Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel  akishuka katika gari wakati alipofikishwa Mahakamani hapo..

 Mbunge wa  Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel akielekea katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
Mbunge  wa Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel akitoka Mahakamani huku akiwa  chini  ya ulinzi wa askari polisi baada ya kusomewa shtaka la rushwa ya  sh.  milioni moja kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya   Mkuranga, Jonathan Liana
---
  MBUNGE wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel (43) leo  amefikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,na  Taasisi ya  Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), kwa makosa ya rushwa  ya  shilingi Milioni moja toka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya  ya  Mkuranga,Jonathan Liana.
  Wakili  wa Takukuru, Janeth Machullia na Ben Lincoln walidai mbele ya  Hakimu  Mkazi Faisal Kahamba kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa  mawili ya  rushwa. 
  Wakili  Machullia alidai kuwa kosa la kwanza ni la rushwa kinyume na  kifungu  cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11  ya mwaka  2007, kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka huu katika maeneo  tofauti  jijini Dar es Salaam , Badwel akiwa ni Mbunge wa Bahi na Mjumbe  Kamati  ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) na wakati huo akiwa ni  ofisa wa  serikali kwa maana ya sheria ya Takukuru, alitenda kosa la  kushawishi  ili apewe rushwa ya jumla ya Shilingi milioni nane toka kwa  Sipora Liana  ili kiasi hicho cha fedha aweze kuwapelekea wajumbe  wenzake wa Kamati  hiyo ya Bunge ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha  ya mwaka 2011/2012  ya Halmashauri hiyo.
   Wakili  Machullia alidai shitaka la pili ni kwamba kati ya Juni 2  mwaka huu,  katika Hoteli ya Peacock,mshitakiwa akiwa na nyadhifa zake  zote hizo  alipokea rushwa ya Milioni moja kutoka kwa Liana ili aweze  kwenda  kuwashawishi wajumbe wa Kamati hiyo ili waweze kuipitisha ripoti  ya  fedha ya Halmashauri ya Mkuranga huku akijua kufanya hivyo ni kosa.  
  Hata  hivyo mshitakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea Mpare  Mpoki  alikanusha mashtaka yote na wakili wa Machullia alidai kuwa  upelelezi wa  shauri hilo umekamilika.
  Kwa  upande wake Hakimu Mkazi Kahamba alisema ili mshitakiwa apate  dhamana  ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja  atasaini  bondi ya shilingi milioni nne na kusalimisha hati zao za  kusafiria  mahakamani, sharti ambalo lilitimizwa na mshitakiwa huyo na  akapata  dhamana. Hakimu Kahamba ameahirsha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka  huu,  kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya  kuja  kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo.