Serikali, kuanzia leo tarehe 01 Agosti, 2012, imewavua hadhi  ya ukimbizi wakimbizi 38,050 wa kutoka Burundi wanaohifadhiwa katika  kambi  ya wakimbizi ya Mtabila iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
 Uamuzi huu wa kuwavua hadhi ya ukimbizi umefanywa na Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kwa Mamlaka aliyopewa  chini ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Wakimbizi.
 Kufuatana na Sheria hiyo mkimbizi anapoteza hadhi ya ukimbizi  kama mazingira yaliyomfanya kuwa mkimbizi yatakuwa hayapo tena, na  atavuliwa hadhi hiyo kama ataendelea kukaidi maagizo halali ya kumtaka  kurejea kwao kwa hiari.
 Hatua ya kuwavua hadhi ya ukimbizi wakimbizi hawa imefikiwa  baada ya Serikali za Tanzania na Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa  la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kujiridhisha kuwa hapakuwa tena na sababu  ya kuendelea  kuwahifadhi wakimbizi hao baada ya hali ya amani kurejea  nchini mwao na hivyo kuwataka kurejea kwao.
 Zoezi la kuwasaili wakimbizi waliopo katika kambi ya  wakimbizi ya Mtabila lilifanyika kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba  mwaka 2011 kwa lengo la kubaini kama walikuwepo wakimbizi wenye sababu  za msingi za kuendelea kuwepo nchini, ambapo ilibainika kuwa wakimbizi  38,050 hawakuwa na sababu za kuendelea kuwa wakimbizi.
 Kufuatia matokeo ya zoezi hilo, Kikao cha Pande Tatu,  kilichojumuisha wawakilishi wa Serikali  za Tanzania na Burundi na  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kilifanyika  jijini Bujumbura nchini Burundi tarehe 22 Februari, 2012 na kukubaliana  kwa pamoja kuifunga kambi ya Mtabila ifikapo tarehe 31 Desemba, 2012.
 Baada ya kuwavua hadhi ya ukimbizi, raia hawa wa Burundi sasa  wataendelea kusaidiwa kurejea kwao kwa hiari hadi tarehe 31 Desemba  mwaka huu, ambapo Kambi hiyo ya Mtabila itafungwa rasmi, na wale ambao  watakuwa hawajaondoka baada ya tarehe hiyowatachukuliwa kuwa ni  wahamiaji haramu, na kushughulikiwa kufuatana na Sheria ya Uhamiaji.
 Historia ya hifadhi ya wakimbizi hapa nchini ilianza tangu  mwaka 1961 ambapo Tanzania ilikuwa na idadi kubwa ya wakimbizi kutoka  nchi mbalimbali za Afrika, idadi ambayo katika miaka ya tisini ilifikia  takribani milioni moja, 641,386 kati yao wakiwa ni wakimbizi kutoka  Burundi.
 Zoezi la kuwarejesha  kwao wakimbizi wa Burundi lilianza  rasmi mwaka 2002 baada ya nchi yao kurejea katika hali ya amani na hadi  sasa kambi nane zilizokuwa zikihifadhi wakimbizi toka Burundi  zimefungwa. Kambi hizo ni Karago, Mtendeli, Kanembwa na Nduta zilizokuwa  wilayani Kibondo, na Muyovosi iliyokuwa wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
 Kambi nyingine zilizofungwa ni Kitali iliyokuwa wilayani Biharamulo, Lukole A na B zilizokuwa wilayani Ngara, mkoani Kigoma.
 Kambi ya wakimbizi ya Mtabila ndiyo itakuwa ya mwisho  kufungwa katika mlolongo wa kambi zilizokuwa zikihifadhi wakimbizi  kutoka Burundi hapa nchini.
 Imetolewa na 
 Isaac J. Nantanga:
 MSEMAJI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI