Pages

Monday, June 25, 2012

TGNP wakemea matusi, kejeli na lugha chafu Bungeni

HALI YA MJADALA WA BUNGE LA BAJETI
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP, tumekuwa tukifuatilia kwa karibu sana mjadala wa
bajeti ya serikali ya mwaka wa Fedha 2012/2013 katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, tumestushwa na kusikitishwa jinsi ambavyo baadhi ya
wabunge wanaonesha tabia ya kutumia nafasi na dhamana waliopewa na wananchi vibaya, kinyume na matarajio.

Bajeti
ya mwaka 2012/2013 imekuja wakati ambapo wananchi walio wengi wanashuhudia hali ngumu ya maisha kutokana na mfumko wa
bei, ukosefu wa ajira, ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, wazee na watoto
na kudorora kwa hduma zote muhimu kwa wananchi ikiwemo , maji, afya, nishati,
elimu na huduma za kijamii hususani kwa walioko pembezoni. Kwa mantiki hii
wananchi wanamategemeo makubwa kwa Bunge na wabunge katika mjadala huo.

Kinyume
na matarajio hayo, tumesikitishwa na tabia ya baadhi ya wabunge kutumia Bunge
kama sehemu ya malumbano ya kisiasa na kutambiana elimu, vyeti na sifa binafsi
badala ya kujadili na kufanya maamuzi yenye manufaa kwa nchi yetu.

Tumesikia
matumizi ya lugha chafu ndani ya Bunge zikitolewa na baadhi ya wabunge, dharau,
jeuri, na kejeli badala ya kujadili bajeti kwa misingi ya mahitaji ya wananchi ambao wanateseka kwa ugumu wa maisha.

TGNP
tunakemea na kukataa matumizi mabaya ya muda na nafasi adimu waliopewa wabunge kwa gharama kubwa za wananchi kutumika
vibaya, kujadili maisha ya watu binafsi, kushambulia vyama vya siasa, kufanya
utani badala ya kujadili jinsi ya kusaidia na kuboresha maisha ya Watanzania waliowengi.

Sisi
kama wanaharakati na watetezi wa ukombozi wa wanawake, haki za bindamu,
demokrasia, na usawa wa kijinsia tunawataka wabunge na ofisi ya Spika kufanya yafuatayo:

* Kuheshimu kwa dhati muda na gharama za walipa kodi zinazowafanya wawepo Dodoma, mijadala ilenge kuleta tija, mageuzi ya kiuchumi na kubadilisha hali duni na umasikini wa Mtanzania ambaye amebaki kupata mlo mmoja kwa siku na wengine hawana kabisa.

* Wabunge wajikite kuchambua, kujadili bajeti na kuishauri serikali namna ya kuboresha na kutekeleza ahadi , mipango yake ya kiuchumi hasa ule wa Miaka mitano (FYDP),MKUKUTA11, Mpango wa Maendeleo(Vision 2025), kwa kurejea Hali halisi ya uchumi wa wananchi kwa sasa iliyosomwa na Waziri wa Nchi (Uhusiano).

* Wabunge kuacha mara moja lugha chafu za matusi, kejeli, dhararu, vurugu na kuchana nyaraka za mijadala Bungeni kwani hiyo ni kuwatusi wananchi walalahoi, ambao ni wapiga kura.

* Spika asiruhusu ushabiki wa maoni ya mtu binafsi au kikundi bali hoja za bajeti ya serikali ambayo inawagusa wananchi wa Tanzania.

Kwa
kushirikiana na wananchi tutaendelea kufuatilia na kudai
uwajibikaji wa wabunge na viongozi wa serikali katika nagzi zote kwa maendeleo
ya Taifa letu. .

Imetolewa
na:

…………………
Usu Mallya
Mkurugenzi
Mtendaji wa TGNP

Popular Posts