Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib  Fereji akitoa taarifa rasmi ya serikali kuhusiana na maadhimisho ya  mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanayofikia kilele chake tarehe  26/06/2012 kila mwaka.Picha na Hassan Hamad-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
  ---
   Janatarehe 26/06/2012,  ni siku ya  maadhimisho ya mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya duniani.  Tamko la kimataifa kuhusiana na matumizi ya dawa za kulevya ni kwamba  bado dawa za kulevya zinaendelea kuathiri afya za binadamu na ndio maana  juhudi za mapambano hayo zikaendelezwa. 
 Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari huko ofisini kwake Migombani Mjini Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Fereji amesema vita dhidi ya dawa za kulevya ni ngumu sana, lakini inawezekana iwapo jamii itashirikiana dhidi ya mapambano hayo.
   “Hii ni kutokana na ukweli kuwa wanaojishughulisha na biashara hii ni  watu wenye fedha nyingi na ujanja kupita kiasi, inafika wakati watu hawa  wanashusha mzigo baharini na kwenda kuuzamia kwa wakati wao na  kuupeleka wanakokujua wao. Na kama wakiamua kuhonga hawahongi laki moja  au mbili, hesabu hiyo inakuwa kwa dola, sasa fikiria”, aliweka wazi Mhe.  Fatma Fereji. 
    Hata hivyo amesema serikali inajitahidi kuongeza nguvu za kupambana na  uingizaji na matumizi ya dawa hizo, sambamba na kusaidia kupata hifadhi  na mafunzo ya amali kwa vijana walioamua kuachana na dawa hizo. 
   Amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali hadi sasa ni  pamoja na kutenga shilingi milioni mia moja kwa ajili ya matayarisho ya  ujenzi wa nyumba za kuwaendeleza vijana walioamua kuachana ya dawa za  kulevya (sober houses) huko Tunguu ambazo zikimalizika zitatoa huduma  zote bure kwa vijana hao.  Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “Tujenge jamii yenye afya  bila ya dawa za kulevya”.