Kwenye barua yake kwenda kwa uongozi wa juu wa gazeti la mwananchi, hii ni sehemu ya barua yake.
Nasikitika kutumia nafasi hii kukuandikia kukutaarifu kuwa gazeti lako  la Mwananchi la Julai 23, 2012, katika habari yake iliyoongoza ukurasa  wa kwanza (lead story) limenilisha maneno na kunikuu isivyo sahihi.
Katika habari hiyo yenye kichwa cha habari kisemacho “Wabunge  wamsafishia Zitto njia ya urais 2015,” gazeti lako limeandika hivi “Mdee  aliyepewa nafasi ya kuwasalimia wananchi alisema amekuwa na Zitto tangu  Chuo kikuu cha Dar es Salaam na kwamba kutokana na ujasiri na umahiri  wake katika kutetea masilahi ya wanyonge na taifa, anafaa kuwa mmoja wa  viongozi wa juu katika Taifa.”
Gazeti lako pia katika aya iliyofuata limenukuu kuwa mimi nimesema;
*“Ndugu zangu watu wa Kigoma, kwa kweli mna bahati sana, achilia mbali  kuwa na vipaji katika sanaa ya muziki na michezo hasa mpira wa miguu,  lakini mna wanasiasa wakali ambao ni tishio hapa nchini. Mimi namkubali  sana Zitto Kabwe na ninaamini kuna siku atakuwa kiongozi wa juu katika  nchi yetu," alisema Mdee”
Nasikitika kusema kuwa gazeti lako limeandika habari zisizo za kweli kwa  kunilisha *maneno na kudai kuwa mimi ndiye nimesema maneno hayo, kisha  kuyaweka kwenye nukuu, likisema kuwa ni nukuu yangu. Sijajua nia au  kusudio la gazeti lako kuamua kupotosha ukweli na kushindwa kabisa  kuninukuu kwa usahihi, kama inavyotakiwa katika misingi ya taaluma ya  habari.
Nasikitika pia kusema kuwa gazeti lako ambalo limeonekana kujijengea  heshima miongoni mwa wasomaji wa kada mbalimbali nchini na hivyo  linapaswa kuwa mfano wa kuigwa, linaweza kusigina misingi ya uandishi wa  habari na hususan katika kufuata maadili ya taaluma hii muhimu, kwa  kiwango cha kufanya moja ya dhambi kubwa ya kukilisha maneno chanzo cha  habari.
Kwa ajili ya kutunza heshima ya gazeti lako, lakini pia kwa ajili ya  maslahi mapana ya taaluma ya habari na jamii ya Watanzania, nakuandikia  kulitaka gazeti lako likanushe maneno liliyoninukuu katika toleo hilo la  Julai 23, 2012. Ni vyema sana hilo likafanyika kwa uzito unaostahili  kama ilivyoandikwa katika toleo hilo.
Habari hiyo imeniletea usumbufu mkubwa hasa kwa wanachama wa chama  changu, CHADEMA, ambao wanajua kuwa chama chao makini ni mahiri katika  kufuata katiba, kanuni na taratibu katika kuendesha mambo yake kwa  manufaa ya watu wote. Napenda kuwa mmoja wa Watanzania makini na  viongozi wanaojua wajibu, ikiwemo kufanya nini na kusema nini, mahali  gani na wakati gani.
Nakutakia utekelezaji mwema katika hilo.
                      -