TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Arusha, Tanzania.
Kituo  cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha kupitia hospitali yake ya AICC  kitaendesha kampeni ya kupima kisukari bure kwa wakazi wa Arusha ili  kusaidia wananchi kutambua kama wana ugonjwa wa kisukari au wapo katika  hatari ya kuugua ugonjwa huo.
Kampeni  hiyo itafanyika kesho (terehe 26-07-2012) katika hopitali ya AICC  iliyopo jijini Arusha ambapo madaktari wa hospitali ya AICC kwa  kushirikiana na madaktari wa wanaohudhuria mkutano wa Shirikisho la  Madaktari wa Kimataifa pamoja na madaktari kutoka Chama cha Ugonjwa wa  Kisukari Tanzania wataendesha zoezi la upimaji huo.
Mkurugenzi  Mwendeshaji wa AICC, Bwana Elishilia Kaaya, amesema kuwa mbali na  kupima kisukari, madaktari hao pia watatoa ushauri wa namna bora ya  kuishi na jinsi ya kuzuia madhara ya kisukari kwa wale watakao kuwa  wamekutwa na ugonjwa huo.
 “Hospitali  ya AICC inatambua umuhimu wa afya za wakazi wa Arusha na Watanzania kwa  ujumla na ndio maana tumeona ni vema kufanya kampeni hii ya kupima  kisukari. 
Napenda  kutumia fursa hii kuwaalika wakazi wote wa Arusha na vitongoji nyake  kufika kwa wingi kwani mbali na kupima pia itatolewa elimu na ushauri  kutoka kwa wataalamu hao.” alieleza Kaaya.
Kwa  mujibu Mkurugenzi Mwendeshaji, upimaji huo utaenda sambamba na mkutano  wa kwanza wa Shirikisho la Madaktari wa Kisukari wa Kimataifa ambao kwa  mara ya kwanza unafanyika hapa nchini.
 Mkutano  huo utafanyika katika kituo cha AICC ambapo madaktari wanaohudhuria  mkutano huo na wale kutoka Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania  watatoa huduma ya upimaji katika zoezi hilo.
“Tunaamini  baada ya kampeni hii wananchi watakuwa wamepata ufahamu juu ya hali ya  afya zao na kutumia vema ushauri wa madaktari kwa ajili ya kujikinga na  kuzua athari za ugonjwa huo”, alielezea Kaaya.
Mbali  na kuendesha kampeni hii, hospitali ya AICC imeanzisha kitengo maalumu  cha kisukari ambapo kila wiki madaktari hutoa huduma za matibabu na  ushauri kwa wagonjwa wa kisukri.
Ugonjwa  wa kisukari umekuwa ukiongezeka kwa kasi duniani ambapo taarifa za  Shirika la Afrya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2011  watu milioni 366 walikuwa wanaugua ugonjwa wa kisukari na mwaka 2030  idadi inakadiriwa kufika milioni 552.