1.0       UTANGULIZI:
 Mkutano  wa Nane wa Bunge unatarajiwa kuanza tarehe 12 Juni, 2012 na kumaliza  shughuli zake tarehe 22 Agosti, 2012. Mkutano huu utakuwa na shughuli  mbalimbali kama vile Kiapo cha Utii kwa Waheshimiwa Wabunge wateule,  kujadili Makadirio ya matumizi na mapato ya serikali kwa mwaka wa fedha  2012/2013, Maswali kwa Waziri Mkuu na Maswali ya kawaida pamoja na  chaguzi mbalimbali ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi baada ya uteuzi wa  Mheshimiwa Rais kwa baadhi ya wabunge kuingia katika Baraza la  Mawaziri.
2.0         MUDA WA MKUTANO WA NANE WA BUNGE:
Kanuni  ya 97(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Mwaka 2007, imeweka kiwango cha  juu cha siku zitakazotumika kwa ajili ya mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya  Serikali kuwa ni siku tano. Pia, Kanuni ya 99(1) imeweka kiwango cha  siku zisizozidi hamsini kwa ajili ya Bunge kujadili utekelezaji wa  Wizara zote za Serikali.
Hivyo  basi katika Mkutano huu wa Nane jumla ya siku nne (4) zimetengwa kwa  ajili ya kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, na jumla siku  aronbaini (40) zimetengwa kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa Bajeti ya  Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara nyingine zote.
3.0    SHUGHULI ZA SERIKALI:
Kwa  mujibu wa Kanuni 17 (1) (d) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007,  Shughuli ambazo zitatekelezwa katika Mkutano huu utakaokuwa wa siku 49  za kazi ni kama ifuatavyo:
3.1.      KIAPO CHA UTII:
Kwa  mujibu wa Kanuni ya 24 ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007 na kufuatia  uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Ibara ya 66 (1) (e) kutakuwa na kiapo cha Utii kwa Wabunge wateule  wafuatao:-
1.    Mhe. James Francis Mbatia;
2.    Mhe. Janet Zebedayo Mbene;
3.    Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo; na
4.    Mhe. Saada Mkuya Salum.
3.2       Miswada ya Sheria:
Miswada ya Sheria itakayosomwa kwa Mara ya Kwanza na hatua zake zote: [Chini ya Kanuni ya 83 ya Kanuni za Bunge] ni kama ifuatavyo:
·         Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2012 (The Finance Bill, 2012).
·         Muswada Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka2012 (The Appropriation Bill, 2012).
3.3       Kujadili Bajeti:
Majadiliano  ya Bajeti ya Serikali yanaongozwa na Kanuni zilizopo katika Sehemu ya  Tisa ya Kanuni za Bunge inayohusu Utaratibu wa Kutunga Sheria kuhusu  mambo ya Fedha. Kanuni ya 96(2) inaelekeza kuwa Hotuba ya Bajeti  lazima iwasilishwe Bungeni na Waziri wa Fedha kabla ya tarehe 20 mwezi  Juni kwa kila Mwaka.
Kutokana  na kanuni hiyo, Bajeti  ya  Serikali  itasomwa  siku  ya  alhamisi   tarehe  14 Juni 2012 ambapo Nchi zote za Afrika Mashariki zitasoma  Bajeti zao kama ambavyo walisha kubaliana.
Katika  siku hiyo baada ya kipindi cha Maswali, Waziri anayehusika na Mipango  atawasilisha na kusoma hotuba yake ya Hali ya Uchumi wa nchi na jioni  kuanzia saa 10.00 Waziri wa Fedha atasoma Hotuba ya Bajeti ya Serikali.
Kutokana  na Utamaduni wetu baada ya kusoma Bajeti hiyo Bunge litaahirishwa kwa  siku moja kwa lengo la kuwapatia Wabunge nafasi ya kusoma na kutafakari  Hotuba ya Hali ya Uchumi na Hotuba ya Bajeti ya Serikali na kujiandaa  kwa majadiliano yatakayoanza tarehe 18 Juni, 2012 hadi tarehe 21 Juni,  2012.
Kwa  Mujibu wa Kanuni ya 98 (2) Siku ya Alhamisi tarehe 21 Juni, 2012, Bunge  litapiga kura ya uamuzi wa Bajeti ya Serikali. Siku hii ni muhimu sana  kwa Wabunge wote kuwa Ukumbini kwa sababu kura hupigwa kwa kuita majina.
Tarehe  22 Juni, 2012 Bunge litajadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha  wa Mwaka 2012 (The Finance Bill, 2012). Tarehe 25 hadi 29 Juni, 2012 kwa  muda wa siku tano kutakuwa na mjadala wa Hotuba ya Waziri Mkuu juu ya  utekelezaji wa Shughuli za Serikali katika Mwaka wa Fedha unaomalizika,  na matarajio ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha unaofuata. Mjadala wa Hotuba  za Mafungu ya Wizara nyingine utaanza tarehe 02 Julai, 2012 kwa  mtiririko kama unavyoonekana kwenye ratiba hadi tarehe 20 Agosti, 2012.
4.0       SHUGHULI NYINGINE:
      4.1    MASWALI:
      (i)         Maswali ya Kawaida:
(Chini ya Kanuni ya 39(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007):
Itakumbukwa  kuwa, nyakati za vikao vya Bajeti, Maswali yanayowekwa kwenye orodha ya  Shughuli za Bunge ni kumi tu kwa siku za kawaida na matano siku za  Alhamisi, Hivyo, katika Mkutano huu inatarajiwa kuwa, Maswali 454  yataulizwa na kujibiwa.
(ii)        Maswali kwa Waziri Mkuu:
(Chini ya Kanuni ya 38(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007):
Utaratibu  wa kumuuliza Maswali Mheshimiwa Waziri Mkuu kila Alhamisi kama  tulivyokubaliana utaendelea na inakadiriwa kuwa maswali yasiyopungua 64  yataulizwa.
4.2       UCHAGUZI WA MWENYEKITI WA BUNGE:
Kwa  mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007  kutakuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge  ili kujaza nafasi  iliyoachwa wazi na Mheshimiwa George Boniface Simbachawene (Mb)  aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati  na Madini.
4.3.      UCHAGUZI WA MJUMBE WA BUNGE LA AFRIKA:
Kwa  mujibu wa Kanuni ya 12 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007  kutakuwa na uchaguzi wa mjumbe wa Bunge la Afrika ili kujaza nafasi  iliyoachwa wazi na Mheshimiwa Stephen Julius Massele (Mb) aliyeteuliwa  na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini.
Imetolewa na :
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma
na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM
Tarehe 8, Juni, 2012