BAADHI YA WANANCHI WAKISHANGAA BAADA YA FAINES KUZINDULIWA NA MTOTO MWENYE MIAKA KUMI ALIYEKABIDHIWA MIKOBA NA MAMA YAKE.
 BIBI NA MJUKUU WAKE WANAOSADIKIWA NI WACHAWI WAKIWA KATIKA GARI LA POLISI.
 FAINES AKIPAKIWA KATIKA GARI YA POLISI.

 FAINES ZAWADI-BINTI ALIYEFARIKI KWA MUDA NA KUREJESHWA DUNIANI AKIWA AMESHIKILIWA NA NDUGU ZAKE.
---
 Jeshi   la Polisi mkoani Kigoma limefanikiwa kuwaokoa watu watatu waliokuwa   wamezingirwa na kundi la wananchi wakitaka kuwaua kwa tuhuma za   kujihusisha na vitendo vya ushirikina.
 Kaimu   Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma SSP Joseph Konyo, aliwataja watu hao   waliokolewa kuwa ni Evania Sephanga(50), mkazi wa wilaya ya Kibondo,   Bruno January(46), mkazi wa kijiji cha Nyamhoza na mtoto mmoja mwenye   umri wa miaka kumi na mkazi wa kijiji cha Nyamhoza Kigoma mjini ambaye   jina lake linahifadhiwa.
 Kamanda   Konyo amesema kuwa wiki iliyopita majira ya saa tisa mchana, watu hao   walizingirwa na kundi hilo kwa madai kuwa walimroga na kumuua msichana   mmoja aitwaye Faines Zawadi(20) mkazi wa kijiji hicho cha Nyamhoza   ambaye siku moja kabla ya kifo chake alionekana kama mtu   aliyechanganyikiwa na kuwa kama kichaa.
 Alisema   katika tukio hilo, bibi kizee mmoja ambaye alikuwa mshirika wa kundi  la  waliodaiwa kuwa wachawi, alifanikiwa kutoroka katika mazingira ya   kutatanisha alipojifanya kuwa anakwenda kujisaidia.
 Kamanda   Konyo amemtaja bibi huyo aliyefanikiwa kutoroka kuwa ni Bibi Editha   Dosiyo mkazi wa kijiji hicho ambaye baadaye alipatikana na kuhojiwa   kabla ya kukabidhiwa kwa Idara ya ustawi wa jamii baada ya kuonekana   kuwa maisha yake yangekuwa hatarini.
 Amesema  baada ya  Polisi kupata taarifa za tukio hilo, walikimbia na kwenda  kuwaokoa  kutoka katika mikono ya kundi la wananchi lakini wakiwa  wameshaadhibu  ingawa ilikuwa haijawa kwa kiasi kikubwa.
 Habari  zinasema  kuwa, baadhi ya wananchi walipata taarifa kutoka kwa mtoto  aliyeokolewa  akisema kuwa baadhi ya watoto waliofariki kijijini hapo,  akiwataja  (majina tunayahifadhi) alikuwa akiwaona nyumbani kwao nyakati  za usiku  wakiosha vyombo na baadaye kupewa chakula.
 Walisema   mara baada ya bibi huyo kutoweka, mtoto huyo wa kiume ambaye ni   miongoni mwa waliozingirwa wakitaka kuuawa, aliamza kutekeleza maagizo   ya bibi huyo na alipomaliza kitendo cha kumruka kwa mara ya saba,   msichana yuyo ambaye alikuwa ni marehemu alizinduka na kuomba uji.
 Wamesema   msichana huyo ambaye alikuwa mfu, alipewa uji na kunywa kisha   akapelekwa hospitalini ambako hadi sasa hali yake inasemekana kuwa   inaendelea vizuri.
 Hata   hivyo Kamanda Konyo ametoa wito kwa wananchi kuacha kuchukua sheria   mkononi na badala yake watoe taarifa Polisi kwa kila jambo wanaloliona   kuwa linaweza kuleta uvunjifu wa amani ili hatua za haraka zichukuliwe   dhidi ya wahusika.
 Mwezi   uliopita watu wawili mke na mume, waliuawa na kundi la watu wenye   hasira kisha miili yao kuchomwa kwa moto mkoani Kigoma baada wa   kutuhumiwa kuwa walikuwa ni wachawi.