Pages

Thursday, July 5, 2012

TAMKO LA KANISA KATOLIKI TANZANIA KWA WAUMINI WOTE

UJUMBE WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA KWA WAAMINI WAKATOLIKI NA WATU WOTE WENYE MAPENZI MEMA
30-06-2012

SISI Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tumekutana katika mkutano wetu Mkuu wa 65 wa kawaida tangu tarehe 23/06/2012 hadi 30/06/2012 Uliowajumuisha Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na wakuu wa Idara ,Tume na Taasisi za Baraza Pamoja na Wawakilishi Walei.

Lengo la Mkutano huu likiwa kutathimini shughuli za kazi zetu za Kichungaji na za huduma za Jamii kwa Kipindi cha miaka Mitatu iliyopita 2009-2012 na vilevile kupanga mikakati ya kuboresha shughuli hizo za Kichungaji na za Huduma za Jamii katika Nyanja za Afya, Elimu, Misaada kwa wasiojiweza utetezi na ushawishi kwa kipindi cha miaka Mitatu ijayo 2012-2015.

Pamoja na kufanya tathimini ya kina ya utendaji wa Baraza letu katika kipindi hicho kilichopita. Na kupanga mipango kabambe kwa ajili ya utendaji wa Baraza kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo Mkutano wetu Mkuu umekuwa na Fursa ya kujadiliana na kushirikishana baadhi ya matukio/mambo ambayo kwa hakika yametikisa jamii yetu ya Watanzania na kuidhalilisha nchi mbele ya Jumuiya ya Kimataifa.

Kwa namna ya pekee kabisa tumetafakari juu ya vurugu za kidini hivi karibuni zilizotokea Visiwa vya Zanzibar kuanzia tarehe 26-28 Mei 2012 na kupelekea kuchomwa moto kwa baadhi ya Makanisa Visiwani humo pamoja na uharibifu wa mali na uvunjifu wa amani.

Bila kupenda kurudia matamko ya wadau mbalimbali wakiyatoa katika nyakati tofauti kulaani bila kusita hali hiyo iliyojitokeza Visiwani Humo ,Tunaunga mkono kwa nguvu zote kauli na jitihada za wale wote wenye mapenzi mema walioguswa na vitendo hivyo na hivyo kulaani.Tunatoa pole na kueleza mshikamano wetu wa kindugu kwa wale wote walioathirika kwa namna moja au nyingine kwa vitendo hivyo vya vurugu ambavyo vimefanya sehemu ya jamii ya wakazi wa visiwani humo hasa Wakristo kuhishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na vitisho vinavyoendelea kutolewa na baadhi ya vikundi pamoja na hali ya kutopewa ulinzi wa kutosha na vyombo husika.Tunaendelea kuwaahidi sala na mshikamano wetu katika kipindi hiki kigumu.

Pamoja na hayo tunapenda kuwakumbusha Watanzania wenzetu hasa wa Mamlaka husika kutafakari na kuzingatia busara za Wahenga waliosema kwamba mwanzo wa makubwa ni madogo na kwamba mdharau mwiba mguu huota tende kumbukumbu zinatuambia kwamba chuki za wazi za kidini zilianza kuinyemelea nchi tangu miaka ya 1990 pale mihadhara ya kashfa ya kidini ilipoanza kuruhusiwa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kuongozwa na busara ya kichungaji kwa nyakati tofauti liliandika barua kuziomba na kuzihimiza Mamlaka husika kuingilia kati na kuhakikisha kwamba mihadhara kama hiyo haipati nafasi kuendelea katika nchi yetu kwani kamwe haiwezi kuwa na tija ispokuwa kuamsha hisia kali za kidini, jazba na kujenga chuki miongoni mwa waamini wa dini tofauti, kwa bahati mbaya ushauri huo wa Braza la Maaskofu ulipuuzwa na Mamlaka husika .

Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la vyombo vya Habari ambavyo vimeanzishwa na ambavyo badala ya kuzingia malengo mazuri ya vyombo vya Habari kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha vimeonyesha malengo ya wazi ya kueneza uzushi, kashfa, chuki na uchochezi. Bado kuna CD, DVD na kanda chungu nzima zinazagaa mitaani zenye mambo kama hayo ambapo kwa mshangao mkubwa wa raia wema licha ya wahusika kufahamika na kuonekana waziwazi hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi yao.

Tunachelea hata kudhani kwamba Mamlaka za Dola zinawakingia kifua wadau wa harakati hizo. Mkusanyiko wa mambo yote haya ndiyo uliotufikisha hapa tulipo. Kwa upendo tulionao kwa nchi yetu na kwa kuzingatia historia ya mlolongo wa matukio yaliyotufikisha hapa tulipo, tuna hofu,l akini kwa uwazi tunapenda kuwaambia mamlaka husika watu wote wenye mapenzi mema na Watanzania wote kwa ujumla kwamba, iwapo hatua mathubuti hazitachukuliwa mara moja ili kurekebisha hali hii baada ya miaka michache, hakika kwamba nchi yetu inaweza kuingia katika machafuko ya kidini.

Ili kuepuka hali hii isitokee kwa moyo wa unyenyekevu kabisa, tunapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe: Sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tutaendelea kusali kuiombea nchi yetu Amani licha ya Sala na maombi ya kawaida kwa ajili ya lengo hilo, Mkutano Mkuu umeamua kwamba tutakuwa na siku moja ya kusali kitaifa ya kuomba Amani, Tutaendelea kutumia sauti yetu ya kinabii kuonya kukemea kukaripia vitendo vyote vile vinavyoashiria kueneza chuki miongoni mwa watu wa dini mbalimbali kwa kutumia tume na Idara zetu.

Tutaendelea kujenga na kueneza mazungumzo na waamini wa dini mbalimbali tukiheshimu tofauti zilizopo hii ni kwa sababu tunaaamini kwamba suala la dini ni wito na hiari ya mtu na hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kumlazimisha mwingine ajiunge na dini nyingine. Kwa upande wa wadau wengine na hasa kwa Serikali yetu pamoja na vyombo vyake vya usalama tunapendekeza yafuatayo:

Mihadhara, Makongamano na Mikutano yenye lengo la kutoa kashfa na kuchochea chuki miongoni mwa dini mbalimbali ipigwe marufuku, vyombo vya habari vinavyoeneza uzushi, kashfa na uchochezi vizibitiwe kwa kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa, uzushi na uongo unaoenezwa na vyombo vya habari na watu wenye lengo la kuwachonganisha Watanzania na waamini wa dini mbalimbali utolewe ufafanuzi mara moja na Wizara na vyombo vingine vinavyohusika, kuweko mpango kabambe wa kutoa Elimu ya Uraia yenye kina na upana katika nafasi zote itakayowawezesha vijana wetu kuwa wazalendo wa nchi yao na kuepuka propaganda za kuwagawa Watanzania kwa misingi ya Dini.

Suala la ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana liangaliwe kwa umakini kwani linaweza kuwa moja ya sababu zinazowafanya vijana wengi kujiingiza katika vikundi vya kidini vinavyojenga chuki na kutoa matumaini ya uongo lakini zaidi ya yote iwapo Serikali yetu na Mamllaka husika inataka kuwa na imani mbele ya jamii kwamba ina nia thabiti ya kuhakikisha kwamba vurugu za kidini hazipati nafasi katika nchi yetu wale wote waliohusika na vurugu hizo wachukuliwe hatua za kisheria mara moja! Ni vigumu kuamini kwamba katika kipindi cha kuanzi mwaka 2001 mpaka sasa Makanisa Ishirini na Tano yamekwisha kuchomwa moto kisiwani Zanzibar lakini hakuna aliyekamtwa na kuchukuliwa hatua za kisheria!

Tumefanya mkutano wetu katika mazingira ya kuwepo mvutano kati ya Madakitari na Serikali na kwa bahati mbaya sana, kama tulivyokwisha kutamka huko nyuma mvutano huo utaleta athari kubwa kwa Raia wasio na hatia, athari ambazo haziwezi kurudishwa. Uhai wa raia wa Tanzania unaaangamia kwa kukosa ulinzi wa tiba katika hali hii tunapenda kukumbusha kuwa kila mmoja ni mdau. Hakuna hata mmoja anayeweza kulikwepa hili tunapenda kurudia himizo letu la awali kwamba ipatikane njia nyingine iliyomwafaka zaidi ya kudai haki na mazingira yanayofaa ya kazi bila ya kuleta madhara ya kupoteza uhai ambayo ni haki ya msingi ya kila mwanadamu.

Tunaisii Serikali yetu ikae tena na Madaktari na kuchambua hoja zitakazowekwa mbele yao. Uwazi na ukweli vikitawala hakuna pande itakayokataa kuridhia eti kwa sababu ya kukataa tu bila hoja. Taifa letu limejipatia aibu mbele ya macho ya Ulimwengu ya jinsi tunavyoshindwa kuhishi kile tunachosema katika majukwaa.

Mwisho tunaendelea kuwaalika Watanzania wenzetu hasa viongozi wa Dini mbalimbali kuwahamasisha waamini wawe raia wema wa nchi hii kwa kuungana pamoja kuhamasisha upendo, haki, amani na maridhiano miongoni mwa Watanzania wote.

Licha ya tofauti zetu tuzingatie hasa yale yanayotuunganisha, ubinadamu wetu na uraia wetu wa nchi yetu tukufu ya Tanzania ambamo tutake tusitake ni lazima wote tuhishi tuepuke ushindani ambao hauna tija isipokuwa kutupeleka katika chuki na hali ya kuzaniana vibaya miongoni mwa waamini wetu. Iwapo kuna sababu ya kushindana, tushindane katika mbinu za kujenga upendo na amani miongoni mwa Watanzania katika kutafuata njia za kuwaletea maendeleo yatakayowatoa katika umaskini, ujinga na maradhi ambavyo ni adui wetu sote. Tunaiombea nchi yetu amani na usalama.

MWISHO

Popular Posts