Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na  Mabalozi wa Heshima wa Tanzania katika baadhi ya Majimbo ya Marekani  Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kulia yake ni Balozi wa Tanzania Washington D.C Bibi Mwanaidi Sinare,  Bwana Kjell Berg Minessota na Bwana  Ahmed Issa Alqassim San Francisco. Kushoto ya Balozi ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Dr. Khalid Slum Moh’d, Naibu wake Nd. Said Shaaban pamoja na  Bwana Saleh ambae ni Msaidi wa Balozi Jimbo la Washington. 
   Makamu wa Pili wa Rais wa Znzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa zawadi kwa  mmoja wa Wafanyabiashara Waandamizi waliounda Kundi la VIP Safari  kutoka Nchini Marekani ambao wapo Nchini kuangalia uwezekano wa namna ya  Kampuni zao kuwekeza Vitega Uchumi Nchini Tanzania.   
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Alio Iddi akiwa katika  picha ya pamoja na Ujumbe wa wa Wafanyabiashara waandamizi wa Kundi la  VIP Safari baada ya kuwaandalia chakula cha usiku hapo Serena Inn Hoteli  Shangani Mjini Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Balozi wa Tanzania Washington D.C Bibi Mwanaidi  Sinare na Balozi wa Heshima MjiniMinessota Bw. Kjell Berg. Kushoto yake ni Waziri wa Hbari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said  Ali Mbarouk, Mke wa Balozi Seif Mama Asha Suleimana Iddi pamoja na Mmoja  wa Wafanyabiashara hao wa VIP Safari.Picha na Saleh Masoud
  ---
   Na Othman Khamis Ame
   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema  Mazingira ya Kimaumbile yaliyoizunguuka Zanzibar bado yana fursa nzuri  ya kutumiwa katika shughuli za Uwekezaji Vitega Uchumi. 
   Balozi Seif alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Mabalozi wawili wa  Heshima wa Tanzania katika majimbo mawili ya Marekani ya Minessota na  San Francisco hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 
   Mabalozi hao Bwana Ahmed Issa Qassim atakayeiwakilisha Tanzania katika  Jimbo la San Francisco na Bwana Kjell Berg wa Jimbo la Minessota  waliongozwa na Balozi wa Tanzania Mjini Washington D.C  Balozi  Mwanaidi  Sinare Maajar. 
   Balozi Seif alisema katika kuyatumia vyema mazingira hayo Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar inajaribu kuongeza nguvu za uimarishaji wa miundo  mbinu katika Sekta ya Utalii. 
   Alisema licha ya Sekta ya kilimo kuchukuwa nafasi kubwa ya Uchumi wa  Taifa lakini eneo la utalii pia lina fursa nzuri ya kuwa muhimili wa  Pili wa Uchumi wa Zanzibar kwa hivi sasa. 
   Balozi Seif alifahamisha kwamba serikali inaangalia pia uwekezaji wa  maeneo ya Kumbi za Mikutano ya Kiutalii kutokana na kupanuka zaidi kwa  sekta hiyo hivi sasa. 
   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaomba Mabalozi hao wa  Heshima wa Tanzania katika Majimbo ya Marekani kuwa wawakilishi wazuri  wa kuitangaza Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kwa wawekezaji kwenye  majimbo watakayoyafanyia kazi. 
   Balozi Serif aliwaahidi wawakilishi hao kwamba Serikali zote mbili  zitajitahidi kutoa msaada kwao kwa vile kazi watakazokwenda kuzifanya ni  kwa ajili ya Watanzania. 
   Mapema Balozi wa Tanzania Mjini Washington D.C Bibi Mwanaidi Sinare  Maajar alisema Zanzibar bado ina Utajiri wa Kihistoria  ambao Wamarekani  walio wengi wanaendelea kuushangaa. 
   Balozi Mwanaidi alisema utafiti unaonyesha kwamba soko zuri liliopo la  Utalii kati ya Marekani na Tanzania linafaa kutumiwa vyema kwa kuweka  mazingira yatakayostawisha pande zote mbili. 
   Alisema yapo Makampuni kadhaa ambayo tayari yameshaonyesha nia ya kutaka  kuitumia fursa hii ya uwekezaji katika Sekta ya Utalii baada ya  kutembelea na kuona maeneo mbali mbali Bara na Hapa Zanzibar. 
   Nao kwa upande wao Mabalozi hao wa Heshima wa Tanzania Bwama Ahmed Issa  Alqassim wa San Francisco na Bwana  Kjell Berg wa  Minessota wameahidi  kutekeleza vyema majukumu yao waliokabidhiwa na Taifa. 
   Mabalozi hao wameishauri Serikali na Jamii kuhakikisha ule Utalii wa  Kiutamaduni { Culture Tourism } ulioanzishwa na Vizazi vilivyopita  unafaa kulindwa na kuenziwa. Walisema Utalii huu ambao zaidi umejikita katika eneo la Kivazi cha  asili umekuwa maarufu  na kufikia hatua ya kuigwa na watu maarufu katika  sehemu mbali mbali Duniani. 
   Wakati wa usiku Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  alijumuika pamoja na Wafanyabiashara Waandamizi waliounda kundi la VIP  Safari kutoka Nchini Marekani katika chakula cha Usiku. 
   Tafrija hiyo iliyoshirikisha pia Baadhi ya Mawaziri pamoja na Watendaji  wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar ilifanyika katika Hoteli ya Serena Inn  iliyopo Shangani Mjini Zanzibar. 
   Akizungumza na Wafanyabiashara hao Balozi Seif alisisitiza kwamba  mchango wa Wafanyabiashara hao unaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa  sekta binafsi katika uimarishaji wa Uchumi wa Zanzibar. 
   Balozi Seif alisema Serikali hivi sasa imelenga kuimarisha Sekta hiyo  kwa kuongeza miundo mbinu itakayowezesha kundi kubwa la Vijana wasio  kuwa na kipato kupata ajira.
    Mapema akitoa shukrani zake Waziri wa Habari, Utamaduni,Utalii na  Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema Marekani hivi sasa imekuwa Mshirika  mkubwa wa Zanzibar katika Masuala ya Biashara na Uwekezaji. 
   Hivyo aliwaomba Wafanyabiashara hao kupitia ofisi za Kibalozi za  Tanzania zilizomo ndani ya Majimbo tofauti ya Nchi hiyo kuendelea  kuitangaza Zanzibar kwa Wawekezaji wa Majimbo yao.
  Na
    Othman Khamis Ame 
  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar