MAMBO YA MSINGI KATIKA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA 1977
Muhtasari
1. JAMHURI YA MUUNGANO NA UTAIFA
2. MGAWANYO WA MAMLAKA
a. Mamlaka Tatu
i. Mamlaka ya Mambo ya Muungano
ii. Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar
iii. Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara
3. SERIKALI MBILI; MUUNDO WAKE
4. UENDESHAJI WA MAMLAKA TATU
a. Maamuzi ya Kisera
b. Utungaji Sheria
c. Usimamizi na Uendeshaji;
i. Fedha na Bajeti
ii. Utawala;
5. UTATUZI WA MIGOGORO YA MUUNGANO
SEHEMU YA PILI- UFAFANUZI NA MASUALI MUHIMU
JAMHURI YA MUUNGANO NA UTAIFA
Ibara ya 1 ya Katiba inatamka; “Tanzania ni Nchi Moja na ni Jamhuri ya Muungano…”
Ibara inaweka bayana kuwa Jamhuri ya Muungano ni Taifa moja lenye mfumo  wa Jamhuri iliyoundwa kwa mfumo wa Muungano. Ibara hii imeandikwa sawa  na vifungu vya Katiba vya nchi ambazo hazina Muungano kama vile Kenya,  Uganda na Uturuki. Nchi nyingi zenye Muungano imara kama vile  Switzerland na hata Urusi Katiba inaeleza bayana kuwa Taifa hilo ni  Muungano wa Nchi au Washirika gani. Aidha hueleza hadhi ya Washirika hao  ndani ya Muungano au Shirikisho hilo.
Masuali muhimu:
a. Kwa vile Taifa limeundwa kwa mfumo wa Muungano, je washirika wa Muungano huo ni wapi na ni wangapi;
b. Nini hatma ya washirika hao baada ya kuungana; wapo au hawapo tena  (Angalia uhusiano wa suala hili Orodha ya Pili, Jadweli la Kwanza kuhusu  kuendelea kuwepo kwa Sheria ya Muungano ya 1964 na pia Orodha ya Pili  hasa vipengele vya 1,2 na 3);
c. Nini hadhi ya Washirika wa Muungano baada ya kuungana (Angalia mfano wa Katiba za Uswizi, Urusi, Marekani )
Kukosekana kwa ufafanuzi huu kumepelekea mkanganyiko mkubwa ndani ya  Katiba kuhusu mipaka ya baadhi ya mambo. Mifano michache ni kama  ifuatavyo:
a). Ibara ya 5 inayotoa haki ya kupiga kura utaofanyika Tanzania. Ibara  hii inatoa picha kuwa ibara hiyo inatumika kwa uchaguzi wowote  utaofanyika katika Jamhuri ya Muungano wakati ukweli ni kuwa Ibara hiyo  inatumika kwa uchaguzi wa Muungano tu kwa Zanzibar .
b). Ibara ya 108 inaanzisha Mahkama Kuu ya Jamhuri ya Muungano. Kwanza  hii inatafautiana na Ibara ya 4(2) ambayo inaeleza kuwepo Mahkama ya  Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Pili, Mahkama Kuu si miongoni mwa mambo  ya Muungano na hivyo hakuna Mahkama Kuu ya Jamhuri ya Muungano; zipo  Mahakama Kuu ya Zanzibar na Mahkama Kuu ya Tanzania Bara. Tatu, hili  limepelekea kuchanganywa kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Bara katika  Uongozi wa Mahaka ya Rufaa jambo ambalo ni kinyume na Katiba na ni  tofauti sana na mfumo uliokuwepo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  ambapo Mahkama ya Rufaa ya Afrika Mashariki haikuwa ya nchi yoyote bali  ya nchi zote na ilikuwa na uongozi na bajeti yake tofauti. Aidha,  mkanganyiko huu umepelekea mtafaruku katika uwakilishi wa Jamhuri ya  Tanzania katika taasisi za kimataifa na kikanda kwa mambo yasiyo ya  Muungano.
MGAWANYO WA MAMLAKA
Ibara ya 4(3) imegawa. Mamlaka tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mamlaka hizo ni kama zifuatavyo:
a). Mamlaka ya Mambo ya Muungano ambayo ni kwa Tanzania Bara na Zanzibar;
b). Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano kwa Zanzibar; na
c). Mambo yasiyo ya Muungano kwa Tanzania Bara
Mamlaka ya Mambo ya Muungano:
Kwa mujibu wa Ibara ya 4(3), Mambo ya Muungano ni yale yaliyotajwa  katika Jadweli la Kwanza, mwishoni mwa Katiba. Kwa kawaida tumezoea  kuyaita mambo hayo kuwa ni 22, lakini kwa uhakika ni haya yafuatayo:
i. Katiba ya Tanzania;
ii. Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
iii.Mambo ya nchi za Nje;
iv.Ulinzi;
v. Usalama;
vi.Polisi
vii.Hali ya Hatari;
viii.Uraia;
ix. Uhamiaji;
x. Mikopo;
xi. Biashara za Nje;
xii. Utumishi katika Serikali ya Muungano;
xiii.Kodi ya Mapato (income tax);
xiv.Ushuru wa Forodha (custom duty);
xv. Ushuru wa Bidhaa (excise duty);
xvi.Bandari;
xvii.Usafiri wa Anga;
xviii.Posta;
xix. Simu;
xx. Sarafu na Fedha;
xxi. Mabenki;
xxii.Fedha za Kigeni;
xxiii.Leseni za Viwanda;
xxiv.Takwimu za Viwanda;
xxv. Elimu ya Juu;
xxvi.Maliasili ya Mafuta;
xxvii.Mafuta yasiyochujwa;
xxviii.Gesi Asilia;
xxix. Aina Nyengine za Mafuta;
xxx. Baraza la Taifa la Mitihani;
xxxi. Usafiri wa Anga;
xxxii.Usafirishaji wa Anga;
xxxiii.Utafiti;
xxxiv.Utabiri wa Hali ya Hewa;
xxxv. Takwimu;
xxxvi.Mahkama ya Rufaani;
xxxviii.Uandikishaji na Mambo mengineyo yanayohusu Vyama vya Siasa.
Masuala Muhimu Kuhusu Mambo ya Muungano:
a. Idadi ya Mambo ya Muungano ni mangapi.
Suala hii linatokana na sababu tatu kubwa. Kwanza, kwa kuzingatia  utaratibu wa kupiga kura chini ya ibara ya 98, jee mambo yaliopo chini  ya Jadweli la Pili, Orodha ya Kwanza na ya Pili nayo ni mambo ya  Muungano. Pili, Ofisi ya Rais na Makamo wa Rais hazikutajwa katika  Orodha ya Mambo ya Muungano, jee Ofisi hizo ni za Muungano au hapana.  Tatu zipo Taasisi kama vile Tume ya Pamoja Ya Fedha hazikutajwa katika  Orodha ya Mambo ya Muungano. Nne, jee Serikali ya Muungano ambayo  imetajwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano lakini ndiyo pia  inayosimamia mambo ambayo si Muungano ni jambo kweli la Muungano. Tano,  kwa mujibu wa Uamuzi wa Mahkama ya Rufaa katika Kesi ya Mchano Khamis na  Wenzake 17, Orodha ya Mambo ya Muungano haikueleza mambo yote ya  Muungano. Kwa hivyo, ni dhahiri kuwa Orodha halisi ya Mambo ya Muungano  haijulikani.
b. Tafsiri ya Mambo ya Muungano
Si Katiba wala Sheria nyengine yoyote iliyotafsiri maana na mipaka ya  mambo ya Muungano. Kwa mfano nini tafsiri ya elimu ya juu, Bandari, Aina  nyengine za Mafuta zinajumuisha bio-fuels, Ulinzi nk.
c. Sera na Utaratibu wa Kubadili Mambo ya Muungano.
Mambo ya Muungano ndio msingi mkubwa wa Muungano. Kuongezwa au kupunguza  mambo ya Muungano kunaweza kubadili dhana nzima ya Muungano. Hivyo  kuwepo sera na utaratibu wa kubadili orodha ya Muungano ni muhimu sana.  Kwa mfano Katiba ya Marekani inakataza kabisa Majimbo mawili kuungana  kuunda Jimbo moja au Jimbo moja kugawanywa kuunda jimbo jengine, kwa  sababu ya kulinda “utaifa” wa Majimbo. Katika Katiba ya Muungano kuna  misingi gani ya Muungano ambayo.
d. Kukosekana Mfumo Rasmi wa Kila Mamlaka Kuitambua Mamlaka Nyengine
Hii ni kasoro kubwa sana katika Muungano na ambayo kwa bahati mbaya  imejificha. Miongoni mwa athari zake ni kama zifuatazo. Kwanza, ingawa  Rais wa Jamhuri ya Muungano ana mamlaka kwa mambo ya Muungano ndani ya  Tanzania Bara na Zanzibar, masuala kama vile ya Sheria za jinai si suala  la Muungano na hivyo kinga aliyonayo ya kutoshtakiwa ndani ya Katiba ya  Muungano haiwezi kutumika Zanzibar kwa vile Zanzibar ina mamlaka na  sheria zake za jinai. Suala muhimu hapa ni jee Rais wa Muungano anaweza  kushtakiwa kwa kosa la jinai ndani ya Zanzibar? Suala hili kwa hali ya  sasa linaweza kuonekana la kituko, lakini ni la muhimu sana. Pili, suala  kama hili ni muhimu kujiuliza kwa Rais wa Zanzibar anapokuwa ndani ya  Tanzania Bara. Tatu, Katiba haijaweka bayana masuala ya mashirikiano ya  kimahkama hasa katika utekelezaji wa amri za Mahkama za pande mbili.  Jambo pekee lililoelezwa ni upelekaji hati za Mahkama. Yapo mambo mengi  ambayo kwa sababu Katiba haijaweka bayana mfumo wa Mamlaka ya upande  mmoja kuitambua Mamlaka ya upande mwengine, Taifa moja limebaki kama  nchi tofauti sawa na nchi nyengine ya kigeni.
Mamlaka ya Mambo Yasiyo ya Muungano Zanzibar
Ibara ya 4(3) ya Katiba ya Muungano inaleta tafsiri kuwa mambo yote  ambayo hayakutajwa katika Jadweli la Kwanza sio mambo ya Muungano.  Ukiachia ibara hiyo hakuna kifungu chengine chchote cha Katiba wala  Sheria kinachoeleza ni yapi mambo ambayo si ya Muungano. Hivyo, mamlaka  ya mambo kwa Zanzibar inasimamia mambo yale ambayo hayakutajwa katika  Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mambo Yasiyo ya Muungano Tanzania Bara
Msingi wa mambo yasiyo ya Muungano kwa Tanzania Bara msingi wake pia ni  Ibara ya 4(3) ya Katiba. Ufafanuzi zaidi utafanywa katika Sehemu ya  Usimamizi wa mambo yasiyo ya Muungano.
SERIKALI MBILI NA MUUNDO WAKE
Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) ina  dhamana ya kusimamia mambo ya Muungano na Mambo Yasiyo ya Muungano kwa  Tanzania Bara, inaongozwa na Rais akisaidiwa na Makamo wa Rais! Waziri  Mkuu na Mawaziri.
Kwa mujibu wa Ibara ya …. Rais huchaguliwa kwa wingi wa kura. Makamo wa  Rais huchaguliwa kwa mtindo wa mgombea mwenza kwa fomula ya kuwa kama  Rais atatoka Tanzania Bara, Makamo wa Rais atatoka Zanzibar na kinyume  chake pia.
Waziri Mkuu, kwa mujibu wa Ibara ya 51(2), huteuliwa na Rais. Hakuna  sharti la kikatiba wala kisheria linalomtaka Rais kushauriana na Makamo  wa Rais katika uteuzi wa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Ibara ya 55(1) Ya Katiba, Mawaziri huteuliwa na Rais kwa  kushauriana na WAZIRI MKUU sio MAKAMU WA RAIS. Rais wa Zanzibar ni  Mjumbe wa Baraza la Mawaziri kwa wadhifa wake.
Hakuna ibara ya Katiba au kifungu cha Sheria kinacholazimisha Wizara za  Serikali ya Muungano kuundwa kwa kuzingatia Wizara zinazosimamia mambo  ya Muungano kutochanganywa na Wizara ambazo hazisimamii mambo ya  Muungano.
Masuali Muhimu
a. Uhalali (legitimacy) wa Rais wa Muungano kuchaguliwa kwa wingi wa kura kwa kuzingatia tofauti ya idadi ya watu baina ya Zanzibar na Tanzania Bara;
b. Uhalali wa Rais wa Zanzibar kuwa Mjumbe tu wa Baraza la Mawaziri  na sio Mwakilishi wa Zanzibar ndani ya Baraza la Mawaziri ili kuepuka  kubanwa na Kanuni ya Baraza la Mawaziri ya Uwajibikaji wa pamoja
c. Nini wajibu wa kikatiba wa Makamo wa Rais katika uendeshaji wa Serikali;
d. Makamo wa Rais ni Msaidizi Mkuu wa Rais wa Muungano kuhusiana na  Zanzibar kama ilivyokusudiwa na Mapatano ya Muungano? Jee ni Msaidizi  Mkuu wa Rais wa Muungano kwa Mambo ya Muungano au Msaidizi Mkuu ni  Waziri Mkuu?
e. Jee Mawaziri wanaotoka Zanzibar waliomo katika Baraza la Mawaziri la  Serikali ya Muungano wanaiwakilisha Zanzibar au ni watumishi wa Rais wa  Muungano kama walivyo Mawaziri wengine?
f. Jee kuna chombo chochote cha Kikatiba au kisheria kinacholazimisha  Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano kukutana, kushauriana na kufanya  maamuzi ya pamoja kama Mamlaka mbili za kuendesha Jamhuri ya Muungano?
g. Katika mfumo wa sasa wa Serikali mbili upo uwezekano wa Serikali  mbili zinazoongozwa na vyama viwili tofauti kufanya kazi kwa maelewano;
h. Jee kipo chombo cha kutatua mizozo inayoweza kujitokeza baina ya Serikali mbili?
USIMAMIZI NA UENDESHAJI WA MAMLAKA TATU ZA JAMHURI YA MUUNGANO
a. Usimamizi na Uendeshaji wa Mambo ya Muungano
Katika kila eneo ni vyema tuangalie Usimamizi na Uendeshaji katika nyanja tatu;
Sera
Sera ndio dira ya maamuzi na utekelezaji wa jambo lolote la umma. Sera  za Mambo ya Muungano zinaanzishwa na Wizara husika. Kwa mfano Sera ya  Mambo ya Nje bila ya shaka itaanzishwa na Wizara ya Mambo ya Nje. Baada  ya taratibu za ndani uamuzi wa mwisho hutolewa na Baraza la Mawaziri.  Hakuna sharti la kikatiba wala la kisheria linaloitaka Serikali ya  Muungano kushauriana na kukubaliana na Serikali ya Zanzibar katika  kuandaa na kupitisha Sera za Mambo ya Muungano.
Utaratibu unaotumika kwa mazoea tu na kwa baadhi ya wakati ni rasimu za  Sera kutumwa na Wizara husika kwa Wizara husika ya Zanzibar ili kupata  maoni ya Zanzibar. Uzoefu wa siku nyingi unaonyesha Maoni hayo ya  Zanzibar si mara nyingi kuzingatiwa. Mfano mzuri ni Sera ya Mambo ya Nje  ambapo Baraza la Mapinduzi liliunda Kamati ya BLM kuandaa mapendekezo  ya Zanzibar ambayo hatimaye yalipitishwa na BLM lakini hayakuzingatiwa.
Sheria
Kwa mujibu wa Ibara ya 64 mamlaka ya kutunga Sheria kwa Mambo ya Muungano ni ya Bunge.
Kwa mujibu wa Ibara ya 98, Bunge linapotunga Sheria linahitaji ridhaa ya  Wabunge kutoka Zanzibar kwa Mambo yaliyomo katika Orodha ya Pili ya  Jadweli la Pili. Mambo hayo ambayo ni 8 si sehemu ya Mambo ya Muungano  ingawa baadhi yake ni mambo muhimu sana.
Kutokana na masharti hayo ya Katiba ni wazi kuwa Sheria zote za Mambo  yote ya Muungano ambayo yameorodheshwa katika Jadweli la Kwanza (Mambo  37), Sheria zake zinapitishwa kwa utaratibu wa wingi wa kura. Kwa mfano,  Sheria ya Uhamiaji, Sheria ya Uraia, Sheria ya Kuanzishwa kwa TRA,  Sheria za kodi na Sheria zote za Muungano zinapitishwa Bungeni kwa wingi  wa kura tu. Kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya Wabunge wa Zanzibar na  Tanzania Bara, ni wazi kuwa Sheria za Mambo yote ya Muungano zinaamuliwa  na upande mmoja tu wa Muungano.
Fedha na Bajeti
Ibara ya 133 ya Katiba ya Muungano inaanzisha Akaunti Maalumu ya Pamoja  (Joint Finance Account). Ibara hiyo inaeleza wazi kwamba katika Akaunti  hiyo, kutawekwa Mapato yote ya Muungano na Matumizi yote ya Muungano  yatatoka katika Akaunti hiyo.
Ingawa Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha ilipitishwa mwaka 1996, Tume  ilianza kazi mwaka 2003 na kutoa Ripoti ya Mapendekezo ya kuanzisha  Akaunti ya Fedha ya Pamoja na mfumo wa mgawanyo wa gharama na mapato ya  Muungano mwaka 2006, bado Akaunti ya Pamoja haijaanzishwa. Suala kubwa  hapa ni uhalali wa Bajeti ya Serikali ya Muungano kwa vile inakwenda  kinyume na masharti ya Katiba ya Muungano.
Aidha, athari ya kutoanzishwa Akaunti ya Pamoja ni kama zifuatazo:
i) Mipaka ya Mambo ya Muungano haijulikani; kwa mfano, ingawa Bunge ni  chombo kinachofanya kazi za Muungano lakini linafanya kazi kwa mambo  yasiyo ya Muungano hivyo inahitajika kuweka uchambuzi wa kiasi gani ya  gharama za Bunge zitoke katika Mapato ya Muungano na kiasi gani yatoke  katika mapato yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara;
ii) Mapato ya Muungano hayawekwi bayana;
iii) Gharama za kuendesha shughuli za Muungano haziko bayana;
iv) Gharama za Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara hayako bayana.  Aidha, haiku bayana ni kiasi gani cha mapato ya Muungano kinatumika  kuendesha shughuli zisizo za Muungano kwa Tanzania Bara;
v) Stahiki au deni la kila upande kutokana na mapato na gharama za kuendesha shughuli za Muungano hazijaweza kuwekwa bayana.
Kwa madhumuni ya kujenga msingi mzuri wa Mjadala katika Mada hii  sitazungumzia Uendeshaji na Usimamizi wa Mambo Yasiyo ya Muungano.  Maelezo ya hapo juu yanatosha kueleza sehemu iliyobaki kuhusiana na  Mambo yasiyo ya Muungano.
Utawala wa Mambo ya Muungano
Utawala wa mambo ya pamoja katika Muungano wowote ni jambo la msingi  katika kuamua uimara wa Muungano huo. Utawala wa mambo ya Muungano una  sehemu mbili. Kwanza ni kuhusu ushiriki wa kila upande katika uongozi na  ajira za mambo ya Muungano na pili ni pahala ambapo Ofisi za mamlaka  husika ya jambo la Muungano yapo. Mambo hayo mawili ni muhimu sana kwa  vile inasaidia kuleta sura ya Muungano, ujuzi kwa kila upande katika  masuala ya Muungano na pia kupata faida ya uwekezaji wa Serikali ambayo  ni ajira kwa raia.
Katika mfumo wa Muungano wa Tanzania hakuna sharti la kikatiba, la  kisheria au sharti rasmi la kisera la Utawala wa Mambo ya Muungano.
Athari ya hali hii ni kuwa uongozi, ajira na uwekezaji katika Ofisi za mamlaka za Muungano zimekuwa upande mmoja wa Muungano.
Miongoni mwa mifano hiyo ni pamoja na:
i) Makao Makuu ya Wizara zote;
ii) Makao Makuu ya Benki Kuu;
iii) Taasisi ya Kodi (TRA);
iv) Mamlaka ya Usafiri wa Anga;
v) Mamalaka ya Mawasiliano;
vi) Tume ya Pamoja ya Fedha;
vii) Uhamiaji;
viii) Tume ya Vyuo Vikuu;
ix) Mahkama ya Rufaa; na
x) Msajili wa Vyama vya Siasa
UTATUZI WA MIGOGORO
Chombo pekee kilichowekwa kutatua migogoro baina ya Serikali Mbili za  Jamhuri ya Muungano ni Mahkama ya Katiba iliyoanzishwa chini ya Ibara ya  125 ambayo taratibu zake zimeelezwa chini ya Ibara ya 126, 127 na 128.  Mahkama hii kama chombo cha kutatua migogoro baina ya pande mbili ina  kasoro kadhaa. Miongoni mwa kasoro hizo ni:
i) Ina mamlaka kuhusiana na mgogoro unaohusu tafsiri ya Katiba ya Muungano tu;
ii) Ni lazima ianzishwe kwa makubaliano ya pande zote mbili; kwa vile Majaji wake wanateuliwa kwa idadi sawa na Serikali mbili;
iii) Uamuzi ni kwa wingi wa kura;
iv) Inaundwa endapo patakuwa na shauri la mgogoro tu na si vyenginevyo.
HITIMISHO
Katiba ya Muungano ina maeneo mengi yanayohitaji kuangaliwa kwa makini.  Hata hivyo maeneo yaliyofafanuliwa katika Makala hii ni miongoni mwa  maeneo muhimu ambayo yanagusa nyanja takriban zote muhimu za Muungano.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ZANZIBAR: OTHMAN MASOUD OTHMAN