(b). Kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh Doctor Ali Mohd Sheini kwa waandishi wa habari siku ya tarekhe 31/05/2012 ikulu mjini Zanzibar haikusimama katika kuzuiya Mihadhara, Makongamano wala Mikusanyiko ya aina yoyote bali ilisimama katika kulinda na kudumusha amani, tunampongeza Mh Raisi kwa hilo na hilo kwa kuwa amelitambua wazi ndilo lengo pamoja na dhamira ya Jumuiya yetu.
JUMUIYA YA UAMSHO NA MIHADHARA YA KIISLAMU(JUMIKI)
للجنة الدعوة الإسلامية
THE ASSOCIATION FOR ISLAMIC MOBILISATION AND PROPAGATION
P. O. BOX: 1266 -Tel: +255-777-419473 / 434145- FAX +255-024-2250022 E-Mail: jumiki@hotmail.com
MKUNAZINI ZANZIBAR
Afisi ya Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mjini/Magharibi,
Sanduku la Posts 237
Zanzibar.
KUH: KUZUILIWA KUFANYA MHADHARA WA AMANI KATIKA VIWANJA VYA LUMUMBA NA JESHI LAKO LA POLISI
Tafadhali rejea barua yako yenye kumb:RPHQ/MJN/58/VOL.V/59 ya tarekh  01, JUNE, 2012 ambayo ina kichwa cha maneno kuhusu Taarifa ya Mhadhara.
Jumuiya yangu imesikitishwa saana na hatua yako pamoja na Jeshi lako la  Polisi ya kutuzuilia kufanya mhadhara wa amani ambao kwa mujibu wa  Sheria za nchi ni haki yetu na imeonelea ikuandikie barua hii kwa kuwa  sababu ulizozitoa za kuzuiya mhadhara huo si za msingi wala si za  kisheria.
Baada ya kukaa pamoja na kujadili hoja ulizozitoa na zilizopelekea jeshi  lako kutuzuilia kufanya mhadhara huo wa amani tumeonelea kukuomba wewe  pamoja na jeshi lako la Polisi kuyazingatia mambo yafuatayo na tunaomba  majibu rasmi juu ya hayo-:
(a). Kwa mujibu wa vyanzo mbali mbali vya habari pamoja na magazeti ya  ndani ya nchi, aliyetoa amri ya kuzuiya kufanyika mihadhara,  makongamano, maandamano pamoja na mikusanyiko ya aina yoyote ni Waziri  wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Raisi ndugu Mohammed Aboud ambaye  kisheria hana nguvu juu ya hilo.
(b). Kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh Doctor Ali Mohd Sheini kwa waandishi wa habari siku ya tarekhe 31/05/2012 ikulu mjini Zanzibar haikusimama katika kuzuiya Mihadhara, Makongamano wala Mikusanyiko ya aina yoyote bali ilisimama katika kulinda na kudumusha amani, tunampongeza Mh Raisi kwa hilo na hilo kwa kuwa amelitambua wazi ndilo lengo pamoja na dhamira ya Jumuiya yetu.
(c). Barua yako uliyoitowa kwa Jumuiya yangu ya tarekh 01/06/2012 haisimami kunizuiliya kufanya na kuendelea na shughuli zangu za Mihadhara, Makongamano bali imesimama zaidi kunipa taaarifa juu ya Kauli ya Serikali ambayo kama nilivyokuelezea hapo juu imetolewa na mtu ambaye Kisheria hana nguvu za kufanya hivyo.
Kwa mantiki ya hoja nilizokuelezea hapo juu inaonekana wazi kuwa Jeshi lako la Polisi limeazimia kufanya uvunjifu wa amani pamoja na kufanya mauwaji kwa raia wasio na hatia, hii inatokana na kauli ya Jeshi lako katika barua uliyoniandikia ya kuwa jeshi lipo tayari kuzuiya kwa nguvu za aina zote mhadhara huo.
Napenda kukufahamisha kuwa kufanya mihadhara, makongamano pamoja na  Maandamano ya Amani katika nchi yoyote ile inayofuata Demokrasia ya  kweli ni kutii sheria na sio kuvunja sheria kama haya yanathibitishwa  katika Katiba zote, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba  ya Zanzibar, tafadhali rejea ibara ya 18 (a,b,c,d) na pia rejea ibara ya  20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia ibara ya  18(1) na 20(1).
Kutokana na maelezo hayo hapo juu, Jumuiya yangu bado inayofursa ya  kufanya Mihadhara pamoja na shughuli zake kwa kufuata Katiba ya nchi na  kufuata katiba ya Jumuiya iliyoitunga, hii ni kwa sababu mpaka sasa  haina ushahidi wowote wa Kimaandishi juu ya kuzuiliwa kufanya shughuli  zake.
Kwa kuwa Jumuiya yangu ni Jumuiya yenye lengo la kulkuza na kudumisha  amani katika nchi, viongozi wa Jumuiya wapo tayari kukaa chini pamoja  na viongozi wakuu wa Jeshi lako la Polisi kulijadili suala hili na  kulipatia ufumbuzi kabla ya madhara makubwa ya umwagaji wa damu ambayo  yameazimiwa kufanywa na Jeshi lako la Polisi yasije kutokea.
Kumbuka ni wajibu wa Jeshi la Polisi wanatakiwa wafanye kazi zao kama  wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa Polisi  unaosema kwamba polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza  amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu. Kila mtu anayo  haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya kitaifa na kimataifa  yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu.
Polisi wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu isipokuwa tu kwa minajil ya kulinda haki za wengine.
Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na kutetea haki za binadamu kwa watu wote.
WABILLLAH TAWFIQ
Natanguliza Shukrani
…………………………
ABDALLAH SAID ALI.
KATIBU MKUU.
JUMIKI.
Nakala:
MUFTI MKUU ZANZIBAR
IGP – Tanzania
CP – Zanzibar
RPC – Mjini Magharibi
RCO – Mjini Magharibi
OC FFU Mjini Magharibi
RSO – Mjini Magharibi
DC – Mjini Unguja.
DSO – Mjini Unguja.
Balozi mdogo wa Marekani Nchini Zanzibar
Vyombo vyote vya Habari