Freeman Aikaeli Mbowe | Mwenyekiti CHADEMA Taifa
MHESHIMIWA rais,
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba kakujalia afya njema tangu  ubebe jukumu kubwa la kutawala taifa hili. Naendelea kumwomba aendelee  kukujalia afya njema na akupe busara za kukabiliana na vikwazo  mbalimbali vya kulijenga taifa la Tanzania na akuepushe na nguvu yoyote  ya giza yenye azma ya kulibomoa.
Mheshimiwa rais,
Leo nimeamua kukuandikia waraka huu. Pengine utashangaa kama  watakavyoshangaa wananchi wako wengi unaowaongoza. Najua wengine  watahoji, iweje nikuandikie kupitia gazetini na isiwe moja kwa moja.  Sababu ni rahisi. Kwa kuandika gazetini, nina hakika itakufikia.
Wengine wanaweza kuona ni utovu wa nidhamu kuweka hadharani barua kwenda  kwa mtawala mkuu wa nchi. Katika mazingira ya kawaida, hii yaweza kuwa  kweli, lakini kwa mazingira na utamaduni uliojengwa na ofisi yako  sambamba na chama chako, rais wetu, unayeitwa “mtu wa watu”, uko radhi  kuonana kikazi au hata kistarehe na watu wengine wote isipokuwa viongozi  wenzako wa vyama vya siasa.
Hata hivyo nikiri, serikali yako, kama ilivyokuwa iliyokutangulia,  hukumbuka viongozi wa vyama vya siasa pale panapokuwepo ugeni wa  kimataifa, jambo lenye kawaida ya kuambatana na hafla ya ulaji na  unywaji Ikulu. Hapo, wapinzani huitwa kwa zamu kwenye ulaji na unywaji.
Aidha, unapokuwa kwenye ziara zako nje ya nchi, serikali yako imejijengea utamaduni wa kuwabeba “msukule” wabunge wa upinzani.
Wapinzani wanaoambatana na wewe hawana jukumu lolote wanalopewa zaidi ya  kuwa sehemu ya kundi kubwa la “watalii” wenye jukumu moja tu, la  kuhalalisha matumizi ya kodi za wananchi, kutambulishwa kwenye kila  kikao au mikutano kwa lengo la kujenga taswira chanya ya serikali yako.
Wengi hubebwa bila hata kujua madhumuni ya safari ni nini! Na wakirejea, biashara huishia pale uwanja wa ndege!
Yatokeapo maazimisho ya sherehe za kitaifa, wapinzani hukumbukwa. Hapa  ni kuwahadaa wananchi wakiwemo waandishi wa habari. Tutaonana Uwanja wa  Taifa kukuona ukikagua gwaride, kisha tutaachana pale, kusubiri sikukuu  nyingine ya kitaifa.
Ninaamini wengi wa viongozi na wabunge wa upinzani hukubali kushiriki  mambo haya kama ishara ya utayari wao na vyama vyao katika kujenga  utaifa wetu na si kwa ajili ya kingine chochote.
Hata hivyo nikiri, upande wa pili wa mchezo huu mchafu, ghafla  umedhoofisha wapinzani dhaifu na wabinafsi na umejenga taswira ya rushwa  ya kisiasa na kimaslahi. Mwaliko mmoja tu wa Ikulu au safari moja na  msafara wako au waziri mkuu, vimeweza ghafla kubadilisha misimamo ya  baadhi ya watu walioonekana awali kuwa makini katika kutetea maslahi ya  taifa.
Kila baya lina jema, utamaduni huu kwa upande mwingine unasaidia taifa hili kujua mchele ni upi na pumba ni zipi.
Naamini kwa dhati kabisa, nia ya serikali yako si njema, kwani ina  kusudio la kuwatumia wapinzani kama chambo, hasa mbele ya macho ya  viongozi wenzako wa nje, kujenga sura ya kinafiki kuwa ndani ya nchi  yetu, tuna mshikamano wa kisiasa.
Mheshimiwa rais,
Waraka wangu kwako leo unakusudia kukukumbusha jambo moja la muhimu  sana, ambalo napenda kuamini unalijua. Cha ajabu ni kwamba, kama  ungekuwa hulijui nisingesikitika. Lakini nasikitika kwa sababu naamini  unalijua, lakini pengine unalidharau.
Nikiri jambo moja. Kama kuna kitu kinaniweka kwenye siasa, si chuki  binafsi, si ajira na wala si cheo, bali ni ndoto yangu ya siku moja  kuona nimeshiriki mchakato wa kuistawisha nchi yangu, kwa pamoja na  mambo mengine, kujenga umoja wa kitaifa.
Hakuna jambo lolote la “neema” linalowezekana katika taifa  lililogawanyika. Si rahisi wote kuwa na fikra sawa, lakini ni rahisi kwa  asilimia zaidi ya 80 ya wananchi kuupenda, kujivunia na hivyo kuuulinda  utaifa wao. Hii haijalishi kama nchi ni maskini au tajiri. Hali hii  hata hivyo, haizuki. Hufanyiwa kazi, tena kimkakati.
Nasisitiza, sifa ya kwanza ya taifa lolote ni umoja wa utaifa wake.  Umoja wa kitaifa kamwe haujengwi na kundi lolote la kijamii ndani ya  nchi kama vile chama, dini au kabila. Hujengwa pale dhamira ya mtawala  inapowaongoza watu wake kuweka kama agenda kuu ya uongozi na dira ya  nchi msingi wa kuunganisha taifa bila kujali mipaka ya kiitikadi,  kidini, kikabila, kijiografia, kijinsia au rangi.
Baada ya kiongozi kujidhihirisha kwa fikra zake, huzitafsiri kuwa  dhamira ambayo huitoa kama kauli, si mara moja, bali kila fursa  itokeapo, kwani kwake ni sawa na sala. Ni uumini. Naye hatimaye  hukamilisha uumini wake kwa vitendo, tabia na mienendo yake ya kila  siku.
Ndiyo, watu na hususan viongozi watapingana kwa mengi ikiwemo mitazamo, lakini yote haya hayawi mapenzi yao kwa taifa lao.
Watalipenda, watajivunia na kamwe hawatalikimbia!
Mheshimiwa rais,
Dhuluma, nguvu na rushwa vinaweza kushinda uchaguzi, lakini haviwezi  kujenga umoja wa kitaifa. Umoja wa kitaifa kamwe haujengwi na fedha,  majeshi au mifumo ya kiusalama. Mifumo hii hujenga hofu na ukondoo!
Penye dhamira nzuri, kila jambo lililo kikwazo cha umoja wa taifa huwa  ajenda yenye kipaumbele kwa kiongozi yeyote anayestahili sifa ya kuwa  mtu wa watu kama ambavyo naamini ungependa. Kwa vyovyote vile,  hutafurahisha wote, lakini wenye kupenda haki katika maisha haya ni  wengi kuliko wenye kudhulumu na kuichukia haki.
Utawala ni kazi ngumu. Inahitaji uwezo wa kufikiri na kutafakari, ambao  nina hakika unao. Penye umoja wa kitaifa, hata baadhi ya maamuzi magumu  ambayo hayapendwi na wananchi huridhiwa.
Kiongozi makini lazima akubali lawama pale anaposimamia jambo ambalo  anaamini lina maslahi kwa taifa. Hali hii inamfanya kiongozi awe mkweli,  muwazi na asiyefanya mambo kwa kificho. Kiongozi mzuri ni lazima basi  kwa kiwango kikubwa atende yale anayoyahubiri.
Mheshimiwa rais,
Niruhusu nikukumbushe jambo moja, ambalo kwa mara nyingine, naamini  unalijua, lakini bado napata wakati mgumu kujua unalitafakari vipi. Hili  linamhusu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye baadhi ya wananchi  wako wameamua kukuita JK kama yeye.
Sikusudii kufungua ukurasa wa somo la Mwalimu, ila nakumbuka wakati wa  kampeni, wapiga debe wako wakuu, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na Mzee  Stephen Wassira – ambao vilevile leo ni mawaziri wako, walifanya mkutano  na waandishi wa habari wakidai sina haki ya kumzungumza Mwalimu kwenye  kampeni zangu, kwani wewe unamjua Mwalimu kuliko mimi!!
Dhamira nyoofu na kauli, vilivyoshabihiana na matendo, ndivyo viliyompa  Mwalimu jeuri, kujiamini, kupendwa, kuheshimika, kuogopwa, kusamehewa,  kuombewa na hatimaye leo, wengine (ndani ya imani yake) wanatafakari  uwezekano wa kumfanya mwenye heri na hatimaye mtakatifu.
MWALIMU ALIJENGA TAIFA!
Mwalimu, kama binadamu, alikuwa na makosa kadhaa ya kisera na hasa ya  kimaamuzi, hususan katika masuala ya baadhi ya sera za kiuchumi.
Aliongoza Tanzania wakati mgumu sana, lakini pamoja na umaskini ule,  kila alichofanya Mwalimu kililenga utaifa, Utanganyika na hatimaye  Utanzania wetu!
Mheshimiwa rais,
Tangu umeingia Ikulu, umezungumza mengi. Ndani ya nchi na hata nje.  Uzuri wa maendeleo ya kiteknologia, yanatusaidia sisi walalahoi kujua  wewe rais wetu umezungumza nini popote duniani.
Nimeona nivunje itifaki zote, niweze kukupongeza bila kificho chochote  mbele ya Watanzania wenzangu, kuhusu hotuba uliyoitoa bungeni Desemba 30  mwaka 2005, wakati ukizindua Bunge jipya baada ya uchaguzi.
Wengine wataendelea kushangaa! Mbona Mbowe anazungumzia mambo ya kale! Hapana!
Mheshimiwa rais,
Tangu umeingia Ikulu, hakuna maneno mazito, ya kizalendo, ya kiungwana  na yenye kutia matumaini ambayo ulishawahi kuyazungumza kama yale. Sifa  zote hizi nakupa kwa sababu moja tu: Hotuba ile ilijenga MATUMAINI YA  UTAIFA.
Mheshimiwa rais,
Hotuba yako ya kufungua ilikuwa ya kujiamini mno. Ilifurahisha wengi,  wakiwemo wa vyama vingine vya siasa. Uliamsha ari ya wananchi wako na  wengine tuliamini angalao kwa kipindi cha wiki chache kuwa, sasa mambo  huenda yatabadilika. Uliweza kuendelea kuwapagaisha wananchi na  kuwafanya “misukule” angalao kwa wiki kadhaa.
Kwa kumbukumbu zangu na ufahamu wangu mdogo wa kisiasa, mara ya mwisho  kusikia hotuba iliyogusa wengi kwa kiwango kile, ni wakati wa uhai wa  Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Mwalimu alitania kwenye hotuba zake,  lakini hukufanya utani, uzushi au masihara na kauli zake au yeyote  atakayekwaza dhamira yake na TAIFA lake!
Kwangu, ile ilikuwa dira ya taifa. Ilijenga hoja za msingi za utaifa  bila kujali zimetoka kwenye ilani ya CHADEMA, ya CCM au ya chama kingine  chochote.
Tunajua kipindi kile, ulikuwa umetingwa na mambo mengi sana ikiwepo  kushangaa, pengine kisirisiri, wingi wa kura zako pamoja na mshikemshike  tuliokupatia kwenye kinyang’anyiro. Busara za kawaida zitajua kuwa  ulikuwa unatafakari namna ya kuzawadia wale wote waliowezesha miujiza  ile kutokea. Ni dhahiri ulikuwa unatafakari namna ya kuunda serikali  yako. Naamini kipindi kile ulikuwa hujatulia na kupumzika.
Siku hiyo, nilikuwa ndani ya Ukumbi wa Bunge kama mwalikwa. Bado  nilikuwa na mimi natibu majeraha. Nilikusikiliza kwa makini na  kujisemea:
Hotuba ya mheshimiwa rais yaweza kuwa jibu la nchi yetu. Je, ameandika vipi hotuba nzuri kiasi hiki wakati ametingwa sana?
Nikakumbuka rais wangu una wasaidizi! Lakini nikajiuliza tena; basi rais  utakuwa na wasaidizi na washauri makini sana! Nikajiuliza umewapata  wapi ghafla? Kwani nilijiaminisha hawawezi kuwa wale wazee walionikebehi  bila haya eti “nisimtumie” Nyerere kwenye kampeni zangu!
Naam, hata kama umeandikiwa, kwa vyovyote umeipitia na kuikubali kwani  hata ulipokuwa unaisoma, uliisoma kwa kujiamini na hata kuongezea  mengine nje ya karatasi. Hivyo basi, lolote lililo ndani yake ni lako.  Napenda kuamini ilikuwa ni dhamira yako! Ni hadidu ya rejea ya miaka  mitano ya utawala wako!
Mheshimiwa rais,
Hotuba yako bado naiwaza na kuisoma mara kwa mara. Nina mengi ya  kukupongeza ndani yake na waraka huu mmoja hautoshi. Najua nawe una  majukumu mengi. Naomba uniruhusu niishie hapa kwa leo na wiki ijayo  niingie kuijadili hotuba yako kama walivyofanya wabunge wetu kule Dodoma  na mijadala yao ikabaki kwenye kumbukumbu za Bunge, ili zije kusomwa na  vizazi vya mbele.
Niruhusu mheshimiwa nifanye kazi hiyo ya kukukumbusha kauli zako  mwenyewe, kifungu kwa kifungu na namna ulivyotekeleza kwa vitendo, ahadi  zako. Nitakuchosha, lakini ndiyo wajibu na heshima yangu kwa utaifa  wetu!
Mheshimiwa rais,
Naomba kutoa hoja…
                      -