Jumuiya Ya Uamsho Na Mihadhara Ya  Kiislamu (JUMIKI) imepinga uvumi uliosambazwa nchini kuwa jana kungekua  na maandamano ya Jumuiya hiyo na kudai kuwa propaganda hizo zinaendeshwa  na baadhi ya watendaji katika jeshi la polisi na usalama wa taifa ambao  hawaitakii mema Jumuiya yao.  
    Hayo yamesemwa na Amiri wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Ahmed wakati  alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari  Maelezo ZanzĂbar kuhusiana na tuhuma ambazo wamezitoa kwa Jeshi la  Polisi dhidi ya Jumuiya yao. 
    Amedai kuwa Jumuiya haijapanga maandamano kwani ni taasisi inayofanya  kazi zake kisheria nakwamba hata ikitokezea kufanya maandamano basi  watafuata taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kulitaarifu rasmi  Jeshi la Polisi. 
    Aidha amedai kuwa kuna mkakati wa muda mrefu wa kutaka kuwabatiza  viongozi wakuu wa jumuiya hiyo kesi za ugaidi hususan Amir Mkuu wa  jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikh Farid Hadi Ahmed ili kuzima vuguvugu  la kudai Zanzibar huru.
    Shekh Faridi amedai kuwa inasemekana kuna mahusiano makubwa baina ya  watendaji ndani ya Jeshi la polisi pamoja na baadhi ya wageni  wanaosadikiwa kuwa ni raia wa Marekani juu ya kuutekeleza mkakati huo  baada ya kuwa tayari umeshakamilika. 
    Amedai kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za kiraia ambao umekuwa  ukifanywa na Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kuwanyima haki ya kufanya  mihadhara yao ndani ya Misikiti  ambapo Juni 17 mwaka huu wananchi  mbalimbali walijeruhiwa kwa mabomu katika vijiji vya Donge,Mkwajuni na  Mahonda. 
    Ameliomba Jeshi la Polisi kufanya kazi zake za kulinda usalama wa  wananchi na mali zao na kuacha kufanya kinyume chake kwani huko ni  kuchochea chuki kati ya Jeshi hilo na raia. 
    Amesisitiza haja ya wazanzibari kuungana na kuachana na Itikadi zao za  kivyama katika kudai hadhi ya Rais na mamlaka ya Nchi ya Zanzibar ndani  na nje ya Zanzibar pale tume ya mabadiliko ya Katiba itakapoanza kazi  zake. 
    Kwa upande wake Naibu Naibu Amir Jumuiya Ya Uamsho Na Mihadhara Ya  Kiisilam Sheikh, Azan Khalid Hamdan amewaomba wanahabari nao kuwa makini  katika taaluma yao kwa kufanya usawa wa taarifa ambazo wamekuwa  wakizitoa. 
    Hivi karibuni Jumuiya hiyo ilitangaza rasmi kushiriki kikamilifu katika  zoezi zima la kutoa maoni yao katika mchakato wa kupata Katiba mpya ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kubadili msimamo wao wa awali wa  kuisusia Tume hiyo. 
 MWISHO.
 IMETOLEWA NA 
  HABARI MAELEZO ZANZIBAR