Pages

Saturday, June 30, 2012

KLABU YA SIMBA KUSHIRIKI KOMBE LA URAFIKI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KLABU ya Simba inapenda kutangaza kuwa itashiriki katika michuano ya Kombe la Tanzania (Urafiki) iliyopangwa kuanza visiwani Zanzibar Jumatatu ijayo.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange, maamuzi ya kushiriki katika mashindano hayo yamefikiwa baada ya majadiliano baina ya uongozi, benchi la ufundi na Kamati ya Ufundi ya Simba.

“Tumeamua kushiriki kwa sababu tumeona haitakuwa vema kufanya hivyo wakati watu wa Zanzibar wametupa heshima kubwa ya kutualika kwenye michuano hii. Kombe la Tanzania lina maana kubwa kwa sasa kutokana na hali halisi ya kisiasa na kijamii iliyopo visiwani humo kwa sasa,” alisema.

Makamu alisema zaidi ya kushiriki michuano hiyo, Simba pia itatumia fursa hiyo kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na Kombe la Kagame lililopangwa kufanyika kuanzia Julai 14 mwaka huu.

Pia, alisema Simba itatumia ziara hiyo kupeleka kombe la Ligi Kuu ya Vodacom kwa wana Simba wa Zanzibar ambao walichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ubingwa Vodacom na pia.

“Tusisahau pia kwamba kabla ya kucheza mechi yetu ya mwisho dhidi ya watani wetu wa jadi Yanga ambayo tulishinda kwa idadi ya mabao 5-0, Simba ilikwenda kuweka kambi Zanzibar,” alisema Kaburu.

Simba itaanza michuano hiyo siku ya Jumatatu ambapo itacheza na Mafunzo ya Zanzibar katika pambano lililopangwa kufanyika usiku. Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Jumatatu jioni lakini imesogezwa mbele hadi Jumatatu usiku.

Jumla ya timu nane zinashiriki katika michuano hiyo ambapo Waekundu wa Msimbazi wapo katika kundi A lenye timu za Simba, Azam, Mafunzo na timu ya soka ya taifa ya vijana ya Zanzibar wenye umri wa chini ya miaka 23 (Karume Boys).

Simba na Express kucheza Taifa

MABINGWA wa soka wa Tanzania, Simba SC, wanatarajiwa kucheza na mabingwa wa soka wa Uganda, Express FC, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, maandalizi yote kwa ajili ya pambano hilo yamekamilika na kwamba kikosi cha Simba kitaundwa na wachezaji wapya na wa zamani.


SIMBA SPORTS CLUB

P.O.BOX 15318 | TEL+255 222183330 |FAX +255 222183330 |MSIMBAZI/MCHIKICHI STREET | DAR ES SALAAM | TANZANIA | EMAIL simbasportsclub@yahoo.com|

WEBSITE www.simba.co.tz| AFFILIATED TO TFF, DRFA and IDFA

Popular Posts