Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na  Kiongozi wa Ujumbe wa Taasisi inayoshughulikia Gesi Nchini Ras Al  Khaimah { RAK Gas } Bwana Kamal Ataya hapo Ofisini kwake Vuga Mjini  Zanzibar. Ujumbe huo umekuja Zanzibar kufuatia mazungumzo ya pande hizo mbili  wakati wa ziara ya Balozi Seif Nchini Ras Al Khaimah hivi karibuni.  
  Kiongozi wa Ujumbne wa Viongozi wa Taasisi inayoshughulikia masuala ya  Gesi Nchini Ras Al Khaimah {RAK Gas } Bwana Kamal Ataya akibadilishana  mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo  Ofisini kwake vuga Mjini Zanzibar.    Picha na Saleh Masoud-Ofisi Ya   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
  --
   Ras Al-Khaimah imejipanga vyema kuhakikisha  Maendeleo ya Kiuchumi na  Ustawi wa Jamii wa Taifa hilo Sambamba na Visiwa vya Zanzibar yanakua  kwa kiwango kinachoridhisha. 
   Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Taasisi inayojihusisha na Masuala  ya Gas { RAK GAS } ya Nchini Ras Al Khaimah Bwana Kamal  Ataya  aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi watano wa Taasisi hiyo wakati  akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 
   Bwana Kamal na ujumbe wake wako Zanzibar kufuatia mazungumzo yao na   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati wa ziara yake  Nchini Ras Al Khaimah hivi karibuni .
    Alisema lengo la mazungumzo hayo ya kujenga uhusiano ni kufanya kazi  pamoja katika kuona Maendeleo ya Mataifa hayo Mawili yanakuwa Kiuchumi. 
   Bwana Kamal Ataya alifahamisha kwamba Taasisi yao imejikita zaidi katika  uimarishaji wa Sekta za Uchumi, Kilimo, Uvuvi, Elimu na Hata Sekta ya  Afya. “ Tumejipanga vyema na tuko tayari  pia kutoa Mafunzo katika Sekta ya  Mafuta hasa zaidi katika fani ya ufundi”. 
   Alisisitiza Bwana Kamal Ataya. Kiongozi huyo wa Taasisi ya RAK Gas alimueleza Balozi Seif kwamba dalili  za matumaini zimeanza kujichomoza kufuatia Mazungumzo yao ya mwanzo na  baadhi ya Viongozi na Watendaji wa sekta tofauti hapa Zanzibar. 
   Aidha Bwana Kamal alieleza kuwa taasisi yake itahakikisha kwamba yale  maeneo yatakayofikia hatua za makubaliano ya pande hizo mbili yanaanza  kuchukuliwa hatua mara moja. 
   Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza  Ujumbe wa Taasisi hiyo kwa hatua zake ilizochukuwa za kufuatilia  makubaliano ya pande hizo mbili katika kipindi kifupi.
    Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa huo kwamba Taifa lina matumaini makubwa  ya kunyanyuka zaidi kwa Uchumi wake kutokana na  muelekeo wa Taasisi  hiyo kuelekeza nguvu zake hapa Zanzibar. 
   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba  Serikali imekusudia kuelekeza nguvu zake katika kuwapatia elimu zaidi  Vijana katika nyanja ya Utalii kwa lengo la kujijengea uwezo wa ajira  katika Sekta hiyo ambayo imekuwa muhimili mkubwa wa Uchumi. 
   Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na Hoteli nyingi za Kitalii za Daraja  la juu lakini idadi kubwa ya wafanyakazi wake inaonekana kutoka nje ya  Zanzibar. “ Zipo Hoteli nyingi za Kitalii ambazo zimetoa ajira kadhaa hapa  Zanzibar lakini kinachoonekana Vijana wengi wanakosa kuajiriwa kutokana  na ukosefu wa taaluma ya fani hiyo”. Alifafanua Balozi Seif. 
   Ujumbe wa Taasisi hiyo ya Masuala ya Gas { RAK GAS } ya Ras Al Khaimah  umekuja kuangalia maeneo yepi ya mwanzo yanaweza kuchukuliwa hatua za  utekelezaji wa makubaliano ya pande hizo mbili katika kuimarisha Uchumi  wa Nchi hizo. 
  Na
   Othman Khamis Ame 
  Ofisi Ya   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar