TAMKO LA SERIKALI KUHUSU MALALAMIKO DHIDI YA MATOKEO YA SOMO LA ISLAMIC KNOWLEDGE KATIKA MTIHANI WA KIDATO CHA SITA 2012
1.0 UTANGULIZI
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha sita 2012 yaliyotangazwa rasmi tarehe  01/05/2012. Tarehe 28/5/2012 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  ilipokea barua kutoka Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu yenye Kumb.  Na. BSK/W/012/01 ya tarehe 22/5/2012 iliyoeleza kutoridhika na ufaulu wa  watahiniwa waliofanya somo la Islamic Knowledge kwa kuwa waliona  matokeo yaliyotangazwa hayakuwa na uhalisia wa uwezo wa wanafunzi.  Kutokana na barua hiyo, Serikali ilifanya uchunguzi kwa kuangalia mambo  yafuatayo:
• Kulinganisha alama za watahiniwa zilizojazwa katika vituo vya  usahihishaji mitihani na zile zilizohifadhiwa katika Kompyuta, yaani  database ya Baraza la Mitihani ili kubaini kama kuna tofauti yoyote; na
• Kulinganisha alama za somo la Islamic Knowledge zilizochakatwa na  Mfumo wa Kompyuta na sampuli ya alama zilizokokotolewa kwa kutumia  kikokotozi (calculator).
2.0 MATOKEO YA UCHUNGUZI
• Baada ya kupitia hatua za uhakiki kuhusu usahihishaji na utoaji wa  matokeo, ilibainika kuwa alama za mwisho katika somo la Islamic  Knowledge zilizokokotolewa na Mfumo wa Kompyuta ZILITOFAUTIANA na alama  zilizopatikana kwa kutumia kikokotozi. Uchunguzi zaidi uliofanyika kwa  lengo la kubaini chanzo cha tatizo katika uchakataji wa matokeo hayo
kwenye Mfumo wa Kompyuta ulionesha kuwa uchakataji uliotumika awali  kutoa matokeo ya mwaka 2012 ulitumia jumla ya “Paper” tatu kama  ilivyokuwa mwaka 2011.
1
• Kutokana na mabadiliko ya Fomati ya Mtihani wa somo la Islamic  Knowledge yaliyoanza kutumika rasmi katika Mtihani wa Kidato cha Sita  2012, mtihani huo kwa sasa una “paper” mbili na siyo “paper” tatu.  Hivyo, tofauti ya alama iliyobainika imetokana na Mfumo wa Kompyuta  kuendelea kutumia “paper” tatu katika kupata wastani wa alama za mwisho  badala ya kutumia “paper” mbili.
3.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI
• Baada ya kugundua dosari hiyo kwa somo la Islamic Knowledge, uhakiki  ulifanyika kwa masomo yao yote ya Mtihani wa Kidato cha Sita 2012  yaliyokuwa na “paper” zaidi ya moja ili kujiridhisha endapo uzito sahihi  ulitumika katika kupata wastani wa alama za watahiniwa. Matokeo ya  uhakiki huo yalionesha kuwa alama sanifu zilizokokotolewa na mfumo wa  kompyuta ni sawa na alama zilizokokotolewa na Kikokotozi. Hivyo hakuna  dosari yoyote iliyobainika katika masomo mengine.
• Matokeo ya somo la Islamic Knowledge yaliyotangazwa awali  yamerekebishwa kwa kutumia Paper mbili kama inavyotakiwa ili kuendana na  mabadiliko ya Fomati ya somo hilo. Marekebisho hayo yaliridhiwa na  Baraza la Mitihani katika Kikao chake Maalum kilichofanyika tarehe  31/05/2012. Aidha, Kikao kati ya wajumbe wa Baraza la Mitihani na  wawakilishi wa Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu kilifanyika tarehe  31/05/2012 ambapo walielezwa kuwa Wakuu wote wa Shule wenye watahiniwa  waliofanya somo la Islamic Knowledge wataandikiwa barua rasmi  kufahamishwa kuhusu marekebisho yaliyofanyika na barua hizo ziliandikwa  tarehe 01/06/2012. Pia walifahamishwa kuwa matokeo yao yote ya masomo  mengine hayana dosari yoyote na yanabaki kama yalivyotangazwa na Baraza  la Mitihani la Tanzania. Matokeo hayo yamewekwa kwenye tovuti ya Baraza  la Mitihani na pia yatatangazwa kwenye magazeti.
• Pamoja na marekebisho hayo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  itaunda Kamati ya wataalamu kuiwezesha serikali kujiridhisha zaidi na  hatua zilizochukuliwa na Baraza la Mitihani ili kuepuka dosari ya aina  hiyo isijitokeza tena kwa siku zijazo.
• Viongozi wa Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu waliridhika na hatua  zilizochukuliwa na Wizara na wameandika barua ya kuishukuru Wizara ya
2
Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu namna walivyoshughulikia malalamiko yao.
4.0 HATMA YA WANAFUNZI WALIOREKEBISHIWA MATOKEO KATIKA MAOMBI YA KUJIUNGA NA VYUO VIKUU
Wizara inapenda kuwahakikishia watahiniwa waliorekebishiwa matokeo yao  kwamba, kwa kuwa zoezi la usajili bado linaendelea hadi tarehe  30/06/2012, waliorekebishiwa matokeo yao watapata fursa ya kuwasilisha  maombi ya kujiunga na vyuo vikuu endapo wana sifa stahiki. Aidha, kwa  upande wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, maombi ya mikopo  hufanyiwa kazi rasmi baada ya Tume ya Vyuo Vikuu kukamilisha mchakato wa  udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu. Hivyo, hapatakuwa na athari  yoyote kwa watahiniwa husika kupata mikopo endapo watakidhi vigezo  vinavyotakiwa.
5.0 HITIMISHO
• Napenda kuhitimisha kwa kuwasihi wazazi, walezi, wanafunzi na jamii  kwa ujumla kuwa na imani na Baraza la Mitihani la Tanzania kama chombo  chetu chenye dhamana kisheria ya kuendesha mitihani nchini. Hapakuwa na  hujuma yoyote iliyofanyika kwa watahiniwa ambao matokeo yao  yamerekebishwa. Kosa lililojitokeza ni la kibinadamu, halikufanywa kwa  makusudi wala kwa lengo lolote la kuhujumu kundi fulani la watahiniwa.  Marekebisho yameshafanyika na matokeo stahiki yameshatolewa. Aidha,  uhakiki uliofanyika kwa masomo yao mengine unaonesha kuwa hakuna dosari  yoyote iliyobainika katika masomo yote.
• Kutokana na dhana ya baadhi ya watu kuwa kunakuwa na upendeleo kwa baadhi ya watahiniwa wa makundi fulani katika usahihishaji
napenda kuwakumbusha kuwa wakati wa mitihani, watahiniwa
huandika  namba  zao  za  mitihani  na  siyo  majina. Katika  taratibu  za
usajili wa Baraza la Mitihani hakuna kipengele chochote kinachomtaka  mtahiniwa kuonesha kabila yake, dini au itikadi ya kisiasa. Vilevile,  utaratibu unaotumika kuwapata wasahihishaji huzingatia uwezo wao  kitaaluma na uzoefu kazini. Aidha, katika fomu ya mapendekezo ya uteuzi  wa wasahihishaji hakuna mahali popote ambapo Mkuu wa Shule hutakiwa  kuonesha kabila yake, dini au itikadi ya kisiasa ya mwalimu
anayependekezwa kusahihisha mitihani.
• Utaratibu unaotumika kusahihisha mitihani hautoi mwanya wa upendeleo.  Katika kudhibiti uwezekano wa kupendelea mtu yeyote kila msahihishaji  husahihisha swali moja tu na kisha humpatia msahihishaji mwingine  asahihishe swali linalofuata. Aidha, kila msahihishaji hutakiwa kuweka  vifupisho vya majina yake (initials) ili ufuatiliaji uweze kufanyika  kadri itakavyohitajika. Pia uhakiki wa usahihishaji hufanyika kwa lengo  la kujiridhisha na usahihi wa kazi na kuhakikisha kuwa kila mtahiniwa  amepata alama anazostahili. Dosari zinazobainika zimekuwa zikirekebishwa  katika mchakato wa usahihishaji na wasahihishaji wanaobainika kuhusika  na dosari hizo wamekuwa wakichukuliwa hatua stahiki mara zinapobainika.
• Pamoja na hayo niliyoyaeleza nina taarifa kuwa yanapangwa maandamano  ambayo yanalenga suala hili hili la kutoridhika na matokeo ya awali ya  somo la Islamic knowledge. Kwa kuwa suala hili limeshapatiwa ufumbuzi,  nawasihi wananchi wajiepushe kushiriki maandamano hayo kwa sababu suala  la msingi lililo wafanya watake kuandamana limeshatolewa maelezo. Hivyo,  maandamano hayo hayatakuwa na tija.
IMETOLEWA NA DKT SHUKURU JUMANNE KAWAMBWA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAREHE 07/06/2012
                      -