
 Makamu  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,  akimkaribisha Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Mhe. Amour Zacarias  Kupela, wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam leo  Juni 05, 2012 kwa ajili ya kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake  nchini.

Makamu  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,  akizungumza na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Mhe. Amour Zacarias  Kupela, wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam leo  Juni 05, 2012 kwa ajili ya kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake  nchini. Picha na Muhidin Sufiani-Ofisi ya Makamu wa Rais
--

Makamu  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal  leo Jumanne ya Tarehe 05 Juni 2012 amekutana na Mabalozi wa nchi za  Sudan na Msumbiji waliomtembelea ofisini kake Ikulu jijini Dar es  Salaam.
Balozi  wa kwanza kufika alikuwa Balozi wa Sudan nchini Tanzania Mheshimiwa  Dkt. Yassir Mohamed Ali ambaye amekutana na Makamu wa Rais kwa mara ya  kwanza na katika kujitambulisha kwake akaelezea nafasi ya Tanzania  katika kuhakikisha Bara la Afrika linabakia kuwa na amani na utulivu.
Balozi  Mohammed alimwambia Makamu wa Rais kuwa wafanyabiashara kutoka Sudan  wamekuwa wakishiriki katika uwekezaji nchini na bado wapo ambao wana nia  ya kufanya hivyo na kwa kuanzia wafanyabiashara hao watashiriki katika  maonyesho ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Saba Saba  yatakayofanyika mwaka huu. Balozi huyo alieleza pia kuwa, Sudan  inadumisha uhusiano wake na Tanzania katika kuhakikisha nchi mbili  zinabakia kuwa na lengo moja kubwa la kuwapatia wananchi maendeleo. 
Kwa  upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais, yeye alimkaribisha Balozi  Mohammed na kumwahidi kuwa Tanzania itazidi kutumia nafasi yake katika  kuhamasisha amani hasa sasa ambapo nchi ya Sudan iko katika mgogoro na  Sudan ya Kusini.
Balozi  Amour Zacarias Kupela wa Msumbiji, yeye sambamba na kumuaga Mheshimiwa  Makamu wa Rais alimwambia kuwa amefurahi sana kuwepo nchini Tanzania na  kwamba anaithamini nchi hii kama nyumbani kutokana na uwezo wake wa  kudumisha amani na pia kwa nafasi yake katika kuhakikisha wananchi wa  Msumbiji wanakuwa huru na wanaishi kwa amani kama ilivyo sasa.
Balozi  huyo alisema serikali ya Msumbiji inatumia fursa zake za kuhakikisha  inakuza kilimo ili kutoa nafasi ya kuwepo chakula cha kutosha nchini  humo na
pia  akafafanua kuwa hali ya kisiasa nchini mwake kwa sasa ni shwari na  hivyo wananchi wa ajukumu moja tu la kujitafutia maendeleo.
Balozi  Maricias alifafanua kuwa upo umuhimu wa kukuza nafasi za kubadilishana  wanafunzi kati ya Msumbiji na Tanzania kwani kama haitafanyika hivyo ni  rahisi wananchi wa nchi hizi kusahau historia ya namna nchi hizi mbili  zilivyoshirikiana katika kipindi cha kupigania uhuru.
Makamu  wa Rais alimueleza Balozi Maricias kuwa, Tanzania inashukuru sana kwa  mchango wake alioutoa kama Balozi na pia katika kazi alizofanya kabla ya  kuwa Balozi. Alimtakia kila la kheri katika kazi zake mpya huku  akimhakikishia kuwa Tanzania itabakia na mahusiano chanya na Msumbiji  katika kipindi chote.
 Imetolewa: 
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
DAR ES SALAAM