Pages

Thursday, July 5, 2012

MZEE SABODO ACHANGIA CHADEMA NA KUTOA AHADI ZINGINE ZA MIRADI





MFANYABIASHARA maarufu na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustafa Jaffer Sabodo
amekichangia tena Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), sh.
milioni 10, huku akitoa ahadi nyingine mpya ya kukipatia chama hicho
mradi wa kukiingizia mapato na kuchimba visima kwa majimbo ya chama
hicho kwa miaka 10.

Amesema kuwa kazi inayofanywa na chama hicho kutoa elimu ya uraia hadi
vijijini, huku kikizidi kuimarisha mtandao wake kwenye ngazi za
vitongoji na mitaa kikidhamiria kuendelea kupigania na kutetea haki za
wananchi, inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania mpenda maendeleo.

Mfanyabiashara huyo ambaye amekuwa akijitokeza waziwazi bila uoga kukichangia chama
hicho cha upinzani, akisema anafurahishwa na kazi ambayo kinafanya ya
kutetea maslahi na rasilimali za Watanzania kutengeneza fursa za
maendeleo, ameongeza kuwa amefurahishwa na Operesheni Okoa Kusini,
ambayo chama hicho kilifanya karibuni mikoa ya Lindi na Mtwara.

Akizungumza jana nyumbani kwake ambako alikutana na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt.
Willibrod Slaa kwa ajili ya kuzungumzia mchakato wa utekelezaji wa ahadi
alizotoa kwa chama hicho, Mzee Sabodo aliahidi kuwa baada ya kukamilika
kwa jengo la kuegesha magari linalojengwa katikati ya Jiji la Dar es
Salaam, sehemu ya mapato yatatumika kuchimba visima kwa miaka 10.

Mbali ya sehemu ya mapato kutoka katika jengo hilo la kuegesha magari ambalo
linajengwa na Taasisi ya Khoja Shia Ithnasheri Jamaat (KSIJAMAAT), pia
Mzee Sabodo alisema kuwa sehemu ya chini ya jengo hilo ambayo itakuwa na
maduka, CHADEMA itapatiwa duka moja kama mmoja wa miradi ya kukipatia
mapato.

“Mtapata sehemu ya mapato ili kuchimba visima kwenye majimbo yenu kwa miaka
kumi…pia mtapata duka pale ili mpate mradi wa mapato. Ili kuharakisha
utekelezaji wa ahadi ya visima vile vingine fanyeni survey ninyi wenyewe
na mpate mkandarasi, itakuwa sehemu ya gharama ya uchimbaji…hizi
milioni 10 mtapata hundi hapa mkafanye kazi za wananchi,” alisema Mzee
Sabodo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Slaa, mbali ya kumshukuru na
kumpongeza Mzee Sabodo kwa ujasiri wake wa kuendelea kujitoa kusaidia
harakati za kupigania haki za wananchi, mabadiliko ya kiutawala na
kimfumo nchini, aliahidi kuwa chama hicho kitaendelea kutimiza wajibu
wake kwa maslahi ya Watanzania.

“Umekuwa mtu wa msaada mkubwa kwetu, umeendelea kuwatia moyo Watanzania wote wa
kila namna kuacha uoga wa kuchangia harakati hizi, kwani lengo letu ni
kuwatumikia Watanzania katika kila fursa tunayoipata, ambapo kwa sasa
tutaendelea kuisimamia na kuiwajibisha serikali ya CCM ambayo ni dhahiri
ielekea mwisho na wananchi wameichoka.

“Nasi tunawaahidi Watanzania wote kuwa tutaendelea kuwatumikia na
hatutawaangusha, tunatambua kuwa katika mparanganyiko huu mkubwa, kama
ugumu wa maisha, hali mbaya ya uchumi, siasa zinazoyumba, ufisadi na
ubadhirifu wa mali za umma na migogoro katika makundi mbalimbali ya
kijamii kwa sababu ya uongozi mbovu, CHADEMA linabaki kuwa ndiyo tumaini
pekee kwa Watanzania,” alisema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa aliyeambatana na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa CHADEMA, Antony
Komu, aliongeza kuwa visima vya ahadi hii mpya kutokana na mapato ya
jengo la maegesho ambayo ni tofauti na ahadi za visima vingine alizowahi
kutoa mwaka jana na mapema mwaka huu, vitachimbwa katika maeneo
mbalimbali ya Tanzania yenye kero kubwa za maji.

Mbali ya ahadi hizo mpya za jana, Mzee Sabodo na Dkt. Slaa walizungumzia juu
ya mchakato wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali zingine za mfanyabiashara
huyo na kada wa CCM, ambazo amekuwa akitoa kwa CHADEMA mara kadhaa
tangu mwaka 2010, zikiwemo za ujenzi wa chuo, uchimbaji wa visima, ofisi
za makao makuu ya chama hicho na baiskeli 100 za walemavu.

Popular Posts