
 Makamu  wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akitoa salaam  za pole kwa viongozi na chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa   Mwanza katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu   Musobi Mageni 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad  akiweka udongo kwenye kaburi la   Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu  Musobi Mageni ,kulia kwake  ni Mwenyekiti wa Cuf Profesa ibrahim Lipumba ambao wote walijumuika  na viongozi na  chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa  Mwanza  katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu  Musobi  Mageni  
--
Makamu  wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad  amejumuika na  viongozi wa chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa  Mwanza katika  mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu  Musobi Mageni  huko kijijini kwao Ngudu, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
  Katika mazishi hayo, pia alihudhuria Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa   Ibrahim Lipumba, Makamu Mwenyekiti, Machano Khamis Ali, pamoja na   wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa, wakiwemo Waziri wa Afya   Zanzibar, Juma Duni Haji na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Haki za   Binaadamu, Salum Bimani.
  Marehemu Musobi alifariki Dunia Mei 30, mwaka huu nyumbani kwake Ngudu   baada ya kusumbuliwa na maradhi ya shinikizo na damu na sukari kwa muda   mrefu.
  Marehemu alihamia chama cha Wananchi CUF mwaka 1994 na kuchaguliwa kuwa   Mwenyekiti Taifa mwaka 1995 hadi 1999 alipostaafu na kubaki kuwa  Mjumbe  wa kudumu wa Baraza Kuu la Taifa na Mkutano Mkuu wa chama hicho  hadi  kifo chake.
  Katika uhai wake, marehemu aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na   Maendeleo Mijini kuanzia mwaka 1972 hadi 1975, mwaka 1976 hadi 1978   Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala Rajan Industries Ltd. Nafasi nyengine   ni alizowahi kushikilia ni Ubunge na Mkuu wa Wilaya katika wilaya ya   Chunya, Kahama na Muleba.
  Akitoa salamu za rambirambi, Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye pia ni   Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wakati   wa mazishi alisema, marehemu alikuwa kisima cha busara na mwenye hekima   kubwa na ndio maana viongozi wa CUF walikuwa wakikimbilia kwake kuchota   ushauri wake.
 “Huu ni msiba mkubwa sio tu kwa familia yake, bali kwa chama chetu na kwa serikali zote mbili”, alisema Maalim Seif. 
 Marehemu ambaye alizaliwa mwaka 1930, ameacha wajane wawili, watoto 15, wajukuu 28 na vitukuu sita. 
Na 
Khamis Haji
Ofisi Ya Makamu wa Kwanza Wa Rais Zanzibar