Kufuatia Wizara ya Maji kukaa kimya bila kujibu barua toka Ofisi ya   Mbunge kwa zaidi ya mwaka mmoja, nimeamua kuchukua hatua za kibunge kwa   kuwasilisha kwa Katibu wa Bunge, taarifa na maelezo ya hoja binafsi   kutaka Bunge, katika mkutano unaotarajiwa kuanza tarehe 12 Juni 2012,   lipitishe maazimio ya kuwezesha uwajibikaji wa Wizara husika na mamlaka   zake katika kushughulikia masuala ambayo nimeyaeleza katika hoja  husika.
Ikumbukwe  kwamba, tarehe 20 Mei 2012 nilitoa mwito kwa Waziri Profesa  Jumanne  Maghembe kuueleza umma hatua saba za haraka zaidi za Wizara ya  Maji  kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka  katika  Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam mara baada ya Waziri  kurejea  ofisini kutoka katika ziara hiyo ya vyanzo vya ruvu juu na ruvu  chini na  kufanya mikutano na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka  (DAWASA) pamoja  na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).
Nilichukua hatua  ya kutoa taarifa kwa umma baada ya Wizara kuwa na  utendaji mbovu wa  kutojibu barua ambapo katika kipindi cha kati ya  mwaka 2011 mpaka 2012  nimeandika jumla ya barua nne kwa Wizara husika  kwa niaba ya wananchi  kwa nyakati mbalimbali bila kupata majibu yoyote.
Katika ya hatua  hizo ambazo Waziri nilieleza anapaswa kuzisimamia  katika Wizara ya Maji  ni; Mosi,  kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa  ya taifa ya kati ya  mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza  Mradi wa ukarabati na  upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka  Jijini Dar es salaam na  maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam  Water Supply and Sanitation  Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6  hata hivyo mpaka sasa katika  maeneo mengi mtandao wake maarufu kama  mabomba ya wachina hautoi maji.
Pili;  kuwasilisha  bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za  Majisafi na  uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam  uliopitishwa mwezi  Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa  bajeti kamili ya  utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013  na kusimamiwa  ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla  za kwenye  ziara.
Tatu; Waziri kueleza hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia  ziara yake  kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji  ulionza  kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia  Juni  2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika  Oktoba  2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu  katika  maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.
Nne;  Waziri kukubaliana na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati  mbalimbali  la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi  wa thamani  ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa  ukarabati na  upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar  es salaam na  maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply  and Sanitation  Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi  (technical Audit)  uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
Tano; Waziri  kuhakikisha Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye  ukaguzi wa kiufanisi  (performance audit) wa miradi ya visima vya maji  takribani 200 ambavyo  vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa  DAWASCO, jumuiya za wananchi  na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma  inavyostahili kwa kadiri ya  malengo ya awali. Aidha, Wizara ya Maji  ihakikishe EWURA inaharakisha  kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na  bei ya huduma ya maji kwa upande  wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es  Salaam.
Sita; Waziri  kuwezesha Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya  ukaguzi wa ufanisi  kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo  ya mijini  (performance audit report on the management of water  distribution in  urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kabla  ya mkutano wa nane  wa bunge ulipangwa kuanza tarehe 12 Juni 2012 ili  maoni na mapendekezo  yazingatiwe wakati wa mchakato wa bajeti.
Saba; Wizara ya Maji  kuhakikisha Serikali inawasilisha kwenye mkutano  wa tisa wa bunge  muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali  za majisafi na  majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous  Amendment Bill) ili  kushughulikia upungufu uliojitokeza katika  utekelezaji wa sheria  zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa  sekta ya maji nchini.
Imetolewa Dar es salaam tarehe 8 Juni 2012 na:
John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
                      -