NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
 SERIKALI  imesema kuwa hakuna malipo  ya kiasi  kidogo cha fedha kilicholipwa kwa  waathirika wa mlipuko wa  mabomu ya  Kambi ya  jeshi  ya  Mbagala yaliyotokea mwaka 2009 kama ilivyoripotiwa na gazeti  moja la kila wiki la hapa nchini hivi karibuni. 
Akizungumza  na Idara ya Habari( MAELEZO) jana ofisini kwake , Mkuu wa Mkoa wa Dar  es Salaam, Said Meck Sadick alisema hakuna fidia ya Shs. 1400  na Shs.  2500 iliyotolewa kuwa ni ya uharibifu wa jumla ya fidia za malipo kwa  wahanga hao, bali malipo hayo ni tofauti ya kiasi cha fedha  kilichokuwa  kinadaiwa na wahanga hao ambacho kilichobakia.
‘’  Unajua malipo ya wahanga  hao yalifanyika katika awamu mbili.  Hivyo  kiasi cha fedha  cha malipo hayo yaliyotolewa katika hundi hizo , ambayo  iliripotiwa katika gazeti hilo ni malipo ya awamu ya tatu.  Malipo hayo  ni tofauti ya fedha  kilichokuwa  kinadaiwa na si kweli kuwa wahanga  hao walilipwa fedha hizo kama jumla ya fidia za malipo yao,’’ alifafanua  Mkuu huyo wa Mkoa.
Mkuu  huyo wa Mkoa, aliongeza kuwa habari hiyo iliyoandikwa  sio sahihi na  haikufuata maadili ya uandishi wa habari kwani hakuweka wazi usahihi wa  taarifa hiyo.Serikali haijamdhulumu mtu yeyote, bali inalipa kutokana  malipo stahili.
‘’Ninaomba  waandishi wa habari waandike habari walizozifanyika utafiti wa kina wa  pande zote ilikuepusha utoaji wa taarifa zisizosahihi,’’ alisisitiza.
Aidha  Mkuu huyo alisema malipo ya waathirika hao yanatolewa kwa awamu tofauti  na kwa idadi ya watu maalum, kwa sababu ya kuepusha utoaji wa malipo  yasiyostahili. Hivyo aliwataka waathirika hao kuvuta subira kwa  kuwa  malipo hayo bado yanaendelea.
Naye  Mtathimini Mkuu wa malipo hayo, Victor  Ndonne akizungumzia kuhusu  suala hilo alisema hundi za malipo ya sh. 1000 na zilizotajwa hapo juu  ni za tofauti ya kiasi cha fedha kilichobakia baada ya  wahanga hao  kutoridhika na malipo hayo yaliyotolewa katika awamu ya kwanza na awamu  ya pili.
‘’  Fedha hizi zimelipwa baada ya kufanyika kwa tathimini mpya Agosti 18  mwaka 2011, ambapo ilioneka baadhi ya wahanga  hawakurithika  na fidia  walizolipwa,’’ alisema Ndonne .
Alifafanua  kuwa orodha ya wahanga wanaodaii malipa yao ni 2,575,  hivyo hundi  zilizotolewa hadi sasa ni 295 kwa ajili ya malipo hayo, ambapo hundi 244  zimeshakabidhiwa kwa wananchi husika, hundi nyingine 18 majina  yamebandikwa katika eneo la Mbagala Kuu na Ofisi ya Mkurugenzi  wa  Wilaya ya Temeke, zaidi ya wiki moja iliyopita na wanasubiri  wananchi waende kuchukua.
Ndonne  alisema hundi 32 zimeonekana kuwa na matatizo mbalimbali  mfano majina  ya vitambulisho vyao ni tofauti na yaliyoandikwa katika hundi na majina  mengine ya hundi hizo wahusika wameshafariki dunia. Aidha aliongeza kuwa  hundi moja imeonekana majina yamejirudia.
Alisema  kuwa hundi za malipo ya fedha ya wahanga hao  zilitolewa kabla ya  mwisho wa mwaka wa fedha uliopita. Malipo ya fedha zingine zitatolewa  mwaka huu wa fedha wa 2012/2013 mara baada ya Serikali kuidhinisha.