Pages

Saturday, August 11, 2012

AJALI ILIYOUWA WANAKWAYA 11 WA KENYA MTO WAMI

Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Makole Mkoa wa Pwani wakiangalia ajali ya gari iliyotokea leo katika eneo la Mto Wami na kusababisha vifo vya watu 11 wote wakiwa raia wa Kenya.
Basi lililokuwa limewabeba raia wa Kenya waliokuwa wakielekea jijini Dar es salaam kwa ajili ya mikutano ya injili likiwa limetumbukia katika korongo jirani na Mto Wami na kuua watu 11 katika Kijiji cha Makole Mkoa wa Pwani.
Baadhi ya abiria walionusurika wakiwa katika eneo la tukio kabla ya kupata msaada.Picha Zote na Mdau Francis Dande
--
WATU 11 wanaoaminika kuwa raia wa Kenya wamefariki dunia papo hapo, huku wengine saba wakiwa mahututi baada ya mabasi waliyokuwa wakisafiria kutoka Nairobi kwenda Dar es Salaam kupata ajali katika Mto Wami mkoani Pwani.Mbali na vifo hivyo, ajali hiyo pia ilisababisha majeruhi 25 na saba kati yao waliripotiwa kuwa mahututi na walipelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha kwa matibabu.
Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Makole, wilayani Bagamoyo wakati abiria hao ambao ni wanakwaya walipokuwa wakisafiri kutoka Kenya kwenda Dar es Salaam kushiriki katika tamasha la uimbaji.

Ajali hiyo ilitokea jana saa 11 alfajiri ikihusisha magari manne, mawili kati yake yakiwa ni mabasi hayo yakitokea Kenya na malori mawili ya hapa nchini.Tukio hilo pia lilifunga Barabara Kuu ya Chalinze - Segera kwa zaidi ya saa nane hivyo abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea na kutoka mikoa ya Kaskazini ikiwamo nchi ya Kenya kwenda na kutoka Dar es Salaam kukwama.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu alisema raia hao wa Kenya ni waumini wa Kikristo na walikuwa wakielekea Dar es Salaam kwenye tamasha la kwaya.

Ajali ilivyotokea
Mangu alisema awali, mabasi hayo yalikuwa yametokea Segera, huku yakiwa yameongozana na moja ilipofika eneo la Makole ghafla liliyumba na kupinduka kisha kutumbukia kwenye korongo.Alisema basi la pili lililokuwa likifuatia nyuma lilipita eneo hilo, lakini baada ya mita 500, dereva alipigiwa simu na mwenzake kuwa amepata ajali na wametumbukia korongoni hivyo ikawalazimu kugeuza kurudi nyuma ili wakawasaidie wenzao.

“Haikuwa rahisi kwa mtu ama gari kuliona haraka hivyo wenzao walipofika hapo nao walipita bila kujua kama kuna gari limeanguka, lakini muda mfupi tu dereva alipigiwa simu na mwenzake akimjulisha kuwa amepata ajali na wametumbukia mtaroni,” alisema Kamanda Mangu.

Alisema baada ya kugeuza na kurudi eneo la ajali, baadhi ya abiria walishuka ili kuwasaidia wenzao na wakati wakiwa kwenye harakati hizo, ghafla lilitokea lori ambalo lililiparamia basi la pili ambalo pia lilitumbukia kwenye korongo.

Kamanda huyo aliongeza kuwa, wakati basi hilo likigongwa, tayari lilikuwa limegeuzwa kuangalia uelekeo wa Chalinze na kwamba baadhi ya abiria walikuwamo ndani.
Alisema baada ya lori hilo kuligonga basi hilo, liliendelea mbele kwa kasi na kugongana uso kwa uso na lori jingine lililokuwa likitokea uelekeo wa Segera, hivyo kufunga barabara hiyo kwa zaidi ya nane.

“Kwa hiyo njia ilikuwa imefungwa kuanzia saa 11:00 alfajiri hadi saa 6:30 mchana baada ya askari wetu kufanikiwa kuyaondoa malori hayo kwenye barabara kuu na sasa (jana) safari zinaendelea kama kawaida,” alisema Mangu.

Popular Posts