
  Balozi  wa China nchini Tanzania Lu Younqing (kushoto) akifurahia jambo wakati  wa mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam ambapo pamoja  na mambo mengine amesema nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano  kati yake na Tanzania katika Nyanja za Kilimo, Nishati, Biashara na  Viwanda. Kulia ni mshauri wa masuala ya Sayansi na Teknolojia wa ubalozi  huo Bw. Liu Dong.
   Baadhi ya wafanyakati wa ubalozi wa China nchini Tanzania wakifuatilia mkutano kati ya balozi wa nchi hiyo  Lu Younqing na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam.
  --
  Na. Aron Msigwa – MAELEZO.-Dar es salam.  Tanzania  itaendelea kunufaika katika nyanja za kilimo, Biashara, uwekezaji wa  nishati, Biashara na viwanda kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya  nchi hizi. 
   Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salam na Balozi wa China nchini Tanzania Bw. Lu Youqing alipokutana  na  waandishi wa habari kuelezea mafanikio yaliyopatikana kutokana na  ushirikiano uliopo kati ya nchi hizi kwa mwaka 2010 na 2012. 
   Balozi  Lu amesema sasa kiwango cha biashara kimeongezeka kutokana na juhudi  mbalimbali zilizofanyika kuondoa vikwazo  vilivyokua vikiwakabiri  
   wafanyabiashara kutoka Tanzania. 
   Amesema kiwango cha uwekezaji kwa mwaka 2011 nchini Tanzania kinafikia dola za kimarekani milioni 339  huku  akifafanua kuwa kuna makampuni mbalimbali yaliyowekeza nchini Tanzania  kwenye kilimo , nishati, shughuli za usafiri wa meli na miradi ya  televisheni kwa mfumo wa digitali. 
   Amefafanua  kuwa tayari China na Tanzania zimekubaliana katika utekelezaji wa  miradi mbalimbali ya kimaendeleo ukiwemo mradi wa uzalishaji wa nishati  ya umeme wa Mchuchuma utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha kiasi cha  megawati 600.  
   Balozi  Lu ameongeza kuwa Tanzania na China kwa muda mrefu zimekuwa  zikishirikiana katika sekta ya biashara huku akitoa mfano wa maonyesho  ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam yaliyomalizika hivi karibuni  katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es salam. 
   Amesema  ushiriki wa China katika maonyesho hayo ni ishara tosha ya ushirikiano  wa kibiashara kati ya Tanzania na China kwa kuwawezesha wananchi wa  Tanzania kuona bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa nchini China zikiwa na  ubora na gharama nafuu. 
   “Nakiri  wazi kuwa maonyesho yaliyomalizika katika viwanja vya sabasaba  yaliwawezesha wafanyabiashara kutoka China kuja Tanzania kuonyesha kazi  wananzozifanya, hiyo ni ishara tosha ya ushirikiano, watanzania waliweza  kuona na kujipatia bidhaa kutoka China kwa gharama nafuu huu ni mfano  tu wa ushirikiano uliopo”