Dkt.  Asha-Rose Migiro akizungumza wakati wa hafla hiyo, akatoa  shukrani   zake kwa  Ban ki Moon kwa kumpatia heshima hiyo ya kihistoria  ambayo   haita kaa ifutike na kwamba  ameupokea uteuzi huo kwa mikoni  miwili na   hasa kutokana na kwamba tatizo la ugonjwa wa ukimwi ni tatizo  ambalo   analichukulia kwa uzito wa aina yake.
   Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayemaliza muda wake, Dkt, Asha-Rose Migiro akimpiga picha Mwanae Pamoja na Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
  --
   Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amemteua  Naibu Katibu Mkuu  anayemaliza muda wake, Dkt, Asha-Rose Migiro kuwa  mjumbe wake maalum  katika masuala ya ukimwi na ugonjwa wa ukimwi Barani Afrika.
  Ban  Ki Moon ametangaza uteuzi huo wakati wa hafla maalum aliyoiandaa  mahsusi kwaajili ya kumuaga  Naibu Katibu Mkuu wake,ambaye anahitimisha   utumishi wake wa  miaka mitano na nusu   katika nafasi ya Unaibu katibu  Mkuu. 
  Hafla  hiyo imefanyika   siku ya alhamisi katika viunga vya Umoja wa Mataifa,  na kuhudhuriwa na wageni waalikwa  mbalimbali wakiwamo mabalozi na wakuu  wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
  “Ninatangaza  rasmi kwamba ninamteua dkt.  Asha- Rose Migiro kuwa  mjumbe wangu  maalum katika masuala ya ukimwi na ugonjwa wa Ukimwi Barani  Afrika.  Akasema  Ban Ki Moon tangazo lililoshangiliwa kwa nguvu na wageni  waalikwa.
  Akiongea  kwa hisia, Ban Ki Moon, ameeleza kwamba ingawa Migiro alikuwa naibu  katibu mkuu wake, lakini amekuwa mwalimu wake, amejifunza mengi toka  kwake na daima ataendelea kuenzi mchango wake mkubwa.
  “  Kama ni kuvaa viatu vyake, naweza kusema ningechekesha sana,  kwa ufupi  siwezi kuvaa viatu vya Migiro, amekuwa msaada mkubwa sana kwangu,  ameniwakilisha vema kila mahali nilipomtuma  hata katika mazingira  magumu na ya hatari,  kote ameniwakilisha vema sana, kama  mwalimu  wangu, na kama profesa wangu anastahili alama ya juu sana” akasema  Ban  Ki Moon na kushangiliwa.
  Akamuelezea   Migiro kama kiongozi si tu mwadilifu, lakini mwanadiplomasia   aliyebobea, aliyefanya kazi kubwa,ngumu na nzito kwa moyo mkunjufu,  uhodari , umakini, na uadilifu wa hali ya juu sana.
  “   Siyo rahisi kuelezea yale aliyoyafanya nyuma ya pazia, namna gani  alivyochapa kazi kwa nguvu,  yapo mengi makubwa ambayo Migiro ameyafanya  na  kuyakamilisha kwa uadilifu wa hali ya juu.
   Migiro ni  mwanadiplomasia aliyebobea lakini ni mtu wa vitendo, vitendo ambavyo  lazima utaona matunda yake” akabainisha Ban Ki Moon na  kuongeza “  Migiro  amefanya kazi na viongozi wagumu,  kiwamo  aliyekuwa  Rais wa Libya Muammar  Quadaff aliyethubutu hata kumrushia  katiba ya Umoja wa Mataifa, amezikuna nyonyo za watu wengi wakiwamo watu  wanyonge na wenye matatizo mbalimbali. Migoro  unaondoka, lakini Umoja  wa  Mataifa  hauta sahau mchango wako. Hapa ni nyumbani kwako, na  nitaendelea kuomba msaada wako na ushirikiano wako, bado nitaendelea  kukuhitaji” akasisitiza Ban Ki Moon Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  akatumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  kwa kumruhusu Migiro kwenda kuitumikia  jumuia ya kimataifa.
  “  Ninapenda  kutoa shukrani zangu za pekee kwa  jamhuri ya muungano wa  Tanzania, kwa kumtoa Migiro katika utumishi wake wa Umma kuja kunisaidia  , kwa serikali ya Tanzania na  watanzania nasema asanteni sana” akasema  Ban Ki Moon..
  Kwa  upande wake, Naibu Katibu Mkuu dkt. Asha-Rose Migiro amesema anaupokea  kwa mikono miwili uteuzi wa kuwa mjumbe maalum wa Katibu Mkuu katika  masuala ya Ukimwi.
  Akasema    masuala ya  ukimwi na ugonjwa wa ukimwi, ni eneo ambalo limo ndani ya  moyo wake  na kwamba anashukuru kuona kwamba Katibu Mkuu anamuamini  kwamba anaweza kumsaidia. Akaahidi kwam atalitekeleza  jukumu  hilo kwa   heshima  kubwa.
  Akamshukuru  Ban Ki Moon, kwa kumuamini kwamba anaweza kumsaidia kama naibu Katibu  Mkuu, na akamshukuru pia kwa ushirikiano mkubwa na uhusiano mkubwa  uliojengeka kati yake na Ban Ki Moon lakini pia kati yake na wasaidizi  wake.  Ushirikiano ambao anasema ulichagiza utendaji kazi  kufanikisha dira na matarajio ya  Katibu Mkuu.
  “Katibu  Mkuu amenipa heshima ya kihistoria, heshima ya kuwa msadizi wake,  ni  heshima kubwa kwangu na kwa yeyote atakayekuja kuandika historia yangu,  kwa namna yoyote ile hawezi kukwepa  kumtaja  Ban Ki Moon, naomba  nikushukuru sana kwa heshima hii kubwa uliyonipa” akasema Migiro.
  Hafla  hiyo pia imehudhuriwa  na familia ya Naibu Katibu Mkuu ikijumuisha   mume wake, Profesa  Cleophas Migiro,  mdogo wa  Naibu Katibu Mkuu, Bi.  Amina  Mtengeti na mtoto wa  mwisho wa Migiro Chansa Jasmin.
  Naibu  Katibu Migiro anakuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo na mwanamke  mwafrika wa kwanza. Lakini pia ni naibu katibu mkuu ambaye amehudumu  katika wadhifa huo kwa miaka mitano na nusu.