoka Bara la Ulaya wakiwemo akina Captain James Lancaster waliofika Zanzibar mwaka 1592 kwa meli inayoitwa “ Edward Bonaventure.”

Ndugu Washiriki,

Taathira nzuri za wageni waliofika Zanzibar kwa madhumuni mbali mbali zipo dhahiri katika miji na vijiji tofauti vya Unguja na Pemba. Taathira hizo baadhi yake zimebakia kama ni sehemu nzuri ya tabia zetu, nyengine zimebakia katika majengo yetu na kuwa vivutio vya watalii wanaofika kututembelea hivi sasa na vimekuwa vikitoa mchango mkubwa katika kuendeleza uchumi wetu. Mfano mzuri ni jengo la Ngome Kongwe lilojengwa na Wageni wa Kireno mnamo mwaka 1710, Msikiti wa Kizimkazi uliojengwa ziadi ya miaka 800 iliyopita, Kanisa la Minara Miwili lilojengwa mwaka 1893 na majengo mengineyo ya kihistoria.

Aidha, kuwasili kwa wageni kwa nyakati tofauti kumechangia kwa kiasi kikubwa katika kukua kwa lugha yetu ya Taifa ya Kiswahili ambayo hivi sasa sio sisi Watanzania tu tunaojivunia, bali pia fahari kwa Bara zima la Afirka, kwani ni lugha ya kwanza yenye asili ya Kiafrika inayozungumzwa na watu wengi na yenye kuimarika kwa haraka.

Ndugu Washiriki,

Historia hii fupi nimeielezea ili kuonesha uhusiano mkubwa uliopo katika historia yetu, utamaduni wetu na maendeleo yetu katika njanja mbali mbali na suala zima la ufikaji na utembeaji wa wageni katika visiwa hivi. Sisi si wageni katika kupokea wageni. Kwa kutambua umuhimu wa wageni wazee walisema misemo ifuatayo: “Zanzibar ni njema atakae aje”; “Mgeni njoo mwenyeji apone”. Nimefurahi sana kuona mkusanyiko wetu huu wenye watu mahiri uko tayari kujadili njia zilizo bora za kuwapokea na kuwahudumia wageni wanaokuja nchini petu kama ni watalii ambao mchango wao katika ustawi wa nchi yetu ni mkubwa.

Inanipa moyo sana kuona kuwa viongozi wa dini mbali mbali zenye wafuasi hapa Zanzibar, wapo hapa kwa mjadala huu. Matumaini yangu ni kuwa kitendo hiki cha kubadilishana mawazo kitatufikisha pazuri na tutaibuka na njia zilizo bora za kuendeleza utalii wetu utakaotilia maanani mila na desturi zetu.

Nilipoitangaza dhana ya utalii kwa wote katika mkutano wa sita wa Baraza la Biashara la Zanzibar tarehe 16 Oktoba, 2011, nilibainisha uhusiano wa utalii na jamii yetu yote bila ya ubaguzi na manufaa yake kwa makundi mbali mbali. Nilielezea juu ya umuhimu wa sekta hii kwa wavuvi, wakulima, wanafunzi na sekta nyengine za biashara ikiwemo hoteli na mikahawa.

Nashukuru kuona kuwa katika dini zote zenye wafuasi hapa Zanzibar hakuna hata moja ambayo katika mafundisho yake inakataza suala la kutalii sehemu mbali mbali ulimwenguni kwa nia njema. Katika Dini ya Kiislamu kwenye Kitabu kitukufu cha Kur-ani kwenye Suurat Al A’nkabut (29:20) Mwenyezi Mungu anatufundisha umuhimu wa kutembea kwa kusema:

‘Tembeeni katika Ardhi na tazameni jinsi alivyoanzisha uumbaji; Kisha Mwenyezi Mungu ndiye anayeumba umbo la baadaye; hakika Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu’

Hii ni ithibati ya kuwa suala la utalii halijakatazwa katika Dini ya Kiislamu. Muhimu zaidi, Dini ya Kiislamu, Dini ya Kikiristo na dini zote zilizopo Zanzibar zinahimiza kufanya takrima kwa wageni. Kutokana na mafundisho mazuri ya dini zote hizi juu ya wageni, Zanzibar imekuwa na misingi mizuri ya kuwakaribisha wageni na kuwasaidia katika kuimarisha maisha yao hapa. Hivi sasa tunakaribisha zaidi wageni wa utalii na sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuongeza ufikaji wao kwa manufaa yetu sote.

Ndugu Washiriki,

Licha ya kuwa dini zote zenye wafuasi hapa Zanzibar hazijakataza kuja kwa wageni kwa kutalii, bado kuna dhana kwa baadhi ya watu kuuona utalii kama ni tatizo na chanzo cha maovu na maasi na unachangia katika kuvunja maadili na kuharibu utamaduni. Hizi ni dhana ambazo zinafaa kuchunguzwa na natumai warsha hii itatoa maoni ya viongozi wa dini katika hayo na kupendekeza namna bora ya kufanya utalii wetu uendane na maadili yetu kwa manufaa ya watu wote na Taifa kwa jumla. Tutilie maanani kauli ya msanii mmoja kuwa “ Maadili ni kipimo cha akili”

Ni muhimu tukafahamu kuwa watalii wengi wanaokuja kututembelea ni watiifu wa sheria na ni raia wazuri wa nchi zao. Ikiwa kasoro hizi zinajitokeza katika jitihada zetu za kuwakaribisha wageni basi nadhani kutakuwa na upungufu kwa baadhi ya watu juu ya namna tunavyowakaribisha na kuwahudumia.

Kadhalika, ni muhimu tukafahamu kuwa dhana na lengo la Serikali la kuleta utalii kwa wote, halikujikita katika kuzingatia manufaa tu, bali pia linazingatia jinsi gani kwa pamoja tunaweza kushirikiana ili sekta hii iwe na tija zaidi kwa jamii yetu sote, na jinsi gani kwa pamoja tunaweza kushirikiana katika kuziondoa zile kasoro na madhara yanayosababishwa na jitihada zetu za kuikuza sekta hii.

Kwa mantiki hiyo, viongozi wa dini na washiriki wengine mliopo hapa, mna jukumu kubwa la kuwaelimisha wananchi juu ya njia bora za kuwakaribisha wageni huku tukilinda dini, desturi na mila zetu. Matumaini yangu ni kuwa warsha hii itatoa miongozo bora itakayochangia katika jitihada za Serikali za kukuza sekta hii bila ya kuharibu sifa njema tulizonazo za maadili mema ya wananchi wa Visiwa hivi.

Ndugu Washiriki,

Serikali imefikia maamuzi ya kuifanya sekta hii kuwa ni sekta kiongozi. Katika kuitekeleza sera hiyo, tunahakiksha kuwa wananchi wote wataendelea kufaidika na sekta hii. Serikali ina azma ya kuzifanya sekta zote kama tulivyokwishasema ziweze kushiriki na kutoa mchango wa moja kwa moja katika kuiendeleza sekta ya utalii na kila mwananchi afaidike na jitihada hizo katika dhana yaUtalii kwa wote.

Itakumbukwa kuwa uchumi wetu ulipata msukosuko baada ya kuanguka kwa zao la karafuu mnamo miaka ya 1970 na 80. Msukosuko huo uliifanya Serikali kulazimika kutafuta mazao mengine ya biashara pamoja na kutafuta njia nyengine ili kuendeleza uchumi wake. Hapo ndipo Serikali ilipoamua kuiendeleza sekta ya utalii. Kabla ya uamuzi huu, Zanzibar ilikuwa inapokea watalii kati ya 25,000 hadi 40,000 kwa mwaka. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2011 ilikisiwa kuwa watalii 175,000 waliingia Zanzibar, lakini inadhaniwa kuwa idadi hii ni ndogo. Lengo la Serikali ni kufikisha watalii 500,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020 lakini kuna kila ishara kwamba idadi hii itafikiwa kabla ya mwaka huo. Sekta ya utalii inachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni tutazoingiza na asilimia 70 ya wananchi wetu wameajiriwa katika sekta hii moja kwa moja au kwa njia ya uhusiano.

Ndugu Washiriki,

Napenda kueleza kwamba licha ya juhudi hizo za kukuza sekta ya utalii, Serikali imekuwa ikichukuwa juhudi mbali mbali katika kukuza uchumi wetu. Juhudi hizo ni pamoja na kufufua zao la karafuu, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutilia mkazo katika za Kilimo na Uvuvi.

Kutokana na jitihada hizo tumeweza kuona mafanikio kwenye uchumi wetu. Katika mwaka 2011 uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.8 na katika mwaka 2012/2013 uchumi wetu unategemewa kukua kwa asilimia 7.5. Aidha, jitihada hizi zimepelekea kukua kwa pato la mwananchi kutoka T.Shs. 782,000 kwa mwaka hadi kufikia T.Shs. 960,000 ambazo ni sawa na Dola za Kimarekani 615 kutoka Dola 560, mwaka 2010. Kiwango hiki kimeiwezesha Zanzibar kuyafikia malengo ya Milenia ambapo nchi zote duniani zinatakiwa ifikapo mwaka 2015 pato la wananchi wake liwe limeshafikia T.Shs. 884,000. Nawasihi wananchi kuunga mkono juhudi hizi za Serikali kwa moyo mmoja na uzalendo ili kufikia malengo tuliyoyakusudia.

Ndugu Washiriki,

Matumaini yangu ni kwamba mkusanyiko wetu huu utasisimua faida ya utalili kwa wananchi na kutoa mwangaza kwa wafuasi wa dini tulizonazo kuunga mkono jitihada zetu. Tukubali kwamba utalii unakubalika kwa misingi ya dini na hivi sasa ni sekta muhimu ya kiuchumi kwa mataifa mbali mbali duniani.

Mabadiliko ya uchumi wa dunia yamelazimisha nchi nyingi kuwekeza na kukuza utalii. Mataifa hayo yakiwemo yale yenye idadi kubwa ya waislamu nayo yameamua kukuza utalii ili utoe mchango katika kusaidia raia wake.

Kuna nchi 44 duniani ambazo zinajuilikana kama nchi za Kiislamu. Nyingi ya nchi hizo zimekuwa zikifanya jitihada katika kukuza utalii ikiwemo Iran. Hivi sasa nchi ya Uturuki, Malaysia, Misri, Moroco na Tunisia ni mfano wa nchi za Kiislamu ambazo zinafanya vizuri katika Utalii. Aidha, katika nchi zenye Wakiristo wengi kama Italy, Ufaransa na Spain utalii umekuwa sekta muhimu katika uchumi wao. Dini zao haziwi kikwazo cha utalii bali viongozi wa dini katika mataifa hayo hutoa michango juu ya namna bora ya kuendesha biashara ya utalii wenye manufaa kwa watu na nchi kwa jumla na unaheshimu dini za wenyeji. Hali hiyo ndiyo tunayoikaribisha hapa kwetu.

Ndugu Washiriki,

Nilipata fursa ya kuitembelea nchi ya Indonesia mara tatu (3). Mara ya kwanza mwaka 1997 na mara mbili mwaka 2005. Mara zote tatu nilishuhudia jinsi utalii ulivyoimarishwa katika maeneo ya waumini wa Kiislamu, Kikristo na Kihindu. Kisiwa cha Bali kimetia fora kwenye utalii kwani wakaazi wake wote wamejihusisha na utalii katika maisha yao ya kila siku. Hawajabadilika katika kufanya ibada zao na kuzingatia mila na utamaduni wao.

Wakati mimi na viongozi wenzangu wa Serikali tulipoitembelea Uturuki kuanzia tarehe 28 Mei hadi 2 Juni mwaka jana (2011) tulivutiwa sana na maendeleo na jitihada za wananchi wa Uturuki waliyofikia katika kuendeleza sekta hii ya utalii. Mnamo mwanzoni mwa miaka ya 80, wananchi wa Uturuki walikaa, wakajadili, wakapanga na kuamua juu ya kuwekeza katika sekta ya utalii. Kabla kupanga mikakati hiyo, nchi yao ilikuwa inapokea si zaidi ya wageni milioni 1.5. Baada ya kupanga na kutekeleza sera madhubiti walizopitisha wakati huo, mwaka uliopita 2011 walifanikiwa kutembelewa na wageni zaidi ya milioni 31.5. Mji wa Antalia peke yake wenye wakaazi milioni mbili, ilipokea watalii milioni kumi (10). Itakumbukwa kuwa zaidi ya asilimia 97.8 ya raia wa nchi hii ni Waislamu.

Miongoni mwa siri ya mafanikio yao ni kuwa waliamua kuielekeza rasilmali yote ya nchi yao katika kutoa msukumo kwenye sekta ya utalii na walihakikisha raia wote wanashiriki katika kutoa michango yao. Miongoni mwa sekta iliyofaidika ni sekta ya afya, kwani hivi sasa nchi ya Uturuki imekuwa ikipokea wageni mbali mbali wanaofika kwa madhumuni ya matembezi na matibabu. Aidha, wageni wengi wanakwenda kuzuru majengo ya kihistoria ya Dini ya Kiislamu na Dini ya Kikristo.

Wakati tulipokuwa nchini humo tulishuhudia jinsi wanavyotumia majengo mbali mbali ya kihistoria ikiwemo misikiti na makanisa kama ni vivutio vya watalii. Natoa wito kwa washiriki wa Warsha hii na wananchi wote kutafuta rai mbali mbali zilizopelekea mafanikio kwa nchi za wenzetu na kuja na njia bora juu ya kutizama uwezekano wa kutekeleza rai hizo nchini kwetu.

Ndugu Washiriki,

Naamini kwa dhati kabisa kwamba tukishirikiana kwa pamoja, tukizitekeleza sera na mipango yetu tuliyonayo na kwa kuzingatia sheria ya utalii iliyopo, tunaweza kuendeleza Utalii huku tukilinda desturi na mila zetu. Kama nilivyosema awali, Watalii ni watiifu wa sheria. Nchi ya Italy imekuwa ikivutia watalii kwa kutumia historia ya mji wa Vatican. Watalii kutoka nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu kila mwaka wanafika sehemu hii yenye historia kubwa. Katika matembezi ya sehemu hii muhimu haizingatiwi dini ya mtu, ila kinachosisitizwa ni ufuataji wa sheria na kuheshimu desturi ya sehemu hii muhimu kwa wafuasi wa Dini ya Kikirsto hasa wa madhehebu ya Kikatoliki.

Jambo muhimu la kujifunza hapa ni kwamba watalii wanaheshimu misingi ya dini za wengine na ndio maana wanapenda kutembelea majengo ya kihistoria. Hapa Zanzibar tunayo majengo ya fahari ya kihistoria ya dini na majengo ya kale, ambayo yanaweza kuchangia katika kukuza utalii. Ni juu ya viongozi wa dini na jamii kutoa ushauri na maelekezo yanayofaa juu suala hili.

Ndugu Washiriki,

Katika kukuza sekta ya utalii na shughuli nyengine zote za maendeleo yetu, ni muhimu kuimarisha ushirikiano wetu katika kulinda na kuendeleza amani na utulivu. Kuna umuhimu wa kuendeleza mila na desturi zetu ya kukaa pamoja bila ya kubaguana kwa misingi ya ukabila au dini. Huu ni msingi wa utamaduni wetu na siri kubwa ya mafanikio yetu. Hivi sasa, hatuhitaji kusoma historia ili tupate kufahamu kwamba amani ikiondoka ni tabu kuirejesha. Ni wakati wa kukaa na kusikiliza yanayowafika wenzetu wa nchi mbali mbali waliojaribu kuichezea amani. Inasikitisha kuona kuwa hivi sasa wananchi wa mataifa kadhaa wamekuwa wakigombana, wakipigana na kuumizana na hata kudiriki kuyahatarisha maisha yao bila ya kuzingatia maendeleo ya nchi yao. Mwenyezi Mungu atujaalie mambo hayo yasitokee kwetu.

Vitendo vya aina yoyote ile vyenye kuashiria kuivuruga amani tusiviruhusu kwani havitamsadia mtu isipokuwa vitaharibu yale yote mazuri tuliyoyajenga kwa jitihada kubwa kwa miaka mingi. Nawasihi wananchi washikamane na maelekezo ya Serikali yao. Vile vile, nawasihi viongozi wa dini wawe mstari wa mbele katika kuiongoza jamii katika maadili mema.

Ni muhimu tukafahamu kuwa utalii ambao uchumi wetu hivi sasa unautegemea sana hutegemea kuwepo kwa amani na utulivu pamoja na kuwepo kwa wenyeji wenye tabia ya kuheshimu na kukaribisha wageni. Nafahamu kuwa sote tunayafahamu haya na tunatambua kwamba kuwepo kwa amani na utulivu kunachangia kustawi kwa maisha yetu lakini ni vyema tukaendelea kukumbushana kutokana na umuhimu wake.

Kwa madhumuni ya utalii kwa wote napenda nisisitize umuhimu wa kuendeleza utalii wa ndani ya nchi yetu. Hili ni suala muhimu sana. Nafahamu fika Kamisheni ya Utalii ina mipango madhubuti ya kuendeleza utalii wa ndani. Lazima tuwahamasishe na kuwashajiisha wananchi wa Kisiwa cha Unguja wayatembelee maeneo ya utalii ili wayafahamu kwani inawezekana wapo wa Kaskazini wasioyajua maeneo ya Kusini na kadhalika wapo wa Kusini wasioyajua ya Kaskazini seuze ya Mashariki na Magharibi. Inawezekana wapo vile vile ndugu zetu wanaoishi Pemba wasioyajua maeneo ya Kaskazini wala ya Kusini na Mashariki wala Magharibi. Lakini inawezekana vile vile wapo wananchi wanaoishi Pemba wasioyajua maeneo ya Unguja na wale wa Unguja wasioyajua maeneo ya Pemba ambayo yamesheheni historia ya visiwa vyao yaliyoambatana na utalii. Vile vile, wapo Wazanzibari kadhaa wasioyajua maeneo maarufu ya utalii ya Tanzania Bara, kama vile Serengeti, Ngorongoro, Ziwa Manyara, Ruaha na kadhalika. Na wapo Watanzania Bara kadhaa ambao hawayaelewi maeneo ya utalii yaliopo Zanzibar, kama vile Mahamni ya Kidichi, Kizimbani, Majengo ya Kale ya Maruhubi, Majengo ya Kale ya Mkame Ndume, Mkumbuu na kadhalika. Hili ni eneo ambalo uongozi wa Kamisheni ya Utali inapaswa ilisimamie kwa nguvu zake zote.

Ndugu Washiriki,

Kwa mara nyengine tena nawashukuru wote walioandaa na kushiriki warsha hii muhimu na nakutakieni uendeshaji na usikivu mzuri na matumaini yangu ni kuwa mtatoa michango yenu bila ya khofu na taaluma mtakayoipata katika warsha hii na kutokana na utaratibu utakaowekwa mtakuwa tayari kuifikisha taaluma hii katika jamii na waumini wenzetu ili kuongeza mwangaza katika mipango yetu mikubwa ya kuleta utalii kwa wote nchini. Nawaahidi kuwa michango yenu itazingatiwa na kufanyiwa kazi kwani ni nyenzo muhimu katika kufikia lengo letu la utalii kwa wote wenye manufaa kwetu sote kama MKUZA II ulivyofafanua. Utalii kwa wote utatekelezwa kwa mafanikio iwapo tutashirikiana kwa dhati na kwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa Warsha juu ya Utekelezaji wa Dhana ya Utalii kwa wote imefunguliwa rasmi.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Popular Posts