Taasisi  ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imeunga mkono kauli  iliyotolewa hivi karibuni na Sheikh mkuu wa Tanzania, Mufti Issa  Shaaban  Simba ya kuwataka waislamu na watanzania  kote nchini kushiriki  kikamilifu katika Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika  Agosti 26  mwaka huu.
  Akizungumza  na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mwenyekiti  wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania Sheikh Hamis  Mattaka amesema hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa baadhi ya makundi  yanayowahamasisha waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kutoshirika  zoezi la Sensa ya watu na makazi.
  Amesema   wao kama jopo la wanazuoni hawaoni tatizo la zoezi hilo kutokana na  umuhimu wake kwa taifa na kuongeza kuwa  Sensa ya watu na makazi ipo kwa  mujibu wa sheria za nchi na imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania.
  Jopo  hilo  limeiomba serikali kuweka sheria itakayozuia utoaji wa takwimu  zinazohusu dini za watanzania zinazotolewa na vyanzo mbalimbali ndani na  nje ya nchi kwa kuwa kipengele hicho si sehemu ya sensa nchini. 
  “Tunajua  kuwa serikali ilikua na nia njema kukiondoa kipengele cha dini katika  Sensa hapana budi nia njema hiyo ya serikali ilindwe kwa kuweka sheria  itakayozuia kutoa takwimu zinazohusu dini za watanzania” amesema Sheikh  Mattaka.
  Amefafanua  kuwa Sensa ya awali ya mwaka 1957 kipengele cha dini kilihusishwa na  baadaye kuondolewa katika Sensa zilizofuata kwenye madodoso ya  kukusanyia takwimu za kaya.
  “Sisi  kama jopo kila siku tunasema ili twende salama kama wananchi wa nchi  hii ni wajibu wetu  kuheshimu na kufuata sheria kwa maana ya kutii  sheria bila shuruti, kwa hiyo tunasema Sensa ya watu na makazi ni jambo  la kisheria si jambo la mitaani, hatuwezi kulumbana na kujadili jambo  ambalo liko wazi kisheria na limepitishwa na wabunge tuliowachagua sisi  wenyewe”
  Amefafanua  kuwa zoezi la Sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali kupanga  mipango ya maendeleo kwa kuwa na takwimu sahihi za watu na makazi, hali  ya kipato cha kaya, vizazi na vifo na pia kuiwezesha serikali kwapatia  huduma bora wananchi wake.
  Katika  hatua nyingine jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania  imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukusanyaji wa  maoni ya katiba.
  Aidha  jopo hilo limewataka watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hiyo  muhimu kutoa maoni ambayo yataiwezesha nchi kupata katiba itakayokidhi  matakwa ya wananchi.
  “  Sisi kama jopo la wanazuoni wa kiislamu tunawataka waislamu na  watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hii muhimu kwa kutoa maoni yao  ili hatimaye nchi yetu ipate katiba itakayokidhi matakwa ya wananchi  kwa miaka mingi ijayo” amesema Sheikh Mattaka.