Pages

Friday, July 6, 2012

MUWAZA yaipongeza JUMIKI

Kwa Uongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu( JUMIKI)
S.L.P 1266
Mkunazini-Zanzibar
E-Mail: jumiki@hotmail.com

Assalama Aleikum,

Kuhusu:
Mkakati

Kwa niaba ya Wanachama wa Jumuiya ya Mustakbal wa Zanzibar (MUWAZA),
Muungano wa Wazanzibari ng’ambo, tunaipongeza Jumuiya ya JUMIKI
kwa uamuzi wa kijasiri na kishujaa wa Viongozi wake kushiriki pamoja na
Wazanzibari wenziwao wote katika mchakato wa kutafuta katiba mpya ya
Tanzania na kukataa katakata suala zima la kususia zoezi hilo. MUWAZA
inakubaliana kwamba ususiaji wa namna yeyote wa zoezi hilo utatoa mwanya
unaotakiwa na Watu wasioitakia mema Zanzibar, na ambao wanaweza
kuutumia mwanya huo kujifanya wao ndio wasemaji pekee halali wa
Wazanzibari. Ni kushiriki kwa wingi na kikamilifu katika kutoa maoni mbele ya
tume hiyo ya Jaji Warioba ndipo wananchi wa Zanzibar wataweza kudhihirisha
hadharani chaguo gani wanalitaka kuhusu mustakbali wa maisha yao ya
baadae ndani ya Zanzibar. Hii ni fursa nzuri na ya nadra ambapo Wazanzibari
wataweza kurejesha heshima ya nchi yao na ya Viongozi wao.

Hata hivyo, MUWAZA inawashauri Viongozi wa JUMIKI, kama inavowashauri
ndugu zetu Wazanzibari, kwamba fursa hii ya mchakato wa katiba
mpya itumike kwa amani na ustaarabu wa kizanzibari unaothaminiwa duniani
kote wa kustahamilia kila mmoja wetu maoni ya mwenzake, hata kama
hakubaliani nayo, kikubwa kabisa ni kuweka maslahi ya juu kabisa ya visiwa
vya Zanzibar na wengi wa watu wake.

MUWAZA, kama ilivyo JUMIKI, pamoja na Wazanzibari wote wanaopenda
amani na maendeleo ya visiwa vyao, kwa nguvu zote unapinga kabisa
matumizi ya nguvu na mabavu dhidi ya wananchi, bila ya kujali kama vitendo
hivyo vinafanywa na taasisi za dola, vyama vya kisiasa, jumuiya yeyote au
mtu mmoja mmoja binafsi. Tunasisitiza haja ya vyombo vya dola, Vyama
vya kisiasa, Jumuiya za kiraia na Wananchi kwa jumla kutetea na kuheshimu
amani ya nchi, uhuru wa watu wote kuweza kutoa maoni yao na kukusanyika
kwa njia huru, bila ya vizuwizi na vikwazo, mradi wanaambatana na sheria na
kulinda amani.

MUWAZA inaamini zoezi la kuwaelimisha Wananchi juu ya haki zao za
kikatiba na kuwazindua juu ya sheria ambazo hazitekelezwi vilivyo kama
ilivokusudiwa, hivyo kupelekea wananchi kukandamizwa na kupoteza haki
zao za kimsingi, ni harakati endelevu isiokuwa na kiwango cha wakati
na kipindi. Hivyo, tunakubali kwamba ni juu ya dola kuweka mazingira
mazuri kwa jambo hilo kufanyika. Ni imani ya MUWAZA kwamba wananchi
wanapozidi kuwa na mwamko zaidi wa kutambua haki zao na kuelewa
namna ya kuzipigania kwa njia ya amani, pamoja na kuelewa namna nchi yao
inavotawaliwa na inavofaa kutawaliwa siku za mbele ni faida kwa nchi yetu na
maendeleo yake.

MUWAZA inakubaliana nanyi kwamba kuna mambo kadha ya dhuluma ndani
ya Muungano, kama ulivo sasa, kwamba Muungano huo umekuwa zaidi
wa kiserikali. Hivyo iko haja ya kuuimarisha zaidi Muungano wa Kijamii na
kuondosha dhuluma zilizokuweko mnamo miaka 48 iliopita.

Kama ilivyo JUMIKI, MUWAZA imelikaribisha kwa tamko la Mheshimiwa
Jaji Warioba alilolitoa mbele ya Waandishi wa habari alipoizindua Tume ya
kukusanya maoni juu ya katiba mpya mjini Dar es Salaam tarehe 18/06/
2012 kwamba maoni yote yataheshimiwa na kuzingatiwa, likiwemo suala la
Muungano ambalo kwa Wazanzibari ndilo suala muhimu.

Pia MUWAZA inatarajia, kutokana na watu waliomo ndani ya Tume ya
Jaji Warioba, kwamba uadilifu, haki na uwazi utaoneshwa katika zoezi
la kukusanya maoni ya Wananchi, maoni ya wananchi walio wengi
yataheshimiwa na tume na baadae na Serikali ya Muungano wa Tanzania
na ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.Tunaitarajia Tume ya Warioba na
Serikali zote mbili zitahakikisha watu wanatoa maoni yao bila ya kutishwa
waseme nini mbele ya Tume, kwamba hawataadhibiwa kwa namna yeyote
juu ya usalama na ajira zao baada ya kutoa maoni yao mbele ya tume.
Tunawahimiza Wazanzibari waseme wazi, tena kwa midomo mipana, pindi
wanatiwa hofu ya aina yeyote wakati wa zoezi hilo.

Kama ilivyo JUMIKA, MUWAZA inatoa mwito kwa Wazanzibari wote waungane
kwa kauli moja ya kurejesha heshima ya rais wa Zanzibar na nchi yao, na
kwamba chimbuko la mamlaka maisha libakie ndani ya mikono ya wananchi.

MUWAZA inapinga vikali vitendo vyovyote vya kuwabeza Wazanzibari
wanaopinga mfumo ulioibakisha nchi yao nyuma kwa miaka na kuwabakisha
wananchi wake wengi katika ufukara na maendeleo duni katika nyanja za
elimu, afya na huduma nyingine za kijamii.

Tunawatakia Wazanzibari kila la kheri, amani na maendeleo, na hayo
yatafikiwa tu ikiwa wenyewe Wazanzibari, katika mazingira yalio huru na ya
amani, watafanya maamuzi sahihi kwa pamoja katika kipindi hiki muhimu cha
historia ya nchi yao.

Iiishi Zanzibar.

Mwenyekiti
Jumuiya ya MUWAZA

Popular Posts